Na Ashrack Miraji – Michuzi blog
Mkuu wa Wilaya ya Same, Mhe. Kasilda Mgeni, ameonesha kukerwa na usimamizi wa mradi wa maji unaotekelezwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) katika Kata ya Kisiwani, wilayani humo. Licha ya serikali kutoa shilingi milioni 720 kwa ajili ya mradi huo, bado haujanufaisha walengwa, huku ikidaiwa kuwa baadhi ya wananchi wamejiunganishia maji kinyemela.
Hali hiyo imebainika wakati wa kikao na wananchi wa kijiji cha Kisiwani Barazani kilichopo kata ya Kisiwani ambapo msimamizi wa mradi alishindwa kutoa maelezo ya maswali yaliyoulizwa kaktika mkutano huo kuhusu gharama za mradi, idadi ya walengwa, na hatua zilizochukuliwa dhidi ya waliojiunganishia maji kinyemela. Kushindwa kwake kujibu maswali hayo kuliibua maswali mengi mbele ya Mkuu wa Wilaya, Kamati ya Usalama ya Wilaya, Mkurugenzi wa Halmashauri, wataalamu, na wananchi waliohudhuria mkutano huo.
Mhe. Kasilda Mgeni alieleza kutoridhishwa na hali hiyo, akisema kuwa ni jambo lisilokubalika kwa msimamizi wa mradi kushindwa kueleza thamani ya fedha zilizotolewa, watu waliopaswa kunufaika, na maendeleo ya mradi huo.
“Yaani kimsingi umenichefua! Kama hii kazi huitaki, sema, kuna watu wanashida na hizi kazi. Mama Dkt. Samia Suluhu Hassan ameleta milioni 720 hapa, na RUWASA ndio mmepewa jukumu la kuutekeleza. Thamani ya hela mliyoletewa hujui, ulilenga kunufaisha watu wangapi hujui! Hapa lazima hatua kali zichukuliwe. Haiwezekani watu wanapewa mradi mkubwa wa milioni 720, halafu mwisho wa siku maji hayatoki, wala hawajali! Hawajui wananchi wangapi wanapaswa kuhudumiwa na huo mradi, hawajui!” Amesema Mhe. Kasilda.
Aidha, amewataka wananchi waliounganisha maji kinyemela kutoka kwenye mradi huo kujisalimisha kabla ya kuchukuliwa hatua kali za kisheria. Pia, amewaagiza wenyeviti wa vijiji na watendaji wa kata kufuatilia na kuwabaini wote waliohusika na vitendo hivyo ili wachukuliwe hatua.
“Waliojiunganishia maji, niwaombe mjisalimishe kabla hamjakamatwa. Ninyi mnafanya wenzenu wakose maji. Ninyi ni wezi kama wezi wengine wanaoiba mali za umma. Hii ni haki ya wananchi wote, si ya wachache wanaochukua kwa ujanja. Hatutavumilia hali hii, na hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wote waliohusika.”
Mhe. Kasilda ameagiza RUWASA kutoa maelezo ya kina kuhusu matumizi ya fedha za mradi, idadi ya walengwa, na hatua zitakazochukuliwa ili kuhakikisha maji yanawafikia wananchi waliokusudiwa.
Mradi huo wa maji katika Kata ya Kisiwani ulilenga kunufaisha jumla ya wananchi 3,150 na gharama halisi ya mradi ni milioni 722,208,335, lakini hadi sasa haujafanikisha malengo yake kutokana na changamoto za usimamizi wa mradi huo.