Unguja. Wananchi 10,270 wamepatiwa boti za kuendeshea kilimo cha mwani kati ya hao 5,389 vijana, 3,159 wanawake na 1,722 wanaume, boti hizo zimetolewa kupitia programu ya Uviko-19.
Pia, kupitia programu hiyo, Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi ilitoa mafunzo kwa wakulima wa mwani 7,300 kuhusiana na namna bora ya kufanya shughuli zao ambao zaidi ya asilimia 80 ni wanawake.
Hayo yamebainishwa na waziri wa wizara hiyo, Shaaban Ali Othman leo Februari 26,2025 kwenye Baraza la Wawakilishi wakati akijibu swali la Mwakilishi wa Mwanakwerekwe, Ameir Abdalla Ameir.
Mwakilishi huyo, alitaka kutambua ni kwa kiasi gani wizara ya uvuvi inatoa hamasa, elimu na miongozo kwa wananchi kuzitambua fursa lukuki za matumizi ya bahari na kwa vipi wizara inalichukulia kwa umakini suala la usawa wa kijinsia katika mnyororo wa thamani wa mazao ya uvuvi.
Pia, alitaka kufahamu ni kwa kiasi gani watu wenye mahitaji maalumu wanakuwa wanufaika wa fursa za uchumi wa buluu.
Akijibu hoja hiyo, Waziri Shaaban amesema wizara hiyo imekuwa ikifanya jitihada kadhaa za kuhakikisha inatoa elimu pamoja na hamasa kwa wananchi kuweza kuzitambua fursa zinazopatikana katika matumizi ya bahari.
Amesema, kuanzia mwaka 2020/24 jumla ya programu 350 za uelewa juu ya dhana ya uchumi wa buluu na kuelezea fursa za matumizi endelevu ya bahari zimefanyika kupitia mikutano, makongamano, warsha na vipindi katika vyombo vya habari.
“Kupitia programu ya Uviko-19 wizara imewawezesha wavuvi na wakulima wa mwani kwa kuwapatia boti na vifaa vyake, jumla ya wananchi 10, 270 walipatiwa boti za kuendeshea kilimo cha mwani kati ya hao 5,389 vijana, 3,159 wanawake na 1,722 Wanaume,” amesema Shaaban.
Hata hivyo, amesema wizara hiyo imejizatiti kutoa huduma kwa wananchi wote wenye mahitaji maalumu na milango yake iko wazi kwa wote wanaohitaji msaada au taarifa kuhusu fursa zinazopatikana katika sekta ya bahari.
Pia, amesema wizara imelipa kipaumbele suala la kijinsia katika utekelezaji wa shughuli zake za kuwawezesha wananchi, kwani imetoa boti 500 za kuendeshea kilimo cha mwani na mashine zake kwa kinamama wanaojihusisha na ukulima wa zao hilo.
Sambamba na hayo, wizara hiyo inatekeleza mpango mkakati wa (Zanzibar Blue Economy Gender Strategy and Action Plan 2022), ambao unakusudia kuwawezesha wanawake kunufaika na fursa za uchumi wa buluu katika mnyororo wa thamani wa mazao ya baharini.
Waziri Shaaban amesema, wizara hiyo haikuwaacha nyuma watu wenye mahitaji maalumu katika utekelezaji wa shughuli zake za uchumi wa buluu na tayari wameshanufaika kupitia programu ya Uviko-19.
Vilevile, Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji inaendelea na usajili wa watu wenye mahitaji maalumu, kwa lengo la kuwezeshwa mara tu fursa mpya zinapotokezea ili waweze kunufaika nazo.
Akiuliza swali la nyongeza, Mwakilishi Ameir alitaka kufahamu kwa kiasi gani wizara hiyo inashughulika na utatuzi wa changamoto za mwingiliano wa watumiaji wa rasilimali ya maji ya bahari ikiwemo wavuvi na wakulima wa mwani, wachimbaji wadogo wa chumvi na wahifadhi wa mikoko ili kutoathiri miradi ya kimkakati ya uchumi wa buluu.
Akijibu hilo, Waziri Shaaban amesema wizara hiyo kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) imekamilisha uandaaji wa mwongozo wa mpango wa matumizi ya bahari (Marine Spatial Planning) na kuchapishwa katika tovuti ya Makamu wa Rais wa SMT.
Pia, Serikali imefanya majaribio ya upangaji wa maeneo ya bahari katika eneo nambari tatu na nambari tano la hifadhi ya bahari ya PECCA Kisiwani Pemba.
Amesema, Serikali ipo katika hatua za mwisho za kutafuta mshauri elekezi ili kuandaa mkakati wa mawasiliano wa mpango mahususi wa matumizi bahari (Communication strategies for Marine Spatial Plan).
Ameeleza, mipango yote hiyo ni kuhakikisha inashughulika na utatuzi wa changamoto za mwingiliano wa watumiaji wa rasilimali ya maji bahari ikiwemo wavuvi na wakulima wa mwani, wachimbaji wadogo wa chumvi na wahifadhi wa mikoko.