Tarime. Serikali mkoani Mara imeunda kamati ya kutafuta suluhisho la kudumu la mgogoro wa ardhi kati ya wakazi wa kijiji cha Korotambe kata ya Mwema na kijiji cha Nyabichune Kata ya Regicheri wilayani Tarime.
Miongoni mwa athari zilizotokana na mgogoro huo hivi karibuni ni watu watatu kujeruhiwa kwa kukatwa mapanga na ng’ombe kadhaa kukatwakatwa mapanga kati ya Februari 6 na 18, 2025.
Kamati hiyo imepewa wiki mbili kuanzia jana Jumanne Februari 25, 2025, inahusisha wataalamu wa ardhi, wazee wa mila na mashuhuri yenye jukumu la kuwatambua na kuwabaini wamiliki wa maeneo katika eneo hilo, lenye mgogoro uliodumu kwa zaidi ya miaka 30 hali iliyosababisha kuwepo kwa mapigano ya mara kwa mara yaliyosababisha vifo vya watu na uharibifu wa mali.
Majukumu mengine ni kutambua mpaka kwa mujibu wa ramani ya wizara ya ardhi pamoja na kutambua mpaka maarufu kwa jina la Ingram uliotumiwa na Mjerumani katika maeneo hayo kabla nchi haijapata uhuru.
Akizungumza katika mkutano na wananchi wa maeneo hayo jana Jumanne baada ya kutembelea eneo lenye mgogoro, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Evans Mtambi amesema baada ya kamati kufanya kazi hiyo Serikali ya mkoa huo itatoa uamuzi kulingana na matokeo kwa kuwa lengo ni kutafuta suluhisho la kudumu na sio ugomvi.
“Nyie hapa ni ndugu kabisa tofauti yenu ni kwamba kuna wa ukoo wa Wakira na wengine ni kutoka ukoo wa Wanchari ni ajabu sana watu wa kabila moja kupigana na kuuana kisa mnatoka koo tofauti, niwahakikishie Serikali haina mpango wa kuchukua ardhi hii isipokuwa inataka kuona inatumika kuwaletea maendeleo lakini kwa amani,” amesema.

Baadhi ya wakazi wa vijiji vya Korotambe na Nyabichune wilayani Tarime wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Mara Evans Mtambi (hayupo pichani) kuhusu mgogoro wa ardhi baina ya wana vijiji hao. Picha na Beldina
Amesema umefika wakati wakazi wa Tarime na Mkoa wa Mara kwa ujumla kuachana na vitendo vya kukatana mapanga pale wanapotofautiana kwa maelezo kuwa vitendo vimepitwa na wakati.
“Jambo linalotokea hapa halifurahishi hata kidogo ni baya sana labda niwaambie tu hakuna sifa ya kuua watu na hakuna utajiri unaopatikana kwenye ardhi iliyomwaga damu, zaidi mnachuma laana tu, badilikeni ndugu zangu tujifunze kutafuta majibu ya changamoto zetu kwa njia sahihi na sio kumwaga damu,” amesisitiza.
Mtambi pia ametumia nafasi hiyo kuwakemea watu wanaotuhumiwa kuhusika kuchochea mgogoro huo wakiwamo wanasiasa. “Nawahakikishia Serikali haitamvumilia mtu yeyote anayesababisha watu kuuana na kujeruhiwa.”
Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Edward Gowele amesema baada ya kuibuka mapigano kati ya Februari 6 na 18 mwaka huu alifanya mkutano na wakazi wa eneo hilo kwa ajili ya kurejesha utulivu, huku jitihada zikifanyika ili kupata suluhisho la kudumu.
“Tulibaini kuna mkanganyiko wa mpaka katika eneo hili, lakini pia kuna hati tatu ambazo zinaonekana umiliki wake una utata tayari hatua zimechukukiwa ili kubaini ukweli, pia nimeagiza kusitishwa kwa shughuli za kilimo hadi pale tutakapomaliza uchunguzi wetu na kuja na majibu sahihi,” amesema Gowele.
Baadhi ya wakazi wa vijiji vya Nyabichune na Korotambe wamesema mgogoro huo wa miaka mingi ni lazima uishe ili waweze kuwa na amani na kufanya shughuli zao kwa utulivu.
“Shida kubwa hapa ni kukosekana kwa ukweli, wapo watu wanaopindisha ukweli kwa masilahi yao, tunamshukuru mkuu wa mkoa kuingilia kati tunaamini hili jambo sasa litafika mwisho,” amesema Chango William.
Amesema kuwepo wa migogoro wa mara kwa mara katika eneo hilo kumesababisha wakazi hao kuishi kwenye umasikini kutokana na wengi wao kupoteza mazao na mifugo kila kunapoibuka migogoro na mapigano. “Migogoro hiyo husababisha mazao kufyekwa mashambani na mifugo kukatwa mapanga na kuchomwa moto.
“Watu wengi sana wameuawa kwa kukatwa katwa mapanga au kuchomwa mishale ,tumechoka hali hii tunaomba kamati iliyoundwa ifanye haraka ili suluhu ipatikane,” amesema Makabe Mtatiro.