Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt Peter Kisenge ameishauri Jamii ya Tanzania kuhakikisha inakula vyakula bora hasa vile vyenye protini, wanga na matunda kwa kiasi kikubwa pia ikiwemo matumizi ya mafuta ya nafaka kama vile alizeti na mahindi sambamba na kuacha uvutaji wa sigara na unywaji wa pombe kwa kiasi kidogo ili kuepukana na magonjwa yasiyoambukiza kwani zaidi ya watu Milioni 17 hupoteza maisha kwa magonjwa yasiyoambukiza huku katika vifo hivyo vingi vikichangiwa na magonjwa ya moyo .
Dkt Kisenge amesema hayo Jijini Dodoma Februari 26,2025 wakati akizungumza na waandishi wa habari alipokuwa akielezea mafanikio ya Taasisi hiyo ya JKCI kuelekea Maadhimisho ya miaka minne ya Serikali ya awamu ya sita.
Na kuongeza kuwa kitu ambacho ni rahisi na kisicho na gharama ni ufanyaji wa mazoezi ambapo ameshauri kila mwananchi ambaye hana changamoto ya afya miguu kuhakikisha anatembea japo kwa nusu saa mara tatu ka wiki kwani kwa kufanya hivyo mtu anajihakikishia kuishi maisha marefu lakini pia kutopata magonjwa yasiyoambukiza.
“Magonjwa yasiyoambukiza yanaongezeka kwa kasi,kwani zaidi ya watu Milioni 17 hupoteza maisha yao na magonjwa ya moyo yanayochangia vifo vingi katika magonjwa hayo yasiyoambukiza”.
“Kwahiyo niwaombe wananchi wanaonisikiliza sasa wahakikishe wanakula vyakula bora hasa vile vyenye protini,wanga na matunda kwa wingi na kutumia mafuta zaidi yale ya nafaka kama alizeti na mahindi pia waepuke sana kutumia mafuta ya wanyama,waache uvutagi wa sigara,wanywe pombe kwa kiasi kidogo,kwani imeshauriwa usizidi uniti 3 au 4 kwa wanamama na uniti 4 kwa wanaume ili uweze kuishi maisha marefu “.
“Lakini kitu ambacho ni kirahisi na hakina gharama ni kufanya mazoezi,hebu kila mwananchi ambaye hana matatizo ya miguu atenge muda wa kutembea japo nusu saa mara tatu kwa wiki,kwani kwa kufanya hivyo una uhakika kuishi maisha marefu lakini pia unakuwa na uhakika wa kutopata haya magonjwa yasiyoambukiza”.
Mbali na hayo Dkt Kisenge amesema katika utekelezaji wa uboreshaji wa huduma za afya mtambo wa kuzalisha hewa ya oksijeni uliogharimu Shilingi Milioni 526,604,116 umefungwa katika Hospital ya Dar Group pia mtambo mwingine wa kuzalisha hewa ya oksijeni wenye thamani ya Shilingi Bilioni 1.3 umefungwa katika Taasisi ya moyo ya Jakaya Kikwete ambapo mitambo hii inatumika kusambaza hewa ya oksijeni kwa wagonjwa wenye uhitaji na kupunguza gharama za kununua Mitungi ya oksijeni kama ilivyokuwa hapo awali.
Aidha Dkt Kisenge ameeleza kuwa wagonjwa waliofanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo wa kufungua kifua na kubadilishwa Valvu za moyo moja hadi tatu,upasuaji wa kupandikiza mishipa ya damu ya moyo,upasuaji wa mishipa ya damu na mapafu walikuwa 2,784 ambapo kati yao watu wazima ni 1,880 na watoto ni 904.
Pia ameongeza kuwa utoaji wa huduma bora na za kisasa za matibabu ya moyo kumezifanya nchi mbalimbali kuja katika Taasisi yao kwaajili ya kujifunza,kuomba ushirikiano katika matibabu ya moyo na kuona namna ambavyo wanaweza kuwasaidia ili na wao wafikie hatua ambayo Taasisi ya JKCI imefikia katika utoaji wa huduma za matibabu ya moyo ambapo amebainisha baadhi ya Nchi ni pamoja na Malawi,Somalia,Burundi, Zambia,Jamhuri ya watu wa Comoro,Burkina Faso,Nigeria,Msumbiji,Gambia,Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Sierra Leon.
Hii ni Hospital maalum na Chuo Kikuu cha Mafunzo ya utalaamu wa matibabu ya moyo inayomilikiwa na Serikali inayotoa mafunzo na huduma za utafiti wa moyo.