ILE mechi ya Simba na Azam, Ahmed Arajiga amefukia sana mapungufu ya marefa wenzake ambayo yamejitokeza mfululizo msimu huu.
Kijiweni tulikuwa na hofu mechi ya dabi ya Mzizima ingeisha kwa malalamiko kwa marefa amebeba upande fulani na ameuonea mwingine kama ambavyo tumeshuhudia kwa marefa wengi wa sasa hivi.
Lakini mwamba baada ya gemu ya juzi kila upande umetoka hauna kinyongo na marefa na hilo linaashiria Arajiga alitimiza majukumu yake kwa ufasaha akisaidiwa na Mohamed Mkono na Kassim Mpanga.
Aliyaona kwa ukaribu matukio mengi kwa vile alihakikisha anakuwa sehemu sahihi ambazo alihitajika kufika wakati timu hizo zinacheza na aliweza kuendana na kasi ya mchezo kwa dakika zote 90 ambazo zilimalizika kwa sare ya mabao 2-2.
Na kingine ambacho wengi tulivutiwa na Arajiga ni jinsi alivyotoa uamuzi wa haki na pale timu moja ilipostahili kitu aliipa na pale ambapo haikustahili hakuipa na kuiepusha mechi kuwa na rabsha ambazo zingeshusha hadhi yake.
Kijiwe kinatoa pongezi kwa Arajiga na wenzake walioichezesha ile mechi maana walifanikiwa kuzima mashambulizi ambayo kabla ya ile mechi yalikuwa yakielekezwa mfululizo kwa marefa wanaochezesha ligi yetu.
Imekuwa jambo jema zaidi kwa vile Arajiga anafanya hayo katika kipindi ambacho anajiandaa kuwa miongoni mwa marefa ambao wameteuliwa kuchezesha fainali za mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani (Chan) mwezi Agosti.
Anapofanya vizuri anaonyesha kuwa mamlaka ambayo imemteua haikukosea kumpa dhamana ya kuwa katika kundi la marefa wa kati wa kuchezesha Chan 2024 akiwa pamoja na refa msaidizi Frank Komba.
Tunatembea kifua mbele kwa vile Arajiga ameshikwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika naye akashikamana.