Simulizi mtoto anayedaiwa kunyongwa Songea RPC, majirani wasimulia

Songea/Dar. Jeshi la Polisi mkoa wa Ruvuma, limethibitisha kifo cha mtoto wa mwaka mmoja na miezi miwili,  Giyan Marco Nchimbi, anayedaiwa kunyongwa katika kijiji cha Namiholo, Kata ya Peramiho Halmashauri ya Songea vijijini.

Taarifa za awali zilieleza kuwa tukio hilo, lilitokea Februari 24, 2025 jioni, baada ya mama mzazi kumuacha akiwa amelala katika chumba cha watoto.

Taarifa za Jeshi la Polisi zimeeleza kuwa mtoto huyo alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Mission Peramiho, baada ya kukutwa katika chumba cha Catherine Gama (12) akiwa amefunikwa na lundo la nguo.

Mtoto Giyan alikuwa akiishi na mama yake mzazi aitwaye Cesilia Mdolo.

Akizungumza na Mwananchi leo Alhamisi, Februari 27, 2025 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Marco Chilya amesema tukio hilo lilitokea jioni ya jana Jumatano, Februari 26, 2025.

Amesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa mtoto huyo mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi miwili saa 10 jioni, mama yake alimwacha akiwa amelala, akatoka yeye na rafiki yake.

Aliporudi hakumkuta mtoto kwenye chumba alichokuwa amelala ambako ni kwenye chumba cha mtoto wake mwingine ana miaka minne.

“Alivyorudi akamuuliza huyo mtoto wake wa miaka minne anaitwa Gerson Nchimbi kwamba mtoto yupo wapi?  Akamjibu kwamba mimi nilimuona anatambaa hapa sijui yuko wapi,” amesimulia.

Amesema walianza kumtafuta mtoto huyo bila mafanikio. Lakini ilipofika saa 12 jioni, kwenye hiyo nyumba kuna binti mwingine anaishi anayeitwa Catherine, akawa ametoka kuanua nguo na kuzirundika kwenye kitanda.

 “Baadaye saa moja usiku wakati wanatandika vitanda wakagundua kuwa kuna mtoto kitandani, pale ziliporundikiwa nguo.

“Hao kina Catherine wakawa wamelalamika kwamba kuna mtoto hapa, njooni. Lakini mtoto akawa amelegea sana, akachukuliwa alipofikishwa hospitali akafariki,” ameelezea RPC na kuongeza;

“Sasa hivi tunachunguza na tunamshikilia huyo mtoto Catherine, awali alikuwa kituo cha Polisi Peramiho, kwa sasa tumemuhamisha kutoka kituo kidogo na kumleta kituo kikubwa cha Polisi Songea,” amesema.

RPC amesema kwa sasa wanafuatilia taarifa ya uchunguzi wa madaktari ‘postmoterm’ na kama kulikuwa na chochote ili kufuatilia zaidi, “kwa kifupi uchunguzi bado unaendelea lakini tukio limetokea namna hiyo.”

Mkuu wa Wilaya ya Songea, Kapenjama Ndile amekiri kuwepo kwa tukio hilo na kuahidi kulizungumzia baada ya kukamilisha shughuli zake katika kijiji cha Maposeni.

Taarifa za awali kutoka kwa mtu wa karibu na familia hiyo (jina linahifadhiwa) zilieleza kuwa mtoto huyo anadaiwa kunyongwa na binti mwenye umri wa miaka 12, anayeishi katika nyumba waliyopanga huku kisa kikitajwa kuwa ni kosa la kuchana noti ‘fedha’ ya binti huyo.

Akisimulia mmoja wa ndugu wa familia hiyo (jina linahifadhiwa) amesema mama wa mtoto huyo anayejulikana kama mcheza ngoma maarufu Peramiho aitwaye Sakina alikuwa na watoto watatu.

“Mimi nipo kijiji cha mbele yake kidogo mitaa ya Peramiho, sikuwepo eneo jirani na tukio, lakini taarifa nilizozipata huyo mtoto amemnyonga mdogo wake, ilikuwaje mpaka amemnyonga watu waliofika siku ya mashujaa huku kijijini kwetu walitueleza,” amesimulia na kuongeza;

“Nyumbani kwake kuna mtoto amemnyonga mtoto wake, chanzo huyo mtoto aliyenyongwa alichukua hela ya ndugu yake akaichana sasa kwa hasira ndiyo akamnyonga.”

Taarifa za awali zilizosambaa jana Februari 26 katika mitandao ya kijamii zikidai haki ipatikane, na kumwamsha Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na wenye Mahitaji Maalum, Dk Dorothy Gwajima, ambaye alitoa msimamo huu.

“Nimesoma, nimepokea, ngoja niwasiliane na huko saiti niweze kusikia kinachoendelea. Nitarudi na mrejesho. Aidha, naomba DM namba za mlalamikaji tafadhali au mpe yangu aniandikie ujumbe ili niseme naye. Shukrani,” aliandika katika ukurasa wake wa mtandao wa X.

Related Posts