PAMBA Jiji ni wazi bado inakumbuka kipigo cha mabao 4-0 ilichopewa na Yanga Oktoba 3 mwaka jana katika mechi ya duru la kwanza ya Ligi Kuu Bara, licha ya kwanza tangu kuanza kwa duru la pili timu hiyo imeonekana kuimarika zaidi na kucheza kwa akili kubwa hasa inapokuwa CCM Kirumba.
Timu hizo zinatarajiwa kukutana leo ikiwa ni kati ya mechi mbili za Ligi Kuu zinazopigwa leo Ijumaa, huku mshabiki wakitarajia kushuhudia pambano la kiufundi zaidi, Pamba ikitaka kulipa kisasi na kulinda heshima ikiwa nyumbani, lakini Yanga ikitaka kuendeleza ilipoishia kabla ya kukabiliana na Mnyama.
Yanga inayoongoza msimamo wa Ligi kwa tofauti na pointi nne dhidi ya Simba iliyo na mchezo mmoja mkononi, itakuwa wageni wa Pamba kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, huku kila moja ikitoka kupata matokeo toafuti vinara hao wakitoka kumfyatua mtu kwa mabao 5-0 na Pamba ikiambuli sare.
Pambano jingine la leo ni lile la mapema saa 8:00 mchana wakati wenyeji Tabora United watakapoialika Dodoma Jiji kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi Tabora, kabla ya saa 10:15 jioni CCM Kirumba kuwaka moto kwa pambano hilo la kukata na shoka lililovuta hisia za mashabiki wengi.

Pamba inaingia katika mchezo huu ikiwa na kumbukumbu ya kutoka sare ya 2-2 na Singida Black Stars, huku kwa upande wa wapinzani wao Yanga, ikiwa na ari nzuri baada ya kuishushia kichapo cha fedheha Mashujaa mabao 5-0.
Timu zote zimekuwa na mwenendo mzuri katika michezo mitano ya mwisho, kwani Pamba iliyorejea Ligi Kuu baada ya miaka 21, tangu iliposhuka daraja 2001, imeshinda mitatu kati ya hiyo, ikitoka sare mmoja na kupoteza pia mmoja.
Katika michezo hiyo mitano, safu ya ushambuliaji ya Pamba imefunga mabao sita na kuruhusu nyavu zake kuguswa mara nne, ni mchezo mmoja pekee ikishindwa kupata bao walipolala 2-0 mbele ya Mashujaa Februari 19.
Kwa upande wa Yanga katika michezo mitano iliyopita, imeshinda minne na kutoka sare mmoja na moja ya safu inayotishia wapinzani ni eneo la ushambuliaji lililofunga mabao 19 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara tatu.

Yanga itaendelea kuwategemea washambuliaji nyota wa timu, Prince Dube na Clement Mzize ambao hadi sasa ndio vinara wa ufungaji baada ya kila mmoja wao kufunga mabao 10, wakionyesha viwango bora vinavyowatesa wapinzani wanaokutana nao.
Dube ndiye nyota aliyechangia mabao mengi ya kikosi hicho katika Ligi Kuu Bara hadi sasa kwani kati ya 55, yaliyofungwa na timu nzima, amehusika na 17, akifunga 10 na kuasisti baada ya kufunga 10 na kuasisti saba.
Mbali na Dube aliyechangia mabao mengi ndani ya kikosi hicho, mwingine anayefuatia ni kiungo, Pacome Zouzoua aliyehusika na 13, baada ya kufunga saba na kuasisti sita, sawa na Mzize aliyefunga 10 na kuhusika na matatu pia.

Kwa upande wa Pamba, itaendelea kutegemea ubora wa mshambuliaji nyota wa timu hiyo raia wa Kenya, Mathew Momanyi Tegisi ambaye hadi sasa amehusika katika mabao matano ya kikosi hicho, baada ya kufunga matatu na kuchangia mawili ‘Asisti’.
Nyota huyo aliyejiunga na timu hiyo katika dirisha dogo la Januari mwaka huu akitokea Shabana FC ya kwao Kenya, amekuwa muhimili mkubwa kikosini kwa kushirikiana na Abdoulaye Camara raia wa Guinea aliyetokea Singida Black Stars kwa mkopo.
Momanyi ni kama ameendeleza pale alipoishia wakati akiwa na Shabana FC, kwani kabla ya kujiunga na Pamba Jiji FC alikuwa amefunga mabao matano kwao Kenya, nyuma ya nyota mwingine wa kikosi hicho, Brian Michira aliyekuwa anaongoza na saba.
Kwa upande wa Camara amefunga moja katika ushindi wa 2-0 dhidi ya Coastal Union Februari 15, huku akiasisti, wakati Pamba ilipoifunga Azam bao 1-0, kwenye Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza Februari 9.
Camara alijiunga na Singida Agosti 14, 2024, ingawa kitendo cha kukosa nafasi ya kucheza mara kwa mara mbele ya Mkenya Elvis Rupia mwenye mabao tisa hadi sasa, kikamfanya kutolewa kwa mkopo kwenda Pamba dirisha dogo la Januari mwaka huu.
Kwa mara ya kwanza, Camara alitua nchini akitokea Milo FC na msimu uliopita aliibuka mfungaji bora baada ya kufunga mabao 21 na kuwavutia mabosi wa Singida, huku akiwahi kuzichezea pia, AS Ashanti Golden Boys na Wakriya AC zote za kwao Guinea.
Akizungumzia mchezo huo, Kocha wa Pamba Jiji, Fredy Felix ‘Minziro’ alisema anatarajia ugumu kutokana na ubora mkubwa wa wapinzani wao, ingawa ameandaa mkakati mzuri wa kuwazuia hasa baada ya kikosi hicho kuwa na safu nzuri ya ushambuliaji.
“Tunacheza na timu nzuri na yenye wachezaji bora hadi sasa, ni mchezo mgumu kama ilivyokuwa mingine iliyopita, ni kweli nimekuwa nikifanya mabadiliko ya mara kwa mara eneo la ulinzi, ila sababu kubwa ni kutokana na uchomvu miongoni mwao.”
Kwa upande wa Kocha wa Yanga, Miloud Hamdi alisema licha ya ushindi mnono wa mabao 5-0, mechi ya mwisho ugenini dhidi ya Mashujaa, ila wao kama benchi la ufundi wamesahau kilichotokea ili kuweka nguvu upya kutokana na huo ni mchezo mwingine.
“Hatuwezi kuzungumzia zaidi kilichopita kwa sababu huu ni mchezo mwingine na una malengo yake tofauti na uliopita, ni kweli mwenendo wetu ni mzuri lakini tunahitaji kuonyesha zaidi ya hiki kinachoendelea kuonekana machoni mwa mashabiki.”

Mchezo mwingine wa mapema saa 8:00 mchana, utapigwa kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi na wenyeji Tabora United watakuwa na kibarua cha kupambana na Dodoma Jiji yenye morali ya kushinda mechi mbili mfululizo ya Ligi Kuu.
Tabora imecheza dakika 270 bila ya ushindi tangu mara ya mwisho ilipoifunga Kagera Sugar 2-1 ugenini na kuanzia hapo imetoka sare ya 1-1 na KenGold na Tanzania Prisons, kisha suluhu na Fountain Gate.
Mchezo huu utakuwa pia wa kisasi kwa Tabora, kwani mechi ya kwanza iliyopigwa kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma ilishinda mabao 2-0, Oktoba 2, mwaka jana, yaliyofungwa na Paul Peter na mshambuliaji wa zamani wa kikosi hicho, Wazir Junior.
Tabora itaendelea kumtegemea nyota wa timu hiyo, Offen Chikola mwenye mabao sita ya Ligi Kuu hadi sasa akiwa sawa na Paul Peter anayetegemewa na Dodoma Jiji, jambo linaloamsha vita ya wachezaji wenyewe kwa wenyewe kwenye ufungaji.
Katika michezo 21 iliyocheza Tabora, imeshinda tisa, sare saba na kupoteza mitano ikishika nafasi ya tano na pointi zake 34, huku kwa upande wa Dodoma Jiji iliyopo nafasi ya saba na pointi 26, imeshinda saba, sare mitano na kuchapwa minane.
Kocha wa Tabora United, Mkongomani Anicet Kiazayidi alisema changamoto pekee anayokabiliana nayo ni kutengeneza balansi ya nyota wapya na waliopo, huku kwa upande wa Kocha wa Dodoma Jiji, Mecky Maxime akitambia mechi mbili zimewaongezea ari zaidi.