Rungu la wajumbe CCM latesa vigogo

Dar es Salaam. Mabadiliko ya katiba ya Chama cha Mapinduzi yameanza kuwavuruga wagombea wa udiwani, ubunge na uwakilishi, ikiwa imebaki takribani miezi mitano kufanyika kwa kura za maoni.

Januari 18-19, 2025, Mkutano Mkuu wa CCM Dodoma, pamoja na mambo mengine ulifanya mabadiliko ya katiba ya chama hicho na kuongeza makundi ya wanachama watakoshiriki kuwapigia kura ya maoni wagombea hao.

Mabadiliko hayo yameanza kuwavuruga wale wanaotarajia kujitosa kwenye kinyang’anyiro hicho, kuhusu namna ya kuwafikia na rasilimali zinazohitajika.

Pengine kinachowasumbua wagombea  hao, ndio kilekile kilicholengwa katika mabadiliko hayo, ambayo kwayo, Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan alisema mgombea akitaka kuwafikia “inabidi ajipange kidogo.”

Hata hivyo, akitoa maelezo ya mabadiliko hayo mbele ya wajumbe wa mkutano mkuu, Katibu wa Oganaizesheni, Issa Gavu alisema mabadiliko yameongeza idadi ya wapigakura za maoni kwenye mchujo wa watia nia ya ubunge, udiwani na uwakilishi kwa lengo la kutanua demokrasia ndani ya chama.

“Imebidi kuongeza idadi ya wapigakura ili kutanua demokrasi kwa wanaCCM, kuweka uwanja mpana wa kuchagua wawakilishi wa eneo.

“Tukiongeza idadi hii inaaminika kwamba sauti ya wanaCCM katika eneo lile itakuwa imekua na wamemchagua mtu ambaye anakubalika na wengi, ndiyo kiini cha mapendekezo hayo,” alisema Gavu.

Kilichofanywa na CCM kilipigiwa kelele mara baada ya kura za maoni mwaka 2020 ama na waliokuwa wagombea au wanachama kutaka kutanuliwa kwa wajumbe watakaokuwa wakishiriki kura za maoni.

Msingi wa hoja hiyo ni kuzuia wagombea wenye fedha kuzitumia kuwashawishi wajumbe kuwachagua.

 Pia, hilo lilijitokeza Juni 2024 katika ziara ya Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi akiwa Babati mkoani Manyara.

Wanachama na CCM waliojitokeza kwenye mkutano wake, walipendekeza wagombea udiwani, ubunge na uwakilishi wachaguliwe na wanachama badala ya wajumbe wachache ili kuzuia mianya ya rushwa.

Pendekezo hilo lilichukuliwa na Dk Nchimbi akisema wanakwenda kulifanyia kazi akisema: “Hata mimi sipendi wagombea ambao hawachaguliki, wanaopatikana kwa rushwa.”

 Kauli hiyo iliibua shangwe kwa wanachama na wananchi waliokuwapo.

Tangu kufanyika kwa mabadiliko hayo ya katiba, kumekuwa na hofu kwa wagombea wanaotetea nafasi hizo au wanaotaka kuingia kwenye kinyangany’iro kuwania fursa za kuwatumikia wananchi kwenye udiwani, ubunge na uwakilishi.

Mwananchi ina taarifa za mijadala ya baadhi ya wabunge wanaotaka kutetea nafasi zao, wakijadiliana jinsi ya kuwakabili wajumbe, ambao mwaka 2020 walijipatia umaarufu zaidi wakisema, ‘wajumbe sio watu.’

Msemo huo uliasisiwa na msanii Steve Nyerere, ambaye mwaka 2020 alichukua fomu ndani ya CCM akiomba kuteuliwa awe mgombea ubunge Iringa Mjini, lakini pamoja na ahadi alizopewa na wajumbe aliambulia kura sita.

Si Steve Nyerere pekee aliyelalamikia wajumbe, mwigizaji Wema Sepetu alilia kuhusu wajumbe, kwa kuwa na yeye kwenye kura za maoni alipata kura 91.

Wema alikuwa miongoni mwa waliowania ubunge wa viti maalumu ndani ya CCM kupitia Mkoa wa Singida katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, lakini kura zake hazikutosha akashika nafasi ya nne kati ya wagombea 13.

Mmoja wa wabunge hao amesema: “Mabadiliko haya ya katiba ndugu zangu yamepanua gilo, kwa sasa kuwakabili wajumbe unahitaji si chini ya Sh500 milioni, tofauti na ilivyokuwa mwanzo.”

“Hapa kwa kweli kikubwa ni kukubalika au kama ni kutoa chochote kwa wajumbe lazima uwe umejipanga. Sasa unaweza kutoa halafu kukawa na mpinzani wako yeye katoa zaidi, unaweza kupigwa ukaangukia kwenye umasikini,” anasema.

Mwingine kwenye majadiliano hayo anasema: “Huu ni mtego, labda cha kufanya unaweza kutoa kwa baadhi au viongozi na kuwaahidi wengine, lakini sasa wajumbe wanachokitaka si mnajua lazima kupata chao mapema.”

Mabadiliko hayo, kiongozi mmoja mwandamizi ambaye ni mjumbe wa kamati kuu, amesema yanalenga kuruhusu wengi kuchagua na kuchaguliwa pasipo kutumia fedha:

“Hii itatusaidia sana kupata wagombea wanaokubalika na si fedha au chochote kitu.”

“Ingawa wengi walipinga sana haya mabadiliko, ukiyaangalia kwa undani jinsi wapiga kura walivyoongezeka, inawatoa jasho hasa wale ambao walipopata nafasi hawakurudi kwa wananchi au walirudi kwa kudonoadonoa, ila kama ulijipanga mapema hakuna shida,” amesema.

Kwa mujibu wa Gavu, mabadiliko yaliyofanyika sasa yanawataja wajumbe watakaopiga kura za maoni kwa wagombea ubunge, udiwani na uwakilishi ni wajumbe wa mkutano mkuu wa kata au wadi, wajumbe wa mkutano mkuu wa jimbo na wajumbe wa mkutano mkuu wa wilaya.

Katika mabadiliko ya sasa, amesema wajumbe watakaopiga kura za maoni kwa wagombea wa ubunge na udiwani ni wajumbe wote wa kamati ya siasa ya kila tawi, kata za jimbo au wilaya husika.

Pia, amesema wengine ni wajumbe wa kamati ya uongozi ya kila shina katika kata au jimbo au wilaya na wajumbe wa kamati ya utekelezaji katika kila tawi na kata ya eneo husika.

Kwa mujibu wa Gavu, wameongeza kifungu cha 47 (1) (s) kwa madhumuni ya kupiga kura za maoni kwa lengo la kuwezesha wajumbe wote wa kamati ya siasa ya kata/wadi na matawi/wajumbe wa kamati za uongozi za kila shina na wajumbe wa kamati za utekelezaji za kila tawi na kata, kuwa wajumbe wa mkutano mkuu wa kata/wadi wakati wa uchaguzi.

Amesema pia kwa upande wa Zanzibar, Ibara ya 60 (1) (T) imeongezwa kwa madhumuni ya kupiga kura za maoni ili kuwawezesha wajumbe wote wa kamati ya siasa ya kata/wadi na matawi, wajumbe wa kamati za uongozi za kila shina na wajumbe wa kamati za utekelezaji za kila tawi na kata kuwa wajumbe wa mkutano mkuu wa jimbo wakati wa uchaguzi.

Utaratibu kama huo pia utafanyika kwenye mchujo wa wabunge wa viti maalumu kupitia Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), kwa kuongezwa wajumbe wa kamati ya utekelezaji kwenye mkutano wa Taifa wa Baraza Kuu la UWT.

Akizungumza kwenye mkutano huo uliofanya mabadiliko ya katiba, Gavu alisema lengo la mabadiliko hayo ni kuongeza ushiriki wa wanachama kufanya uamuzi, kuimarisha muundo wa ngazi ya shina pamoja na kudhibiti vitendo vya rushwa.

Kwa mujibu wa kanuni za uteuzi wa wagombea uongozi katika vyombo vya dola, kura ya maoni inapigwa kwenye Mkutano Mkuu wa CCM wa Wilaya ambao baadhi ya wajumbe wake ni mwenyekiti na katibu wa CCM wa wilaya, wajumbe wa NEC wanaoishi kwenye wilaya hiyo, mkuu wa wilaya anayetokana na CCM, katibu wa siasa na uenezi wa wilaya.

Wengine ni mbunge au wabunge wa wilaya hiyo, wakiwamo wa viti maalumu, wajumbe NEC wa mkoa wanaoishi kweye wilaya, wa-NEC wilaya na wenyeviti na makatibu wa jumuiya zote UWT, UVCCM na wazazi.

Utaratibu huu unaelezwa ni ngumu kujua idadi sahihi ya wajumbe kwa kila jimbo, kwa kuwa jimbo linaweza kuwa na kata 14 na lingine kata 45, hivyo idadi ya wajumbe kutofautiana.

Kwa upande wa wabunge wa viti maalumu kupitia UWT ambao wako kwenye makundi ya viti maalumu, wafanyakazi, watu wenye ulemavu, vyuo vikuu na mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) nao wameongezewa wigo wa idadi ya wajumbe.

Kwa kawaida mchujo ndani ya UWT, wagombea wanachukua fomu kwa katibu wa UWT mkoa na baadaye mchujo unaanzia kwenye kamati ya siasa mkoa, Baraza la UWT mkoa na Baraza la UWT Taifa na inaelezwa wataongezewa wajumbe wa kamati ya utekelezaji.

Mchujo wa madiwani nao unapitia kwenye mkutano mkuu wa kata ambao utaongezewa wajumbe wa kamati ya siasa na wale wa utekelezaji wanaotoka kwenye jumuiya za chama.

Mkutano Mkuu wa Kata, baadhi ya wajumbe wake ni mwenyekiti na katibu wa kata, katibu wa siasa na uenezi wa kata, wenyeviti na makatibu wa CCM wa matawi yote kwenye kata na mbunge na diwani wanaotoka kwenye kata hiyo.

Historia ya mchujo wa watia nia wa ubunge ndani ya CCM kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 1995 uliruhusu wana-CCM wote ambao uanachama wao una umri wa kuanzia miezi sita na kuendelea kabla kupiga kura ya maoni.

Lakini, kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 utaratibu huo uliondolewa na kuruhusu mwana-CCM yeyote kuwa na haki ya kupiga kura ya maoni bila kujali ameingia lini kwenye chama na ulileta changamoto kuingizwa mamluki kwa watu kupewa kadi za CCM siku ya mchujo.

Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917

Related Posts