Utafiti uliowahi kuchapishwa na Jarida la Internal Medicine, uligundua uwezekano wa kupunguza hatari ya kifo cha mapema kwa kila hatua 2,000 unazotembea kwa siku.
Ulibaini kutembea hatua 10,000 kwa siku kunapunguza hatari ya kupata ugonjwa wa moyo na mishipa ya damu, aina 13 za saratani na kiharusi.
Kutembea kunaweza kufanyika katika maeneo ambayo ni rafiki na salama ikiwamo ua wa nyumbani, barabara za pembezoni, maeneo ya wazi, viwanjani au katika mashine za kisasa.
Faida kubwa ni pamoja na kupunguza hatari ya kupata uzito uliokithiri au unene. Na pia kuendelea kulinda utimamu wa mwili.
Unene ni kihatarishi cha kupata magonjwa yasiyoambukiza ikiwamo kisukari, shinikizo la juu la damu, magonjwa ya moyo na mishipa ya damu, ugonjwa sugu wa figo na saratani.
Tumia dakika 30-60 kwa siku katika siku tano za wiki hivyo kuupa mwili siku mbili za kusahihisha dosari za ndani kwa ndani ikiwamo majeraha ya wastani ya misuli baada ya kufanya mazoezi.
Unapofanya mazoezi haya kwa muda huu inasaidia mwili kuchoma kiasi kikubwa cha kalori yaani sukari hatimaye pia kudhibiti unene.
Ili kupata hamasa zaidi unaweza kutembea pamoja na marafiki, mwenza wako au utembeaji wa makundi kwa kushiriki katika marathon mbalimbali zinazofanyika nchini.
Kanuni ya mazoezi ya kutembea ya 6-6-6 inawashauri watu wazima kati ya miaka 60+ kutembea kwa dakika 60 kwa siku muda wa asubuhi saa 12 asubuh au jioni saa 12.
Utembeaji kwa kutumia kanuni hii ni ubunifu wa wataalamu wa afya na mazoezi ili kupata matokeo makubwa hasa kwa watu ambao tayari umri wao ni 60+ ili kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza.
Kabla ya utembeaji huo inahitajika kwa dakika sita za kupasha mwili moto kwa mazoezi ya viungo na dakika sita za kupumzika.
Kwa watu wazima yaani wazee wa umri miaka 60+ ambao uwezo wa kukimbia umepungua , utembeaji hatua 10,000 kwa siku unaweza kuleta matokeo chanya kiafya.
Unaweza kutumia simu janja kwa kutumia aplikesheni ambayo inahesabu na kutunza kumbukumbu ya hatua zako unazotembea kwa siku. Wazee wanaweza wakatembea umbali wa hapa na pale kila siku wakiweka lengo la kutimiza hatua 10,000.
Kampeni ya utembeaji hatua 10,000 kwa siku ilizinduliwa nchini Japani mnamo mwaka 1964 wakati michezo ya Olympic. Utafiti wa kisayansi wa tiba umethibitisha kwamba ni zoezi rahisi linaloweza kupunguza magonjwa.
Utafiti wa kitiba unapendekeza kwamba kutembea hatua 9,800 kwa siku ndiyo “dozi bora” ya kupunguza hatari ya ugonjwa ya akili kwa asilimia 50 ikiwamo ugonjwa wa kusahau.
Kutembea hatua 10,000 kwa siku kunaweza kusaidia pia kupunguza dalili za magonjwa mengine ya akili kama vile sonona, wasiwasi na mfadhaiko wa akili.
Vilevile kupunguza maumivu ya magoti na viungo kwa watu walio na ugonjwa wa shambulizi la viungo au baridi yabisi.