Dar es Salaam. Tatizo la nguvu za kiume limeendelea kusumbua vijana nchini.
Wakati baadhi wakitajwa kutumia za asili ambazo hazitambuliwi na mamlaka, baadhi yao imegundulika kuja na mbinu mpya ya kununua dawa za kawaida kwenye maduka ya dawa, huku wakibadilisha matumizi yake.
Kwa mujibu wa uchunguzi wa siku kadhaa wa Mwananchi, dawa zilizobainika kutumika zaidi, ni zile zinazotibu magonjwa mbalimbali lakini wao huzitumia kwa namna tofauti kwa kile wanachokileza kama ‘kujibusti’.
Hata hivyo, watalaamu wa afya, wanaonya kuwa vijana hao wanakosa ushauri wa namna ya kumaliza tatizo, badala yake wanalifanya kuwa kubwa zaidi.
Uchunguzi huo umefanyika ikiwa imepita miaka miwili tangu Rais Samia Suluhu Hassan alipowaagiza watafiti nchini kufanya utafiti wa kina kubaini chanzo cha tatizo la ukosefu wa nguvu za kiume linalotesa vijana ambao ni nguvu ya Taifa.
Akizungumza Oktoba 3, 2022, Rais Samia alisema msingi wa tatizo hilo unaanzia kwenye lishe, huku akiwapa kazi watafiti wafanye kazi kuwasaidia vijana wawe mashababi, ili hatimaye wazae watoto wenye afya kwa ajili ya kulitumikia taifa lao.
Mwananchi imefanya uchunguzi kuzunguka maduka mbalimbali ya dawa makubwa na madogo jijini Dar es Salaam na kubaini uwepo wa dawa hizo, huku wauzaji wakieleza biashara hiyo kwa sasa imechangamka.
Wataalamu wa dawa kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili, wanakiri dawa hizo zinatumika kuongeza nguvu za kiume, ingawa kusudio la awali la kutengenezwa kwake, lilikuwa kutibu watu wenye presha ya mapafu na wanaopanda milima mirefu lakini hawajajiandaa.
Wanasema na hata zinapohitajika kutumika kwa ajili ya kuongeza nguvu, hilo linapaswa kufanywa ka mujibu wa maelekezo ya daktari na sio kiholela kama wanavyofanya vijana hao.
Muuzaji wa dawa hizo katika duka moja lililopo Tabata Shule, Joyce Helina, anasema watumiaji wa kubwa wa dawa hizo ni vijana, ingawa hata wazee wenye matatizo kama kisukari na presha nao wanatumia kwa kiasi.
“Katika duka langu hili kwa siku naweza kuwauzia vijana kuanzia saba hadi 10 na wengi unakuta ni wageni wa hapa, huwezi kuwajua lakini kusema ukweli dawa hizi zinanunuliwa zaidi,” anasema.
Muuzaji mwingine, Juma Mustafa anasema ubora wa dawa wanazouza, inategemeana na aina ya kampuni
“Tunauza ingawa Viagra inanunuliwa zaidi kutokana na bei yake kuwa chini, wateja ni wengi unajua kipindi cha nyuma tulizoea kupata wazee wenye matatizo ya presha, kisukari lakini kwa sasa vijana ni wengi,”anaeleza.
Mustafa anasema wanapokuja huwa wanawapa ushauri wa namna nzuri ya kuzitumia, huku akieleza kwa kawaida kwa mwezi wanatakiwa kutumia mara moja.
“Changamoto kijana akifika kununua dawa hii haji tena anaenda sehemu nyingine anaogopa kujulikana, kesho anaenda kununua duka lingine,” anasema.
Baadhi ya vijana waliozungumza na Mwananchi wanadai wanatumia dawa hizo ili kujenga stamina kwa kusisimua misuli na kuongeza nguvu za kuufanya tendo kwa ufanisi na kwa muda mrefu.
“Binafsi sina tatizo la nguvu za kiume ila nilitumia kwa sababu kuna dada mmoja alikuwa mzuri alinitambia kwamba siwezi …, nilimueleza rafiki yangu ndipo akanishauri na kunipa dawa,’’ anasema Hussein Malima.
Anasema kuanzia hapo akawa anawatuma vijana wenzake kwenda kumnunulia kwenye maduka ya dawa bila kwenda kupima wala kupata ushauri wa kitaalamu.
Vidastus Richard anasema ana miaka miwili tangu ameanza kutumia dawa ya kuongeza nguvu, akidai alielekezwa na mmoja wa marafiki zake tangu alipokuwa chuo.
“Vijana wengi wanatumia lakini huwezi kununua dawa hizi kila siku duka moja, kwakuwa baadhi ya wauzaji wanapenda kuzusha hawawezi kutunza siri,” anasema.
Kwa upande wake, Laizer Jackson anasema:
“Siku hizi maisha yamekuwa magumu unakuta vijana muda mwingi tunajikita kutafuta fedha ukirudi nyumbani umechoka… sasa dawa hizi zinasaidia kuondoa hofu na wasiwasi wa kushindwa kufanya tendo.
Mtaalamu wa saikolojia, Charles Kalungu anasema kugubikwa na hofu ni sababu ya watu wengi kuendelea kutumia dawa hizo kwa wingi, ingawa mambo wanayojaribu kuhusisha yana uhalisia, lakini anasisitiza kuwa chanzo cha wengi ni mfadhaiko.
“Chanzo kingine ni suala la taarifa, kwa sasa vyanzo ni vingi na inakuwa rahisi mtu kuogopa kutokana na kupata ujumbe uleule na wakati mwingine tafsiri ya wafanyabiashara kuona huo ni mwanya kutengeneza vipato kupitia hofu za watu,” anasema.
Anasema matumizi yamekuwa makubwa lakini wengi wao ukiwafuatilia na kuwauliza kujua kama wamewahi kunufaika na matumizi ya dawa hizo, watakukatalia.
“Kutokuwa na ufanisi wa kutosha kwenye ngono ni sababu ya kuwasukuma kuingia katika matumizi hayo, hasa kwakuwa wanakosa elimu sahihi ya kijinsia na kujamiana ,”anasema.
Mfamasia na mkufunzi wa Shule ya Ufamasia kutoka Chuo Kikuu Muhimbili (Muhas), David Myemba anasema dawa za kuongeza nguvu ziko nyingi mitaani, ingawa mwanzoni zilitengenezwa kwa ajili ya kutibu tatizo la presha ya mapafu.
“Baada ya watu kutumia ilionekana zinasababisha athari chanya upande wa uume kusimama kwa muda mrefu au kupita kiasi…’’ anaeleza.
Alisema baada ya kuona upande huo unasoko zaidi, walibadilisha kutoka kutibu presha ya mapafu na kutumia kwenye ukosefu wa nguvu za kiume.
“Ina uwezo wa kutumika kihalali kabisa kwa wenye matatizo ya nguvu za kiume au kutibu presha ya mapafu,” anasema
Anasema mtu anayepaswa kutumia ni yule mwenye uhitaji kwa maana ya kukosa nguvu za kiume, na vyanzo vyake ni vingi inaweza kuwa msongo wa mawazo au wenye magonjwa kama kisukari, mafuta mengi kwenye damu au matatizo katika mfumo wa fahamu.
“Inatakiwa atumie mtu asiyeweza kusimamisha uume katika kiwango kisichokuwa cha kuridhisha angalau kwa dakika moja hadi tano mfululizo na usiwe na magonjwa,”anasema.
Hata hivyo, anasema watumiaji wengi hawapo kwenye kundi hilo, kwa sababu ni vigumu kumpata mtu anayeshindwa kusimamisha uume.
“Wengi wanatumia kutaka kuongeza ufanisi wa tendo la ndoa lakini vijana wengi wanasumbuliwa na msongo wa mawazo hasa kwenye utafutaji wa kimaisha na wanashindwa kupata nguvu na dawa zinakuwa kama kimbilio,”anasema.
Mtaalamu wa afya kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dk Paul Masua anasema dawa hizo zote ni aina moja isipokuwa majina yake ni tofauti na zinapaswa kutolewa kwa cheti cha daktari.
“Mbali na kutibu nguvu za kiume na presha ya mapafu, zinatumika kwa watu wanaohitaji kupanda mlima, mathalani mlima Kilimanjaro na hawana mazoezi ya kutosha, hawa wanaweza kutumia,”anasema.
Anaongeza: “Walio wengi wanajitibu wenyewe bila kufanyiwa uchunguzi na bila kuandikiwa na daktari. Wanaume wa sasa ni tofauti na wanaume wa miaka 50 iliyopita na tafiti zinaonyesha uwezo umepungua.’’
Myemba anasema kutumia dawa hizo wakati huna tatizo, ni kujiweka kwenye mazingira ya kupata matatizo ya kiafya, kwani dawa hizo zinasukuma damu nyingi kwenye uume na misuli inasimama kwa muda mrefu.
“Ukitumia dawa hizo wakati huna tatizo unaidhohofisha misuli baada ya muda inaweza kuchoka na ubaya zaidi ukianza na dozi ya gramu 50, haitakutosha na baada ya mwezi utahitaji dozi ya gramu 100 na mtu anakuwa tegemezi bila kutumia hiyo dawa huwezi kusimamisha,” anasema.
Anasema madhara mengine ni kifo cha ghafla hasa kwa watumiaji wanaougua magonjwa ya moyo.
“Dawa hizi kazi yake kubwa ni kushusha presha ya mapafu sasa mtu ukiwa na magonjwa ya moyo ukitumia unaweza usipate mzunguko mzuri wa hewa ya oksijeni kwenye damu na mwishowe zitasababisha kifo cha ghafla,” anasema.