Nahimana kiboko ya penalti Ligi Kuu

KIPA Jonathan Nahimana wa klabu ya Namungo ameonyesha umahili mkubwa wa kudaka mikwaju ya penalti baada ya juzi (Alhamis) usiku kudaka penalti ya Feisal Salum  wa Azam Fc katika mchezo wa Ligi Kuu  uliomalizika kwa sare ya 1-1 kwenye uwanja wa Azam Complex.

Penalti hiyo ilipatikana dakika ya 48 ambayo kama ingeingia wavuni basi ingeifanya Azam  iongoze kwa bao 2-1 lakini umakini wa Nahimana ulifanya mchezo huo kuendelea kusalia 1-1 hadi dakika 90.

Nahimana hadi sasa kwenye mechi 11 ambazo amekaa golini amepigiwa penalti tano na kudaka tatu.

Nahimana amedaka penalti ya kwanza ya Nicolas Gyan kwenye mchezo dhidi ya Fountain Gate huku ya pili kwenye mchezo dhidi ya Simba akidaka ya Ateba na juzi dhidi ya Feisal wa Azam Fc.

Kipa huyo ameshindwa kufua dafu kwa Ahoua wa Simba ambaye alimfunga penalti mbili kwenye mchezo mmoja ambao Simba ilishinda 3-0.

Akizungumzia umahili wake wa kuonyesha kudaka mikwaju ya penalti, Nahimana alisema Siri kubwa ni mazoezi anayofanya mara kwa mara na makipa wenzake.

“Mara nyingi huwa makini kwenye macho ya mpigaji sambamba na miguu yake, hivyo vitu navizingatia sana, siri kubwa ni mazoezi pia,” alisema Nahimana.

Kipa huyo ambaye ameidakia Namungo mechi 11 hadi sasa hajaruhusu nyavu zake kuguswa kwenye michezo sita.

Mechi alizodaka Nahimana ni dhidi ya Tanzania Prisons huku Namungo ikishinda 1-0, Pamba Jiji 0-1 Namungo, Simba 3-0 Namungo, kmc 1-0 Namungo, Namungo 2-1 Fountain Gate, Namungo 1-0 Tanzania Prisons, Namungo 0-3 Simba, JKT Tanzania 0-0 Namungo, Namungo 2-2 Dodoma Jiji, Coastal 0-0 Namungo na Azam 1-1 Namungo.

Related Posts