Siku saba zaongezwa kwa waombaji ajira Zimamoto

Dar es Salaam. Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limeongeza muda wa siku saba kwa waombaji wa nafasi za ajira kupitia tangazo lililotolewa Februari 13, 2025 na Kamishna Jenerali wa jeshi hilo, John Masunga.

Kwa mujibu wa tangazo  hilo la awali  lilihusisha nafasi za ajira za ngazi ya konstebo kwa vijana waliohitimu kidato cha nne ambalo muda wa mwisho wa kutuma maombi ulipaswa kuwa leo Februari 28, 2025.

Hata hivyo leo jeshi hilo limetoa tangazo la kuongeza muda wa siku saba hadi Machi 7, 2025  na kuwataka vijana wenye sifa kuendelea kutuma maombi.

Alipotafutwa na Mwananchi, Msemaji wa jeshi hilo, Puyo Nzalayaimisi amesema jeshi limeongeza muda huo ili kutoa fursa kwa kila mwenye vigezo kuomba.

“Tunahitaji kila mwenye kigezo aombe, hii ni Serikali sikivu,” amejibu Puyo kwa ujumbe mfupi alipotafutwa na mwandishi wa Mwananchi.

Miongoni mwa vigezo vilivyoainishwa katika tangazo hilo la ajira ni mwombaji kuwa raia wa Tanzania wa kuzaliwa, mwenye umri wa kuanzia miaka 18 hadi 25 na urefu usiopungua futi 5.7 kwa wanaume na futi 5.4 kwa wanawake.

Pia awe na afya njema kimwili na kiakili, awe hajawahi kutumia aina yoyote ya dawa za kulevya, awe hajawahi kuoa wala kuolewa, hajawahi kuajiriwa serikalini, asiwe na rekodi za uhalifu wala alama za michoro mwilini.

Mwombaji pia anatakiwa kuwa na cheti cha kuzaliwa, kitambulisho au namba ya utambulisho iliyotolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) na awe tayari kuhudhuria mafunzo ya taaluma ya zimamoto na uokoaji.

Related Posts