Dodoma. Watu takriban 100,000 kutoka katika vijiji 120 wamenufaika na mradi wa umeme uliogharimu Sh165 bilioni.
Akizungumza katika ufungaji wa mradi wa umeme wa Makambako (Njombe) hadi Songea (Ruvuma), Balozi wa Sweden nchini, Charotta Ozaki Macias amesema serikali ya Sweden ilisaini mkataba wa utekelezaji wa mradi huo mwaka 2008.
Amesema pia iliahidi Sh165 bilioni kwa ajili ya utekelezaji wa ujenzi wa njia za kusambazia umeme na miradi ya umeme vijijini.
“Mradi ulifanikiwa kikamilifu kuwaunganishia umeme watu takriban 100,000 katika kaya 23,232 kwenye vijiji 120.
Charotta amesema kuwa ushirikiano wa nchi mbili hizo katika sekta hiyo umeendelea kuchochea juhudi za maendeleo kwa Watanzania.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Felchesmi Mramba amesema nchi ya Sweden imehusika kwa kiasi kikubwa na miradi ya umeme vijijini ikiwemo katika maeneo ya Makambako (Njombe), Urambo (Tabora), Serengeti (Mara), Simanjiro (Manyara) na Ukerewe (Mwanza).
Kuhusu mradi wa Makambako ambao umegharamiwa na nchi ya Sweden, Mramba amesema ulikamilika tangu mwaka 2019.
Amesema mradi huo ulikuwa wa Kilovoti 220 ulioanzia Makambako hadi Songea Mjini kupitia Njombe, Madaba na baada ya kukamilika ulienda hadi Wilaya za Mbinga, Nyasa, Namtumbo na sasa wanaendelea kusogoza hadi Tunduru.
Katika hatua nyingine Mramba amesema Serikali kwa kushirikiana na Sweden wanafanyia ukarabati mkubwa kituo cha kuzalisha umeme cha Hale mkoani Tanga.
Amesema kituo hicho kimejengwa mwaka 1964, kilipunguza uwezo wake wa kuzalisha kutoka megawati 21 hadi megawati nne kutokana na uchakavu wa mitambo.
“Tunafanya ukarabati mkubwa wa kituo cha Hale na kitakapokamilika kitakuwa kama kipya lakini Sweden wamekuwa watu wa karibu katika miradi ya umeme. Ni watu walioendelea sana kwenye miradi ya umeme wa maji,”amesema.
Amesema ukarabati wake umeshafikia zaidi ya asilimia 50 na Agosti mwaka 2026, kitakuwa kimekamilika kwa gharama ya Sh49.9 bilioni ambapo nchi ya Sweden imechangia asilimia 60 huku Tanzania ikitoa asilimia 40.
Amesema kukamilika kwa kituo hicho kutasaidia kuimarisha hali ya upatikanaji wa umeme katika mikoa ya Kaskazini ukiwamo Tanga.