KLABU ya Cosmopolitan imeachana na aliyekuwa kocha mkuu wa timu hiyo, Idd Nassor ‘Cheche’, baada ya makubaliano ya pande mbili, huku sababu ikiwa ni mwenendo usioridhisha wa kikosi hicho katika Ligi ya Championship.
Kocha huyo wa zamani wa matajiri wa Jiji la Dar es Salaam, Azam FC, aliliambia Mwanaspoti ni kweli amefikia makubaliano hayo ya kusitisha mkataba wake wa miezi mitatu uliobakia, kwa lengo la kutoa nafasi kwa mwingine kuendeleza alipoishia.
“Ni kweli nimefikia uamuzi huo kwa masilahi mapana ya klabu kwa sababu mwenendo wetu sio mzuri na ninavyoona hakuna kitu ambacho ninaweza kukibadilisha kwa muda uliobakia, siwezi kusema nimefeli bali nimeamua kuwajibika mwenyewe,” alisema.
‘Cheche’ aliyewahi kuifundisha pia Pan Africans, alisema anaushukuru uongozi wa kikosi hicho kwa nafasi waliyompa tangu amejiunga nacho, huku akikiri hajafikia malengo aliyotamani ayafikie kutokana na changamoto mbalimbali zilizojitokeza.
“Niliichukua timu katika kipindi kigumu sana na malengo yalikuwa kuitoa sehemu moja kwenda nyingine ila imeshindikana, nafikiri ni muda kwa kocha mwingine kuendeleza nilipoishia, naamini nafasi ya kufanya vizuri bado ipo mikononi mwao.”
Kocha huyo alijiunga na timu hiyo Januari 23, mwaka huu akichukua nafasi ya mtangulizi wake, Mohamed Kijuso aliyeondoka pia baada ya mwenendo mbaya ndani ya kikosi hicho, alichokiongoza katika michezo 14, ya Ligi ya Championship msimu huu.
Kijuso msimu huu hadi anaondoka ndani ya kikosi hicho alikiongoza katika michezo 14 ya Ligi ya Championship na kati ya hiyo alishinda miwili, sare miwili na kupoteza 10, akikiacha kikiwa nafasi ya 13, kwenye msimamo na pointi zake nane.
Kwa upande wa ‘Cheche’ ameiongoza katika michezo mitano na kati ya hiyo ametoa sare mmoja tu wa (1-1) v Songea United na kuchapwa minne, akianza na (2-1) v African Sports, (3-0) v Mtibwa Sugar, (4-0) v Mbeya Kwanza na 1-0 dhidi ya Bigman FC.
Kwa sasa kikosi hicho kinashika nafasi ya 14 na pointi 12, baada ya kucheza michezo 21 na kati ya hiyo, imeshinda mitatu tu, sare mitatu pia na kuchapwa 15, ambapo safu ya ushambuliaji imefunga mabao 12 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 33.