Masahaba walivyopokea Mwezi wa Ramadhani-2

Toleo lililopita liliangazia namna Masahaba wa Mtume wa Allah walivyokuwa wakiupokea na kuukaribisha mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Nilionyesha namna walivyoupokea mwezi wa Ramadhani kwa furaha, kulipa saumu zao walizokuwa wakidaiwa huko nyuma, kuomba dua na kufanya maandalizi mbalimbali. Endelea…

Kuzidisha usomaji wa Qur’ani

Salama bin Kuhail alieleza kuwa mwezi wa Shaaban ni mwezi wa wasomaji wa Qur’ani. Hata hivyo, Habiib bin Abi Thabit alikuwa akisema mwanzoni mwa mwezi Shaaban: “Huu ni mwezi wa wasomaji wa Qur’ani.”

Amru bin Qais alikuwa akijitenga na shughuli nyingine ili apate muda wa kusoma Qur’ani kwa wingi. Zubaid Al-Yami alikuwa akiwaunganisha Maswahaba ili kushindana katika kusoma Qur’ani na kuikamilisha mara kadhaa.

Wema waliotangulia (Allah awaridhie) walikuwa wakihimiza sana ibada za sunna, ikiwa ni pamoja na kufunga Saumu za kujitolea. Imamu Al-Shatibi, – Allah amrehemu- katika kitabu chake Al-Muwafaqat, alieleza kuwa ibada za sunna na za kujitolea ni njia ya kujitayarisha kwa ibada za faradhi (lazima) na kuzitimiza kwa namna inayomridhisha Allah Mtukufu.

Wema waliotangulia (As.Salaf As-Salih) walikuwa wakiwapendelea wengine katika kuwafuturisha wakati wa mwezi wa Ramadhani. Miongoni mwao ni Abdullah bin Umar, Daud Al-Tai, Malik bin Dinar, na Ahmad bin Hanbal. Ibn Umar (Allah amridhie) alikuwa hafungui saumu yake isipokuwa akijumuika pamoja na masikini na mayatima.

Kusimama usiku (Qiyamu Al-Layl)

 Mfano mashuhuri wa kufanya ibada ya usiku ni namna Uthman bin Affan (Allah aridhie) alivyokuwa akisoma Qur’ani nzima ndani ya usiku mmoja.

Kutambua umuhimu wa Ramadhani,

Muislamu anapaswa kuelewa umuhimu wa kujiandaa kwa mwezi wa Ramadhani kuanzia mwezi wa Rajab na Shaaban.

Ukarimu na ukunjufu wa moyo ni miongoni mwa sababu za kupata maisha mema, na mja hulipwa kwa wema wake. Inapaswa kufahamika kuwa utoaji hauishii tu kwa mali, bali (utoaji) una maana pana zaidi ya hivyo.

Mfano mashuhuri wa ukarimu wa watu wema waliotangulia ni hadithi ya Qais bin Sa’d bin Ubadah. Siku moja alipougua, watu walichelewa kumtembelea.

Alipouliza sababu, aliambiwa kwamba waliogopa kwenda kwa kuwa walikuwa na madeni kwake (kwa maana akiwadai). Akawaamuru watangaze kwamba amewasamehe wote waliokuwa na madeni yake.

 Kufanya kazi (amali njema) kwa ufanisi

Wema waliotangulia (Allah awaridhie) walikuwa wakihimiza kufanya kazi (amali njema) kwa ufanisi na umakini. Walikuwa wakisisitiza kuwa kazi (amali) ndogo iliyofanywa kwa umakini ni bora zaidi kuliko kazi kubwa isiyofanywa kwa usahihi.

Vilevile, Mama wa Waumini, Aisha (Allah amridhie), alikuwa analazimiana na kazi (amali) fulani hadi aipatie umakini wake wote na kuikamilisha kwa ufanisi.

Kujitenga kwa ajili ya Mwenyezi Mungu

Mwezi wa Ramadhani ni mwezi wa kiroho na ukaribu wa kipekee kwa Allah Mtukufu. Muislamu anapaswa kujitahidi katika siku hizi tukufu kujitenga na mambo ya dunia na kujielekeza kwa Allah Mtukufu kwa dhikr, ibada, na tafakuri.

Imeelezwa kuwa baadhi ya wema waliotangulia walikuwa wakiagana na wenzao katika siku za Ramadhani kwa sababu ya kujishughulisha kwao na itikafu, ibada ya usiku, na kumdhukuru Allah Mtukufu.

Kuwalisha watu ni mojawapo ya njia bora za kufanya wema, na Mtume wa Allah alihimiza sana tendo hili.

Ali bin Abi Talib (Allah amridhie) alisema: “Kwangu mimi, kuwakusanya watu miongoni mwa maswahaba wenzangu na kuwapa sahani moja ya chakula ni bora zaidi kuliko kwenda sokoni na kumnunua mtumwa kisha kumwacha huru.”

Muislamu anapaswa kuelekea kwa Allah Mtukufu peke yake katika mwezi wa Ramadhani na kujishughulisha na yeye tu. Chuki na uhasama kati ya watu husababisha madhara mengi, ikiwa ni pamoja na kizuizi cha kukubaliwa kwa matendo mema.

Imepokewa katika Sahih Muslim kutoka kwa Abu Huraira (Allah amridhie) kwamba Mtume wa Allah amesema:

“Milango ya Pepo hufunguliwa siku ya Jumatatu na Alhamisi, na husamehewa kila mja asiyemshirikisha Allah na chochote, isipokuwa mtu aliyekuwa na uhasama kati yake na ndugu yake. Husemwa (malaika watawaambia): ‘Waacheni hawa wawili mpaka wapatane, waacheni hawa wawili mpaka wapatane, waacheni hawa wawili mpaka wapatane.'”

Kwa hivyo, Muislamu anapaswa kuukaribisha mwezi wa Ramadhani kwa moyo safi, usiokuwa na chuki na uhasama, akifuata maadili mazuri yaliyohimizwa na Uislamu.

Related Posts