Serikali yagharamia mafunzo kwa bodaboda, bajaji 100 kuepusha ajali

Mwanza. Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta) Kanda ya Ziwa inawapa mafunzo ya nadharia na vitendo madereva bodaboda na bajaji zaidi ya 100, ili kuwaepusha na ajali ambazo asilimia 65 ya waathirika ni madereva hao.

Kwa mujibu wa tovuti ya Wizara ya Afya, waathirika wa ajali za barabarani ni watu wenye umri kati ya miaka 19 hadi 59, ambapo katika kipindi cha Juni 2023 hadi Machi 2024 majeruhi 11,434 waliohudumiwa kwenye hospitali 16 za rufaa za mikoa 16 nchini, huku asilimia 61 wakikuwa bodaboda.

Madereva Bodaboda na Bajaji wakimsikiliza Mkurugenzi wa Veta Kanda ya Ziwa, Janeth Nyoni wakati wa maadhimisho ya miaka 30 ya Veta. Picha na Saada Amir

Katika kipindi hicho, mikoa iliyoongoza kwa kuwa na majeruhi wengi ni Dar es Salaam, Morogoro, Mwanza, Dodoma na Kagera.

Akizungumza mbele ya madereva hao jana jijini Mwanza wakati wa maadhimisho ya miaka 30 ya kuanzishwa kwa Veta, Mkurugenzi wa Veta Kanda ya Ziwa, Janeth Nyoni amesema ajali nyingi za bodaboda zinatokea kwa kuwa wanajifunzia vijiweni na kuanza kutoa huduma kwa abiria, bila kuwa na ujuzi rasmi wa udereva.

“Madereva hawa wengi wanapata ajali, wanakufa na wengine wanapata vilema vya maisha kwa sababu wanajifunza mitaani bila kupitia vyuo vya mafunzo. Tunaamini mafunzo haya yatawasaidia kwa kuwa mtafundishwa theory (nadharia) na practical (vitendo) kisha mtapewa cheti,”amesema Nyoni.

Madereva Bodaboda na Bajaji wakimsikiliza Mkurugenzi wa Veta Kanda ya Ziwa, Janeth Nyoni wakati wa maadhimisho ya miaka 30 ya Veta. Picha na Saada Amir

 Nyoni amesema Serikali kwa kulitambua kundi hilo, imegharamia mafunzo hayo ya muda mfupi, akiwataka madereva hao kuwa mabalozi wazuri wanapokuwa kwenye shughuli zao za kuwahudumia abiria.

Naye, Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Hassan Masala amewataka madereva hao kutumia fursa na ujuzi walioupata vizuri pasipo kusababisha ajali kama wanavyolalamikiwa na watumiaji wengine wa barabara.

“Hatujaja hapa kupoteza muda, sikilizeni mafunzo kisha mkafanye kwa vitendo. Mkipata cheti mwende mitaani mkaendeshe kwa kuzingatia usalama wenu, wa abiria ambao ni lazima mfuate sharia za usalama barabarani,” amesema Masala

Mkurugenzi wa Veta Kanda ya Ziwa, Janeth Nyoni akizungumza wakati wa maadhimisho ya miaka 30 ya Veta yanayofanyika jijini Mwanza. Picha na Saada Amir

Mmoja wa bodaboda anayeshiriki mafunzo hayo, John Niclaus amesema awali hakuona umuhimu wa kuzingatia sheria za barabarani ikiwemo kufuata alama za barabarani, lakini baada ya kufundishwa atakuwa balozi kwa madereva wenzake wanaovunja sheria za usalama barabarani.

Maadhimisho hayo yameenda sambamba na uhamasishaji wanafunzi wa shule za sekondari umuhimu wa kujiunga na vyuo vya ufundi na upandaji miti kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Related Posts