Majeraha yamtibulia Camara Simba | Mwanaspoti

KIPA namba moja wa Simba, Moussa Camara ‘Spider’ kwa mara ya kwanza anatarajiwa atacheza mechi ya Ligi Kuu Bara kesho wakati timu hiyo ikiwa wageni wa Coastal Union, kutokana na kuwa majeruhi kama ilivyo kwa beki wa kati, Fondoh Che Malone.

Camara ametumika katika mechi 20 zilizopita za timu hiyo katika Ligi Kuu akiisaidia kushika nafasi ya pili ikiwa na pointi 51 nyuma ya Yanga inayoongoza kwa alama 55 baada ya mechi 21 na leo jioni itashuka tena uwanjani kuvaana na Pamba Jiji.

Katika mechi hizo 20 ambazo ni sawa na dakika 1,800 Camara amevuna clean sheets 15 akiruhusu mabao manane tu akiwa ndiye kinara wa Ligi Kuu kwa sasa.

Timu hiyo, kesho Jumamosi itakuwa wageni wa Coastal kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid baada ya awali kufungana mabao 2-2 katika mchezo wa kwanza ulipigwa KMC Complex, Dar es Salaam.

Akizungumza na Mwanaspoti, kocha wa Simba, Fadlu Davids alisema anatarajia kuwakosa wachezaji wangu wawili katika mchezo huo wa 21 kwa kikosi hicho na wa 22 kwa Wagosi wa Kaya msimu huu  kutokana na kusumbuliwa na majeraha.

“Nitamkosa kipa namba moja, Camara na beki Che Malone ambaye pia bado anaendelea kuwa chini ya uangalizi wa daktari baada ya kuumia kwenye mchezo wetu dhidi ya Azam FC,” alisema Fadlu na kuongeza;

“Natambua umuhimu wa wachezaji hao kikosini mwangu kutokana na mchango wao lakini naamini wachezaji waliopo pia watafanya kazi nzuri kuhakikisha tunapata matokeo na kuendelea kufukuzia ubingwa tunaouhitaji sasa.”

Alisema licha ya Camara kumaliza mchezo alipata maumivu ya mguu ambayo pia yanafanyiwa uchunguzi na daktari taarifa kamili zitatolewa, lakini ameweka wazi kuwa hatakuwa sehemu ya mchezo dhidi ya Coastal Union.

“Hatujasafiri nao wote wawili tumewaacha kwaajili ya kufanyiwa vipimo na kuanza matibabu haraka ili kuwa katika hali nzuri na kumalizia mechi zilizobaki.”

Wawili hao wote ni panga pangua kikosi cha kwanza cha Simba na ndio wachezaji waliocheza dakika nyingi zaidi msimu huu.

Kukosekana kwa Camara ni nafasi ya Aishi Manula na Ally Salim kuonyesha makali yao baada ya kukosa nafasi kwa muda mrefu tangu alipotua beki huyo akicheza mechi zote za ndani na nje.

Mcameroon huyo aliumia kwenye mchezo uliopita kati ya Simba na Azam FC aliotolewa dakika za mapema na nafasi yake kuzibwa na Chamou Karaboue, huku mechi ikiisha kwa sare ya 2-2.

Che Malone aliyesajiliwa misimu miwili iliyopita amekuwa beki tegemeo katika kikosi cha Simba kilichopita mikononi mwa makocha wanne akiwamo Fadlu aliyeshtushwa na tukio hilo linaloweza kumfanya Che Malone kuikosa Coastal Union na kuwa katika hatihati ya kuivaa Yanga.

Kikosi cha Simba kimeondoka alfajiri ya leo na kitfanya mazoezi ya mwisho leo kabla ya mchezo huo wa kesho.

Related Posts