Kibaha. Watu wenye ulemavu nchini wamesema ukosefu wa wataalamu wa lugha ya alama kwenye maeneo ya huduma za jamii huwafanya wapate huduma tofauti na walizokusudia.
Hayo yameelezwa leo Februari 28, 2025, wakati wa mafunzo ya afya ya uzazi kwa wanachama wa Shirikisho la watu wenye Ulemavu (Shivyawata) Kibaha, Mkoa wa Pwani.
Changamoto zingine zinazotajwa na watu wa kundi hilo, ambazo wanadai kuwa zinautweza utu wao, ni kutengwa, kubaguliwa, na kutoaminika ndani ya jamii na maeneo mbalimbali ya kutolea huduma za msingi.
Hili limewasukuma kuiomba Serikali iweke mikakati madhubuti ya kuondoa tatizo hilo.

Maeneo yaliyotajwa kuwa changamoto kwa watu wenye ulemavu ni yale yanayotoa huduma za afya, elimu, na taasisi mbalimbali za umma na binafsi.
Akieleza changamoto hizo, Mwenyekiti wa Shivyawata Wilaya ya Kibaha, Jabiri China, ametoa mfano wa hospitali, akisema wakati mwingine hufanyiwa vipimo tofauti na tatizo lililowapeleka, hasa kwa wenye ulemavu wa usikivu.
“Leo hii mtu mwenye ulemavu wa kiziwi akifika hospitali kupata matibabu anapata changamoto kubwa hadi kupata huduma. Utakuta wahudumu hawajui lugha ya alama, sasa hadi wafikie maelewano inakuwa shida kubwa, na wakati mwingine anaweza kuondoka bila kutibiwa,” amesema China.
Kwa mujibu wa China, ili kupata suluhisho la tatizo hilo, Serikali inatakiwa kuzingatia pendekezo lao la kuingiza kipengele cha somo la lugha ya alama kuanzia shule za msingi hadi sekondari.
Amesema pendekezo hilo lina umuhimu mkubwa wa kuwezesha wanafunzi kupata uelewa kuhusu lugha ya alama, itakayowasaidia katika maisha yao baada ya shule.
“Hata kabla ya kuanza kwa mtalaa huo, hivi sasa kuna umuhimu wa Serikali kuwaweka wataalamu wa lugha za alama kwenye maeneo yote ya kutolea huduma, ikiwemo hospitali, TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania), na Tanesco.
“Maeneo mengine yote muhimu, hata mahakamani, hii itasaidia watu wenye ulemavu wa aina hiyo kuwa huru na kupata uelewa pindi wanapofika kupata huduma hizo,” amesema.
Kwa upande wake, Violeth Sarali amesema jamii bado inaendelea kuwabagua watu wenye ulemavu ukilinganisha na wasio na changamoto hiyo, huku wakisahau kuwa kila mtu ni mlemavu mtarajiwa.

“Miaka miwili iliyopita nilienda hospitali moja, sitaitaja jina, lakini nilijisikia vibaya baada ya kusikia maneno magumu juu yangu. Wakasema, ‘Hivi wanaume hawana huruma hadi wanawapa ujauzito watu wenye ulemavu? Iliniuma sana,” amesema.
Amesema alibaini jamii inawaona watu wenye ulemavu kama wasio na haki ya kuzaa wala kupata wenza, jambo ambalo linapaswa kupigwa vita ili kuweka usawa baina ya watu wa kundi hilo na wasio na ulemavu.
Akizungumza kwa niaba ya Sudi Mohamedi, mjumbe wa Kamati ya Siasa Mkoa wa Pwani, amesema kuwatenga wenye ulemavu ni jambo linalopaswa kupigwa vita, kwani hakuna anayejua hatima ya maisha yake.
“Sisi sote hapa ni walemavu watarajiwa, hivyo ni vema tukashirikiana vyema na wenzetu ambao wamekutwa na hali hii,” amesema.
Ofisa Tarafa wa Kiponzelo, Catherine Njau, ambaye alizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, amesema Serikali inaendelea kuzifanyia kazi changamoto hizo hatua kwa hatua ili kuhakikisha zinatatulika.
“Hata hizi changamoto mlizowasilisha nazibeba, nitazifikisha kunakohusika, naamini zitafanyiwa kazi,” amesema.