Dar/mikoani. Wakati mfungo wa mwezi Mtukufu wa Ramadhan ukitarajiwa kuanza, waumini wa dini ya Kiislam wameaswa kutumia mfungo huo kutenda mema, kusaidia wenye uhitaji, kutii mamlaka na kuwaombea viongozi wa dini na Serikali kama sehemu ya ibada ya kumrejea Mungu.
Pia, viongozi hao wa dini ya Kiislam wamewataka waumini wao kuliombea Taifa liendelee kuwa na amani na mshikamano kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu.
Wakizungumza na Mwananchi viongozi wa dini hiyo kutoka mikoa mbalimbali wamewaasa Waislam wenye uwezo wa kufunga kufanya hivyo huku, wakiwataka wafanyabiashara kutopandisha bei za bidhaa kwa sababu mfungo huo ni moja ya nguzo muhimu ya dini.
“Swaumu ina mambo mengi ikiwa ni pamoja na kutimiza moja ya nguzo kuu ya Uislamu; hivyo niwaombe Waisilamu wote wahakikishe tunaanza mfungo na kumaliza salama huku tukitegemea kupokea thawabu,” amesema Sheikh wa Mkoa wa Mara, Kassim Msabaha
Sheikh wa Mkoa wa Kagera, Haruna Kichwabuta amewataka waumini wa dini ya Kiislam kutumia mfungo huo kuombea Taifa amani wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, huku akiwasihi Watanzania kila mmoja kwa eneo na nafasi yake akitimiza wajibu wa kuhakikisha uchaguzi huo unakuwa wa amani na utulivu.
‘’Tuiombee Taifa letu tufaye uchaguzi wa amani na utulivu…yaani kila mmoja atambue kuna maisha baada ya uchaguzi. Wasiupelekee uchaguzi kama ndio mwisho wa maisha ya binadamu,” amesema Sheikh Kichwabuta
Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (Bakwata), Sheikh Khamis Mataka amewataka Waislamu kukitumia kipindi hiki cha mwezi mtukufu kuimarisha tabia njema.
“Mwezi wa Ramadhani ni chuo cha tabia njema, basi, shime tuimarishe kiwango chetu cha tabia njema ili tuupokee Mwezi Mtukufu wa Ramadhan tukiwa waja wema watakaonufaika na Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kupitia kufanya ibada mbalimbali.
“Unakuta mtu ana swali Swala Tano, anafunga Swaumu ya Ramadhani, anatoa Zakkah lakini hana tabia njema: anatukana watu, anavunja heshima za watu, anawadhulumu watu, anawasingizia watu, anaua watu, anapiga watu kwa dhuluma. Ibada zake alizozifanya vyema hazimsaidii kwa kukosa tabia njema” amesema Sheikh Mataka ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Taasisi ya Masheikh na Wanazuoni wa Kiislamu Tanzania.
Sheikh wa Mkoa wa Kigoma, Hassan Kiburwa amesema pamoja na ibada, kushiriki matendo ya huruma kwa kusaidia wenye uhitaji, mfungo wa Ramadhani pia hutumika kutoa mafunzo maalum kwa waumini kuhusu umuhimu wa utii kwa viongozi wa dini, kijamii na Serikali.
“Katika mwezi huu tutakuwa na program za kufundisha watu namna ya kuzoea mambo ya kufanya utiifu kwa Mwenyezi Mungu, utiifu kwa Taifa na kuwasaidia viongozi kutenda mema,’’ amesema Sheikh Hassan.
Sheikh wa Mkoa wa Shinyanga, Ismail Makusanya amesema pamoja na kufunga, Waislam pia wanatakiwa kuepuka mambo yanayomchukiza Mungu, huku kila wakati wakijitahidi kuepuka kuwa chanzo cha magomvi ndani ya jamii.
Sheikh wa Mkoa wa Mwanza, Hassan Kabeke amewataka Waislam kutambua thamani ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwa kuacha kutenda matendo maovu kwa sababu funga bila kutenda mema ni sawa na kutofunga.
‘’Tutumie mfungo wa Ramadhani kuwa chachu ya kuishi katika matendo mema kwa mwaka mzima…tutende mema na kuwasaidia wahitaji,’’ amesema Sheikh Kabeke.
Shekhe wa Kata ya Ikungi na Mwenyekiti wa Kamati ya Maridhiano Sheikh Salum Ngaa ametaja mambo matatu ambayo Waislam wanapaswa kuyafanya katika kipindi cha kuingia mwezi Mtukufu wa Ramadhan.
Mambo hayo ni pamoja na kuacha maovu yote na kuwa watenda mema ili wajiepushe na moto, waache magomvi na badala yake wawe watu wa kusamehe lakini wawe tayari kutekeleza nguzo za dini hiyo.
Sheikh Ngaa amesema katika kipindi cha mfungo kila hatua ina miiko yake, lakini akataja kumi la kwanza kwamba hutumika zaidi katika kuwaweka sawa Waislam na kuwaepushia adhabu hasa wakijitofautisha na maovu.
“Kwanza wajiandae kikamilifu, pili ili kufunga inakutaka uwe na nia hasa ya kufunga siyo kuacha kula na kunywa pekee halafu ndiyo useme upo kwenye misingi, hapa hata ukichokozwa na mtu mwambie mimi nimefunga naomba kukusamehe,” amesema Ngaa.
Hata hivyo, amesisitiza kwa watu ambao watakuwa tayari na wasiokuwa na makwazo kwamba ni lazima kufunga na wasifanye visingizo ambavyo vinakwenda kuwazuia kuingia kwenye mfungo.
Sheikh Mussa Mabuga yeye anasema hiki ni kipindi cha muislamu kumrudia Mungu awe na ndiyo muda wa kukumbushwa kuwa inawapasa kuwa watenda mema siyo kwa ajili ya kuiona pepo, bali wawe sehemu ya kusababisha na wengi kuiona.
Sheikh Mussa anasema upole na kutokuwachokoza watu wengine ndiyo msingi wa hayo yote lakini kukumbuka muda wa kuwa karibu na muumba kwenye nguzo zote tano.
Kwa mujibu wa kiongozi huyo wa dini, mara nyingi watu hujitahidi kuwa karibu na misingi ya dini lakini wanasahau familia zao wala watu wanaoishi nao ambao mara nyingi huwaacha majumbani wakati wao wanakwenda kuswali.
Kwa upande wake Sheikh Ibrahim Bombo amesema mwezi wa Ramadhani ni wa kipekee kuanzia ibada na matendo akiwaomba Waislamu kutumia nafasi hiyo kuchuma baraka.
Amesema itakuwa ni dhambi kwa wajasiriamali wanaouza futali kupandisha bei wakiamini waliofunga lazima kununua akieleza kuwa hali hiyo itaondoa baraka katika biashara kwakuwa itakuwa tofauti na maelekezo ya Quruan.
“Watanzania wote watumie mwezi huu kufanya ibada na matendo yaliyo mema, waepuke kufanya yale ambayo yanaweza kuwaondoa katika baraka za Mungu” amesema Sheikh Bombo.
Ujumbe kwa wafanyabiashara
Kadhi wa Mkoa wa Mbeya, Sheikh Hassan Mbarazi amewataka na kuwaomba wafanyabiashara kutopandisha bei ya bidhaa sokoni kwani kufanya hivyo ni kinyume na utaratibu akieleza kuwa mfungo wa Ramadhani una neema kubwa kwa kwa binadamu.
“Waislamu wapikee mwezi huu kwa amani, wajiandae vyema kwa kufanya toba na ku.rejea Mungu, sisi viongozi tunawatakia maandalizi na mwanzo mwema wa Ramadhani, wafanyabiashara wasipange kupandisha bei bidhaa” amesema Sheikh huyo.
Wito kwa wafanyabiashara kutopandisha bei ya bidhaa zinazotumika kwa wingi wakati wa mfungo pia imetolewa na Sheikh wa Mkoa wa Simiyu, Sheikh Issa Kwezi akisema kitendo cha kupandisha bei ya bidhaa inaweza kuwa kikwazo kwa ibada ya mfungo wa Ramadhani.
Kuhusu bei za bidhaa, Sheikh Kichwabuta amewasihi wafanyabishara kuepuka tabia ya kupandisha bei kipindi cha mfungo wa Ramadhani.
Imeandikwa na Saada Amir (Mwanza), Amina Mwambo (Shinyanga), Beldina Nyakeke (Mara), Gofrey Chubwa (Kigoma) na Samweli Mwanga (Simiyu), Sadam Sadick (Mbeya), Habel Chidawali (Dodoma) na Elizabeth Edward (Dar).