Padri Mwang’amba afariki dunia | Mwananchi

Unguja. Padri wa Kanisa Katoliki Jimbo la Zanzibar, Anselmo Mwang’amba amefariki dunia Februari 27, 2025 kisiwani hapa.

Taarifa iliyotolewa na Askofu Mkuu jimbo hilo, Agustino Shao imesema mipango ya mazishi inaendelea.

“Roho ya padri Anselmo Mwanga’mba ipate rehema kwa Mungu ipumzike kwa amani,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Februari 28, 2025, Katibu Mkuu wa Jimbo hilo, Padri Cosmas Shayo amesema wapo kwenye vikao vya mazishi.

Amefafanua kuwa maziko yanatarajiwa kufanyika Jumanne Machi 4, 2025 Kitope Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Hata hivyo, hakutaka kuzungumza zaidi kuhusu msiba huo kwa kile alichoeleza bado wapo kwenye vikao vya mipango.

“Taarifa zaidi tutatoa baadaye kwa sasa bado tunaendelea na vikao,” amesema.

Itakumbukwa mwaka Septemba 2013, padri Mwang’amba alimwagiwa tindikali na kulazwa katika Hospitali ya Mnazimmoja kisha kuhamishiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Tukio hilo lilitokea katika Mtaa wa Mlandege Mkoa wa Mjini Magharibi na kujeruhiwa usoni, kifuani na mkononi.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana wakati huo, kiongozi huyo wa kiroho alikuwa akitoka katika duka la huduma za mawasiliano ya mtandao wa simu saa 10:15 jioni na watu waliommwagia walimtega mlangoni kabla ya kufanya uhalifu huo, kisha kutokomea kwenye vichochoro vya mitaa ya mtendeni na Mchangani.

Katibu Mkuu wa Anglikana, Padri Stanley Lichinga amesema japo kifo ni mipango ya Mungu, lakini pengo lake haliwezi kufutika.

“Ametumika na amefikia wakati wa kutuaga roho yake ilazwe pema, hatuwezi kukataa kwamba asiondoke wakati wa kuondoka umefika tusimkufuru mungu,” amesema.

Related Posts