Arusha. Mahakama ya Rufani, imemng’ang’ania mkazi wa Kijiji cha Upendo, wilayani Chunya Mkoa wa Mbeya (jina linahifadhiwa), aliyembaka binti yake wa kumzaa aliyekuwa na umri wa miaka 12, baada ya kurudi nyumbani akiwa amelewa ikisisitiza kifungo cha miaka 30 jela alichopewa ni sahihi.
Tukio hilo lilitokea kijijini humo Desemba 24,2019 ambapo mwanaume huyo aliyekuwa ametengana na mke wake, alikuwa akiishi na watoto wake wawili wa kike na siku ya tukio, alirudi nyumbani akiwa amelewa akamwita binti yake chumbani, akamvua nguo na kumbaka.
Hukumu hiyo ilitolewa Februari 25, 2025 na jopo la majaji watatu walioketi jijini Mbeya, ambao ni Winfrida Korosso, Panterine Kente na Leila Mgonya.
Rufaa hiyo ya jinai namba 618 ya mwaka 2021, ni ya pili ambapo awali Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, iliridhia adhabu aliyopewa mrufani huyo, ambaye awali alihukumiwa adhabu hiyo na Mahakama ya Wilaya ya Chunya.
Katika hukumu hiyo ya Mahakama ya Rufani, watoto wawili wa mrufani akiwemo mwathirika wa tukio hilo ndio waliotoa ushahidi uliommaliza baba yao.
Kulingana na hukumu hiyo, mtoto huyo aliieleza Mahakama ya Wilaya ya Chunya kuwa mama yake na baba yake walitengana mwaka 2016 na siku ya tukio wakiwa wanaishi katika nyumba ya kupanga na baba yao, wao walikuwa wakilala sebuleni na baba yao akilala chumbani.
Alisema kuwa baba yao alirudi nyumbani akiwa amelewa, akamwamsha na kuingia naye chumbani kwake, akamuamuru avue nguo akambaka, na licha ya kupiga kelele kutokana na maumivu aliyokuwa akipata hakupata msaada wowote.
Mtoto huyo alieleza kuwa siku iliyofuata alikwenda kwa bibi yao aliyekuwa akiishi jirani na kumweleza kuhusu suala hilo, ambapo bibi huyo alitoa taarifa kwa Mtendaji wa Kijiji, kisha kukamatwa mtuhumiwa huyo.
Shahidi wa tatu (mdogo wa mwatahirika wa tukio hilo), alisema akiwa amelala sebuleni alisikia kilio cha dada yake kikitoka chumbani, lakini aliendelea kulala.
Mahakama hiyo ya rufani imekibariki kifungo anachoendelea kukitumia mrufani huyo cha miaka 30 jela, baada ya kujiridhisha kuwa upande wa mashitaka ulijiridhisha bila kuacha shaka kuwa alitenda kosa hilo.
“Katika tukio hilo, tunaona kesi ya upande wa mashitaka dhidi ya mrufani imethibitishwa pasipo shaka yoyote na hivyo kutupilia mbali rufaa hiyo kwa kutokuwa na sifa,” amesema Jaji Korosso.
Ni kutokana na ushahidi wa watoto wake hao wawili na mashahidi wengine akiwemo daktari aliyemfanyia uchunguzi mtoto, mshtakiwa alitiwa hatiani na kuhukumiwa miaka 30 jela, ambapo wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo katika mahakama ya chini mrufani huyo alikana kutenda kosa hilo na kudai ushahidi dhidi yake ulitungwa.
Hata hivyo, hakuridhika na hukumu hiyo ambapo alikata rufaa ya kwanza Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya ambayo ilitupilia mbali rufaa yake kisha akakata rufaa ya pili Mahakama ya Rufani akiwa na sababu tisa.
Katika rufaa yake ya kwanza mrufani huyo alikuwa na sababu nane ikiwemo Mahakama kushindwa kuzingatia utetezi kwa kutegemea tu ushahidi wa upande wa mashitaka, kutozingatia kuwepo kwa ugomvi wa kifamilia na chuki kati ya wanandoa waliotengana, ambayo inaweza kusababisha mashitaka kama hayo.
Nyingine zilikuwa ni kushindwa kuchambua ipasavyo mashaka yaliyotokana na ushahidi wa pili na tatu, kuhusu tukio na kutegemea ushahidi huo, kushindwa kuchambua ipasavyo ushahidi wa mashitaka na kushindwa kuwaita mashahidi muhimu (wapangaji wenza, bibi au jirani).
Katika Mahakama ya Rufani mrufani huyo alikuwa na sababu tisa za rufaa ikiwemo kushindwa kutathimini ushahidi wa upande wa mashitaka, upande wa mashitaka kutoita ushahidi wa mashahidi muhimu kama vile majirani pamoja na kushindwa kuzingatia utetezi wake kuwa shitaka hilo lilikuwa la kutengenezwa kutokana na uhusiano mbaya na shahidi wa kwanza (mama wa watoto wake).
Katika rufaa hiyo, mrufani huyo hakuwa na uwakilishi wa wakili na badala yake alijiwakilisha mwenyewe huku upande wa mashitaka ukiwa na mawakili wawili.
Baba huyo alisisitiza kuwa kesi hiyo ilipangwa dhidi yake na aliyekuwa mke wake kwa vile walikuwa na ugomvi kuhusu nani anafaa kuwalea watoto wao.
Jopo la majaji hao watatu ilitupilia mbali sababu hizo na kueleza kuwa imeridhika kuwa upande wa mashitaka uliweza kuthibitisha shitaka hilo kwa viwango vinavyokubaliwa kisheria, na ushahidi wa watoto ukiwemo wa mwathirika wa tukio hilo ulitosha kumtia hatiani.