Tanga. Rais Samia Suluhu Hassan amesema miongoni mwa matamanio yake ni kuurejesha Mkoa wa Tanga kuwa wa viwanda, kama ulivyowahi kuwa kabla.
Katika kulifanikisha hilo, amesema tayari Serikali imeanza kuchukua hatua za kupanua viwanda vilivyopo na kujenga vipya ili kutoa fursa za ajira kwa wananchi.
Kauli hiyo ya Rais Samia, inajibu ombi la Mbunge wa Tanga Mjini, Ummy Mwalimu aliyetaka Serikali iurudishe mkoa huo kuwa wa viwanda na hivyo kutoa fursa ya ajira kwa wananchi.
Hata hivyo, mkuu huyo wa nchi amesema mkakati huo pia, utaleta suluhu ya changamoto ya ajira na kupunguza watu wanaokaa vijiweni kunywa kahawa na kupiga umbea.

Rais Samia ameyasema hayo leo, Ijumaa Februari 28, 2025 alipohutubia mkutano wa hadhara wa kuhitimisha ziara yake ya siku sita mkoani Tanga, katika Uwanja wa CCM Mkwakwani.
Ameigawa hotuba yake hiyo katika maeneo matatu, ya matamanio yake kuhusu Tanga, aliyoyabaini na majibu ya changamoto zilizobainishwa na viongozi.
Kuhusu matamanio yake, amesema ni kiu yake kuirudisha Tanga ya viwanda kama ilivyowahi kuwa katika miaka iliyopita.
“Kwanza ninatamani kuirudisha Tanga ya viwanda kama ilivyokuwa huko nyuma, hili ndilo tamanio langu kubwa,” amesema.
Amesema tayari kuna hatua zimeshaanza kuchukuliwa kwa baadhi ya viwanda kuanza kufanyiwa upanuzi na vingine vinajengwa upya.

Ameahidi kulegeza masharti ya uwekezaji ili kuwavutia wawekezaji wengi zaidi na hatimaye kutengeneza fursa lukuki za ajira kwa vijana wa mkoa huo.
“Hiyo ndio Tanga ninayotamani kuirudisha ili vijana wetu wapate ajira na Tanga kusiwe na watu wanazubaa kwenye vijiwe kunywa kahawa na kupiga majungu hapana,” amesema.
Ameliambatanisha tamanio lake hilo na kile alichoeleza, amebaini kuwepo kwa mashamba makubwa yasiyotumika wala kuuingizia chochote mkoa huo.
Kwa mujibu wa Rais Samia, kuwepo kwa mashamba hayo kunatokana na kutoendelezwa na wawekezaji waliobinafsishiwa.
Kwa sababu hiyo, amesema ameshaiagiza Ofisi ya Msajili wa Hazina na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kupitia upya vipengele vyote vya mikataba ya ubinafsishwaji na kubainisha iwapo mienendo ya wawekezaji hao haivunji masharti ya mikataba yao.
Amesema kama wamevunja, ofisi hizo zishauri hatua za kuchukuliwa kwa mujibu wa masharti ya mikataba husika.
“Pia, ofisi hizo zieleze hatua zinazopaswa kuchukuliwa ili kuona namna ya kusaidia viwanda ili ajira zitengenezwe,” amesema.
Msingi wa agizo lake hilo, amesema ni kuona mashamba na viwanda vilivyopo zinachukuliwa hatua nyingine ili kutengeneza ajira.
Amesema mkoa huo una mashamba na viwanda vingi, lakini havichangii chochote kwa Serikali na hata kuwasaidia wananchi.
“Hali hii lazima ifike mwisho, tunataka wakulima wapate soko la mazao yao, lakini tuwawezeshe wazalishe kwa wingi,” ameeleza.
Tamanio lake lingine kwa Tanga, amesema ni kuuona unakuwa wa utalii wa fukwe, historia na utamaduni.
Amesema kwa mandhari ya Tanga inatosha kuwa kivutio cha utalii, kupitia fukwe zake, milima na utajiri wa kihistoria kwa kuzingatia hulka na asili ya ukarimu.
“Naamini Tanga inaweza kuwa kituo kikubwa cha utalii wa fukwe, historia kwa sababu kuna mapango ya Amboni, magofu ya Pangani, misikiti ya kale, watu mashuhuri kama Shaaban Robert,” amesema.
Marehemu Sheikh Shaaban Robert alikuwa mtaalamu wa ushairi na mtunzi wa vitabu aliyezaliwa Januari Mosi mwaka 1909 katika Kijiji cha Vimbarani jirani na Kijiji cha Machui kilichopo kilomita 10 kutoka kusini mwa jiji la Tanga.
Alifariki dunia Juni 22, 1962 na kuzikwa Machui. Amewahia kuandika vitabu 22 vikiwa vya kusadikika, kufikirika na maisha ya baada ya miaka 50

Amesema ili ndoto hiyo itimie lazima wananchi wa waendelee kuwa wamoja, kadhalika chama (CCM) na Serikali vizungumze lugha moja.
“Kwa upande wa wananchi changamkieni fursa zitokanazo na ndoto hii, kwa mfano bandari kuna fursa ikiwemo uwakala wa forodha jifunzeni taratibu za kuwa wakala wa forodha bandarini ili kunufaika na fursa hizi.
“Haipendezi tunatanua fursa za kiuchumi, halafu watu wanatoka mikoa mingine kuja kunufaika na fursa hizo, Tanga jipangeni,” amesema.
Amewataka wananchi wa Tanga kuchangamkia fursa za utalii kwa kujifunza taaluma zinazohusu uongozaji wa utalii, masuala hayo sambamba na kufungua kampuni za kitalii.
“Ndugu zangu naondoka Tanga nikiwa na ari ya kubwa ya kuendelea kuwatumikia Watanzania kwa bidii zaidi. Nimewaeleza kwa kifupi maono yangu ya Tanga ijayo, kwamba ni Tanga ya viwanda, iliyofunguka kiutalii, Tanga yenye uzalishaji zaidi wa mashambani na viwandani na Tanga iliyofunguka kwa kuunganishwa na njia za usafiri ili kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na watu,” amesema.
Katika ziara yake hiyo, amesema ameona kazi iliyofanywa, pia changamoto katika utekelezaji wa baadhi ya miradi.
Kutokana na hilo, amewataka maofisa masuhuli wanaosimamia miradi mbalimbali wafuatilie kwa karibu ili ikamilike haraka kama ilivyopangwa.
Katika ziara hiyo, amesema amebaini kuwepo kwa masuala kadhaa katika mkoa huo, ikiwemo changamoto za baadhi ya miundombinu ya barabara.
Kwa kuwa CCM mwaka huu inaandaa ilani ya mwaka 2025/30, amesema maombi mbalimbali ya barabara yataingizwa kwenye ilani hiyo.
Pia, amesema ameshuhudia usambazaji wa maji ni kati ya asilimia 75 hadi 78 na kwamba anatarajia miradi mingine ikitekelezwa yatawafikia asilimia 90.
Amesema Serikali imeanza kufufua bandari ya Tanga ili kuongeza fursa za ajira za vijana wa Tanga na baadaye wataifanya kuwa maalumu kwa mbolea na mazao ya kilimo.
Rais Samia amesema kupitia sera za biashara na uwekezaji, Serikali inaendelea kuvutia wawekezaji wakubwa Tanga na kuongeza fursa za ajira kwa wananchi.
Ameahidi kuongeza uzalishaji wa korosho, kokoa na viungo, mazao ambayo yana soko kubwa duniani.
“Niombe Tanga, waweke jitihada kubwa katika uzalishaji wa mazao haya kwa sababu yana bei kubwa duniani,” amesema.
Amesema katika mkoa huo ameona usikivu hafifu wa redio ya TBC na mawasiliano ya simu na kwamba mradi wa kuimarisha usikivu huo umefikia hatua nzuri.
Rais Samia amesema katika mkoa huo ameshuhudia migogoro ya ardhi inayochoshwa na kuwepo kwa mashamba makubwa yasiyozalisha.
Awali, Mbunge wa Tanga Mjini, Ummy Mwalimu ametumia dakika zake tano za salamu kumwomba Rais Samia arejeshe historia ya Mkoa wa Tanga kuwa wa viwanda kama ulivyokuwa miaka ya 1980.
Ameomba alifanye hilo kwa kufufua viwanda vya chuma, mbolea, saruji, mablanketi na mkonge ili wananchi wa Tanga wapate ajira.
“Najua huruma yako mama yangu (Rais Samia) ukirudi Ikulu Oktoba, tunakuomba utubariki na viwanda,” amesema.
Lingine aliloomba ni kuanzishwa kwa Chuo Kikuu jijini humo, akipendekeza kiitwe Shaaban Robert, akisema kuna eneo la ekari 1,000 linaloweza kutumika kwa ajili ya hilo.
“Makao makuu ya mkoa yanapaswa kuwa na chuo kikuu, utakaporudi Ikulu, tunakuomba utubariki na chuo kikuu na sisi watu wa Tanga tunapendekeza kiitwe Chuo Kikuu cha Shaaban Robert ili kulinda na kuenzi heshima ya mzee wetu,” amesema.
Katika hotuba yake hiyo, Ummy pia amefanya kama alivyofanya January Makamba, kwa kumshukuru Rais Samia kwa nafasi za uteuzi katika wizara mbili tofauti alizowahi kumpa.
“Nitaienzi na kuzitunza heshima hii Samia, kupitia kufanya kazi chini yako, nimeona dhamira, kiu na huruma yako ya kuboreshea maisha Watanzania,” amesema.

Makamba alifanya hivyo, katika salamu zake alizotoa katika mkutano wa hadhara wa Rais Samia alipokuwa Lushoto.
Amesema iwapo Barabara ya Tanga-Pangani itawekwa lami, itawezesha fukwe za Tanga kuwa na manufaa kiuchumi.
Imeandikwa na Juma Issihaka, Bakari Kiango na Rajabu Athumani