SIKU chache baada ya kutangazwa kuwa meneja wa Singida Black Stars, straika nyota wa zamani wa Simba na Yanga aliyeacha alama katika Ligi Kuu, Amissi Tambwe amevunja ukimya na kuteta na Mwanaspoti, akisema amefanya uamuzi sahihi kukubali ofa hiyo na wala hakukurupuka tu.
Tambwe alitua nchini kwa mara ya kwanza Julai, 2013 na alisaini mkataba wa miaka miwili wa kuitumikia Simba kabla ya baadaye kuongeza mkataba mwingine ambao hata hivyo hakuumaliza kufuatia kutemwa mwishoni mwa 2014 na kutua Yanga baadae akatua DTB FC inayoshiriki Ligi ya Champonship (zamani Ligi Daraja la Kwanza) na kuibuka kinara wa upachikaji mabao.
Akizungumza na Mwanaspoti, Tambwe alisema amefanya uamuzi wa kuwa meneja wa timu hiyo baada ya kustaafu kucheza soka aliloweka wazi kuwa amecheza kwa mafanikio.

“Kwa sasa nimestaafu soka, nimepata sehemu nzuri ya kuisha maisha ya soka napenda mpira hivyo kuwa meneja bado naendelea kuyaishi maisha ha na nasimamia kitu ninachokipenda, nilifurahi sana baada ya kupata nafasi hii,” alisema na kuongeza;
“Naushukuru uongozi wa Singida Black Stars kwa kuthamini na kutambua umuhimu wa mimi kuitumikia timu hii kwa kuwasimamia wachezaji, nina furaha nimekutana na wachezaji wengi ambao nimecheza nao na tulikuwa tunafanya kazi vizuri.”
Tambwe alisema atatumia nafasi aliyopewa kufanya kazi nzuri na wachezaji ambao ameweka wazi wamekuwa wakimpa heshima na kumsikiliza kutokana na namna waliyoishi pamoja wakiwa wachezaji na sasa ana majukumu mengine.

Katika msimu mmoja na nusu Simba (2012/13), Tambwe alifunga hat-trick mbili na kuacha rekodi ya kipekee ambayo hata hivyo ilifikiwa na Ibrahim Ajibu msimu uliofuata.
Msimu huo, alifunga hat-trick dhidi ya Mgambo JKT na Simba ilishinda mabao 6-0, akifunga manne, kabla ya kufunga nyingine dhidi ya JKT Oljoro iliyolala 4-0.
Tambwe alionekana wa moto zaidi Yanga alikocheza na kufunga jumla ya hat trick nne, akifunga mbili katika miezi sita ya mwanzo kabla ya kufanya hivyo tena msimu uliofuata.

Katika mwaka mmoja na nusu Simba, hakushinda taji Ligi Kuu, licha ya kumaliza kama mfungaji bora msimu wa 2013/14, Wekundu hao wakimaliza nafasi ya nne nyuma ya mabingwa Azam, Yanga na Mbeya City.
Hata hivyo, Tambwe alifatwaa taji la Nani Mtani Jembe lililokuwa maalumu kwa Simba na Yanga akifunga mabao mawili katika mechi hiyo mwishoni mwa 2013 na kulitetea mwaka 2014.