Mbeya. Mama mzazi wa mwandishi Furaha Simchimba, aliyefariki dunia katika ajali iliyoua wanne, Yusta Mwaisakila amejikuta akipoteza fahamu kwa muda kwenye mazishi ya mwanaye, huku vilio na simanzi vikitawala wakati wa kumpumzisha marehemu huyo.
Simchimba ni miongoni mwa watu wanne waliofariki dunia Februari 25 katika ajali iliyohusisha gari la Serikali na basi la Kampuni ya CRN wakati msafara wa CCM ukitoka kumsindikiza Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Taifa, Fadhil Rajabu.
Katika ajali hiyo watu watatu walifariki dunia papo hapo ambao ni Simchimba, Mjumbe wa kamati ya utekelezaji CCM Wilaya ya Rungwe, Daniel Mselewa na utingo wa basi, Isaya Geazi. Dereva wa Mkoa na Thadei Focus aliyefariki dunia wakati akipatiwa matibabu na wengine sita walijeruhiwa.

Mama mzazi wa marehemu Furaha Simchimba Yusta Mwaisakila akiwa ameshikiliwa baada ya kuzimia wakati wa mazishi ya mwanaye aliyefariki wakati wa ajali iliyotokea Februari 25, 2025 katika ziara ya CCM mkoani Mbeya. Picha na Saddam Sadick
Katika mazishi ya mwandishi huyo, ambayo yaliongozwa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya, Patrick Mwalunenge ulishuhudiwa mamia ya wananchi walijitokeza kushiriki mazishi hayo yaliyofanyika kwenye makaburi ya Lumbila jijini humo.
Katika shughuli ya mazishi hayo, mama mzazi, Yusta alijikuta akipoteza fahamu kwa muda, huku akipewa msaada na wasaidizi wake kumpepea na kumfariji.
Akizungumza wakati wa ibada ya kuuaga mwili huo katika Kanisa la Molaviani Kata ya Iyunga, Mwalunenge ametoa salamu za pole kwa familia, akiwaomba kuwa wastahimilivu katika kipindi hiki kigumu.

“Tumtangulize Mungu wakati wote kwa kuwa ni kipindi kigumu sana, Chama Cha Mapinduzi kitaendelea kuwa na nyie katika kuomboleza msiba huu mzito,” amesema Mwalunenge.
Msemaji wa familia, Esau Godwine amewashukuru wananchi kwa faraja zao akieleza kuwa mipango yote mwamuzi ni Mungu akiomba kuendelea kufarijiana wakati wote.