YANGA imejipigia Pamba Jiji kwa mabao 3-0 ikiendelea kujitanua juu ya msimamo wa Ligi Kuu Bara, lakini mashabiki wa timu hiyo wamekata kiu baada ya kumuona staa mpya, Jonathan Ikangalombo ‘Ikanga Speed’ kwa mara ya kwanza.
Ikangalombo aliyesajiliwa na Yanga kupitia dirisha dogo la usajili hakuwahi kucheza mchezo wowote huku utetezi mwingi ukitoka kwa makocha wawili tofauti, kuanzia Sead Ramovic na sasa Hamdi Miloud.
Lakini leo katika pambano hilo dhidi ya Pamba lililopigwa kwenye Uwanja wa CCm Kirumba, Mwanza, kocha Hamdi aliwasapraizi mashabiki kwa kumuanzisha benchi kabla ya kumuingiza uwanjani dakika ya 69 akimpokea Clement Mzize.
Kiungo huyo akitumika kwa dakika 21 za kwanza ndani ya Yanga ambapo dakika 90 zilipomalizika ziliongezwa nne ambazo winga huyo kutoka AS Vita alikiwasha kwa kuonyesha kiwango bora akigusa mpira mara 13 ambapo kwenye maeneo yote alipoteza mpira mara mbili pekee kwa pasi zake kutofika.
Ikanga aliyepachikwa jina la utani la Ikanga Speed alionyesha kitu kusadiki jina hilo akiwa mzuri kwa kasi akifanya hivyo mara nne kwa nyakati tofauti.
Mchezaji huyo alipiga krosi moja ambayo ilihusika kutengeneza bao la pili dakika 74, alipomchungulia Mkongomani mwenzake Maxi Nzengeli upande wa pili ambaye naye alipiga krosi nyingine iliyomkuta Stephanie Aziz KI na kufunga bao kwa kichwa.
Winga huyo ni mzuri pia kwa kutoa pasi za mwisho ambapo ndani ya mchezo huo alitengeneza moja nzuri, lakini Aziz KI akashindwa kuitumia kumalizia akipiga shuti rahisi lililodakwa na kipa Yona Amos.