Straika KVZ hashikiki ZPL, atupia manne akiiua Maendeleo

STRAIKA Suleiman Mwalim Abdallah wa KVZ ameonyesha dhamira ya kubeba kiatu cha dhahabu cha Mfungaji Bora wa Ligi Kuu Zanzibar (ZPL) kwa msimu huu, baada ya jana Alhamisi kuweka rekodi akitupia mabao manne wakati maafande hao wakiizamisha Maendeleo kwa mabao 7-3.

Mabao hayo manne yamemfanya nyota huyo wa KVZ kufikisha 19 na kuzidi kuwaacha washambuliaji wa timu nyingine zinazoshiriki ligi hiyo akiwamo Ibrahim Hamad ‘Hilika’ wa Zimamoto mwenye mabao 14 na aliyekuwa amepishana naye kwa bao moja tu kabla ya mechi ya leo.

Katika mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Amaan Kwa Wazee, uliopo nje ya Uwanja Mpya wa Amaan, mjini Unguja, Suleiman alifunga mabao mawili kila kipindi ikiwa ni hat trick ya kwanza kwake na rekodi kwa msimu huu kwa mchezaji mmoja kuifunga mabao manne katika mechi moja.

Suleiman alifunga mabao mawili ya chapuchapu dakika ya saba na tisa kabla ya Maendeleo kuchomoa moja dakika ya 19 kupitia Mboni Stephen Kibamba, bao lililozidi kuitia hasira KVZ kwa kucharuka zaidi na kuongeza mabao mengine.

KVZ iliongeza mabao mawili ikitumia dakika moja tu kupitia Sabri Dahar aliyefunga dakika ya 34 na Halifa Hassan Nolo kuongeza lingine dakika ya 35, kabla ya Kibamba kuifungia tena Maendeleo bao la pili dakika ya 41.

Dakika moja kabla ya mapumziko, Bagy Joseph Fundumo aliifungia KVZ bao la tano na kipindi cha pili kilipoanza iliwachukua maafande hao kuongeza bao la sita kupitia tena kwa Suleiman aliyekuwa akikamilisha hat trick dakika ya 48 kabla ya kuongeza jingine lililokuwa la nne kwake na la saba kwa KVZ dakika ya 56.

Maendeleo iliendelea kupambana na ilijipatia bao la tatu la kujifuta machozi lililowekwa kimiani na Rashid Bakar Msokeo dakika ya 66.

Hadi kipyenga kinapulizwa kuashiria kukamilika kwa dakika 90 za pambano hilo, KVZ ilikuwa wababe kwa ushindi huo mnono na mkubwa katika ZPL kwa msimu huu wa mabao 7-3 na kuifanya timu hiyo kuchupa kutoka nafasi ya tano hadi ya pili katika msimamo ikifikisha pointi 47.

Pointi hizo zilizotokana na mechi 24 zinalingana na ilizonazo Zimamoto iliyocheza michezo 23, ila zinaibeba KVZ kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa, huku JKU ikiwa kileleni mwa msimamo kwa kukusanya pointi 50 kutokana na kucheza mechi 23.

Mabao hayo manne aliyofunga Suleiman imemfanya afikishe 19, ikiwa ni matano zaidi na aliyonyo Ibrahim Hamad ‘Hilika’ wa Zimamoto aliyepo kwa sasa na kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars ambayo jana ilifungwa mabao 2-1 na Sudan katika mechi ya kirafiki ya kimataifa iliyopigwa Saudia Arabia mwenye mabao 14.

Nyota hao wawili wanaochuana kwa muda mrefu katika orodha ya wafungaji mabao kwa msimu huu wanafuatiwa kwa mbali na Ibrahim Is-haka wa KMKM na Yazidu Idd Mangosogo wa New City ambao kila mmoja akifunga 10.

Pia, hat trick hiyo ya Suleiman inakuwa ni ya tatu kwa msimu huu katika ligi hiyo baada ya awali, Hilika na Is-haka kila mmoja kufunga mabao matatu katika mechi ambazo timu wanazozitumikia ziliibuka na ushindi wa mabao 5-0.

Hilika alikuwa wa kwanza kufunga hat trick katika mechi ya ufunguzi wa msimu dhidi ya Ngome, iliyopigwa Septemba 13 mwaka jana kabla ya Is-haka kujibu mapigo siku watetezi wa ligi hiyo, KMKM ilipoibuka na ushindi wa 5-0 mbele ya New City.

Katika hatua nyingine, mabingwa wa zamani wa ZPL na Ligi Kuu ya Muungano, Malindi wamejikuta wakipoteza mechi mezani mbele ya Chipukizi ya Pemba baada ya kuadhibiwa na Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF) kutokana na tukio la kufanya fujo na kumshambulia mshika kibendera siku ya mchezo baina ya timu hizo na kusababisha pambano hilo kuvunjika kabla ya muda wake.

Kwa mujibu wa maamuzi yaliyotolewa na Kamati ya Mashindano ya Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF) ni kwamba Malindi imepoteza mchezo huo kwa pointi tatu na mabao mawili na kuifanya Chipukizi kufikisha pointi 35 na kuchupa kutoka nafasi ya saba hadi ya tano. Kwa adhabu hiyo, Malindi imeporomoka kwa nafasi moja kutoka nafasi ya nane iliyokuwako hadi ya tisa ikisaliwa na pointi 29 kutokana na michezo 24 sasa, huku ligi ikibakiza mechi za raundi sita kabla ya kufikia tamati katikati ya mwezi ujao.

Hilo ni tukio la pili katika Ligi Kuu Zanzibar kwa msimu huu, kwa timu kupata ushindi mezani kutokana na vurugu za uwanjani, kwani awali Kundemba iliyokuwa imefungana mabao 2-2 na Zimamoto zilipokutans mchezo Novemba 22 mwaka jana, iliadhibiwa pia kutokana na mashabiki wa timu hiyo kufanya fujo uwanjani na kumpiga mwamuzi hali iliyovunja pambano hilo.

ZFF iliizawadia Zimamoto ushindi wa pointi tatu na mabao mawili, huku wakiilima Kundemba pia, faini ya zaidi ya Sh 2 Milioni kwa utovu huo wa nidhamu.

Related Posts