Dodoma. Serikali imesema ushauri wa kuwarejesha papo kwa papo wahamiaji haramu wanapokamatwa utazingatiwa katika mapitio yanayoendelea ya Sheria ya Uhamiaji.
Naibu Waziri wa Mambo Ndani ya Nchi, Daniel Sillo ameyasema hayo leo Mei 17,2024 wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Mwasi Kamani.
Mwasi amehoji kama Serikali haioni haja ya kupitia sera, sheria, kanuni na taratibu ili kusimamia wahamiaji haramu tofauti na sasa wakikamatwa wanapelekwa magerezani.
Amesema kuwa jambo hilo linaipa Serikali mzigo mkubwa wa kuwahudumia, hivyo wabadilishe wanapokamatwa warudishwe papo hapo nchini kwao badala ya kupelekwa magerezani.
“Serikali ina mkakati gani kuhakikisha wanalishughulikia tatizo hili kwa haraka kwa kulinda mipaka yetu kwa uhakika,”amehoji.
Akijibu swali hilo, Sillo amesema Sheria ya Uhamiaji inafanyiwa mapitio na kuwa ushauri huo watauzingatia.
“Kuhusu mikakati ya kuzuia wahamiaji haramu ni pamoja na kufanya doria ya mara kwa mara ya wahamiaji haramu na kutoa elimu kwa umma kuhakikisha kuwa wanatambua majirani zao,”amesema.
Katika swali la msingi Mbunge wa Viti Maalum, Asia Halamga amehoji ipi kauli ya Serikali kuhusu wahamiaji haramu waliomaliza vifungo vyao na bado wako magerezani.
Akijibu swali hilo, Sillo amesema Serikali inaendelea na jitihada za kuwaondoa nchini wahamiaji haramu waliomaliza vifungo vyao magerezani.
Amesema katika kipindi cha mwaka 2022 hadi Aprili, 2024 jumla ya wahamiaji haramu 7,120 waliomaliza vifungo walioondolewa nchini.
Hata hivyo, amesema wahamiaji haramu 224 bado wapo magerezani na wote ni raia wa Ethiopia wakisubiri taratibu za kuondoshwa kwao zikamilike, ikiwemo kupata hati za kusafiria kutoka nchini mwao.