Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema kuna uwepo wa kimbunga “IALY” katika Bahari ya Hindi kaskazini mwa kisiwa cha Madagascar.
Tofauti na Kimbunga Hidaya, kimbunga IALY kwa mujibu wa TMA, kitaishia katika bahari ya Hindi katika eneo kati ya Madagascar na visiwa vya Shelisheli kwa siku nne zijazo.
Taarifa hiyo inakuja katika kipindi ambacho, Tanzania ipo katika kumbukumbu za maafa yaliyosababishwa na kimbunga Hidaya kilichotokea kuanzia Mei 2 hadi 5, mwaka huu.
Kimbunga Hidaya kilisababisha mvua zilizonyesha kwa takribani saa 36 zikiambatana na upepo mkali na kusababisha vifo vya watu watano na majeruhi saba, huku kaya 7,027 zenye watu 18,862 zikiathiriwa.
Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa nyumba 2,098 ziliathirika kati ya hizo, 678 zimebomoka kabisa, 877 zimeharibika kiasi, na 543 zimezingirwa na maji.
Kisiwa cha Mafia mkoani Pwani, ndicho kilichorekodi athari zaidi, baada ya shule zaidi ya 20 kuathiriwa na kimbunga hicho na mafuriko kwa pamoja.
Taarifa hiyo imetolewa leo Mei 17, 2024 ambapo imeeleza, “mifumo ya hali ya hewa inaonesha kuwa kimbunga hicho kitaendelea kusalia katika Bahari ya Hindi katika eneo kati ya Madagascar na visiwa vya Shelisheli kwa siku nne zijazo kabla ya kuanza kupungua nguvu.”
Aidha, kutokana na umbali kutoka nchini, kimbunga hicho hakitarajiwi kuwa na athari za moja kwa moja katika kusababisha ongezeko la mvua nchini.
TMA imeshauri watumiaji wa bahari na wananchi kuendelea kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri kutoka Mamlaka hiyo pamoja na kupata ushauri na miongozo ya wataalam wa kisekta.
Pia, TMA inaendelea kufuatilia mwenendo wa kimbunga hicho na athari zake kwa mifumo ya hali ya hewa hapa nchini ambapo imeahidi kuendelea kutoa taarifa.