Kiungo wa Simba, Saido Ntibazonkiza ameendelea kuwa lulu katika kikosi cha timu ya taifa ya Burundi baada ya kujumuishwa katika kundi la wachezaji 21 watakaotumika kwa mechi mbili za kuwania kufuzu Kombe la Dunia dhidi ya Kenya na Shelisheli mwezi ujao.
Ntibazonkiza ni miongoni mwa nyota wawili pekee kutoka Tanzania waliojumuishwa kwenye kikosi hicho cha Burundi huku mwingine akiwa ni kipa wa Namungo, Nahimana Jonathan.
Hakukuwa na nafasi kwa beki anayefanya vizuri wa Namungo FC, Mukombozi Derrick, pia Burundi imemfungia vioo kipa aliyeachwa na Mtibwa Sugar, Justin Ndikumana.
Kikosi hicho cha Burundi kinaundwa na idadi kubwa ya nyota wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi hiyo huku wachache wakiwa wanacheza nyumbani.
Matumaini makubwa ya Burundi yataendelea kuelekezwa kwa kiungo, Ndayishimiye Youssouf anayecheza OGC Nice ya Ufaransa, pia mshambuliaji Sudi Abdallah anayecheza Al Ittihad Misurata FC.
Nyota wa zamani wa Yanga, Bigirimana Gael anayeichezea Dungannon Swifts, naye ni miongoni mwa waliojumuishwa kikosini pamoja na nahodha msaidizi wa timu hiyo, beki Nsabiyumva Frederick.
Kocha Ndayiragije amewaita makipa Nkurunziza Matteo, Jonathan Nahimana pamoja na Bizimana Aladin wakati mabeki ni Nihorimbere Vaillance, Niyukuri Claus, Bukuru Keita, Nsabiyumva Frederick, Nshimirimana Ismail na Lucien Delaigle.
Viungo walioitwa katika tmu hiyo ni Ndayishimiye Youssouf, Henry Msanga, Elie Mokono, Naudts Jamir, Saido Ntibazonkiza, Donasiyano Irakoze, Akbar Muderi, Gael Bigirimana na Abeid Bigirimana.
Washambuliaji ambao wameitwa ni Shaban Hussein, Richard Kilongozi, Kamsoba Elvis, Amissi Mohamed, Sudi Abdallah, Bienvenu Kanakimana na Jordy Liongola.