MSHAMBULIAJI wa Yanga, Joseph Guede amezungumzia mambo manne yaliyomrejesha kwenye fomu haraka, huku akiweka wazi mipango yake msimu ujao.
Guede aliyetua Jangwani katika dirisha dogo la usajili lililopita, awali alionekana kuwa na mwanzo mgumu katika kikosi cha kocha Miguel Gamondi, lakini kadri muda unasonga ameonekana kubadili upepo kiasi cha kuwazidi kete mastraika Clement Mzize na Kennedy Musonda ambao amekuwa akigombania nao namba na hata vbaadhi ya viungo wa timu hiyo.
Mshambuliaji huyo aliyekaa nje ya uwanja kwa zaidi ya miezi mitatu tangu alipoachana na Tuzlaspor ya Uturuki, amehusika katika mabao matano kwenye Ligi Kuu Bara.
Akizungumza na Mwanaspoti amesema baada ya kuanza kazi kwa presha akitakiwa kuthibitisha ubora, wachezaji wenzake na makocha wa timu hiyo walikuwa upande wake wakimjenga kujiamini wakiamini kwamba mabao yake yatakuja tu.
Amesema licha ya presha kubwa iliyokuwa inamuandama, watu hao waliendelea kuwa na imani naye huku wakimpa mazoezi na mbinu tofauti zilizomsaidia kufanya vizuri.
“Kwanza makocha Gamondi (Miguel) na Mussa (N’daw) kwa pamoja wamekuwa na programu maalumu waliyokuwa wananipa ambayo imeongeza nafasi ya kurudisha kiwango changu mbele ya uso wa goli na kunirejesha kwenye ubora wangu wa kufunga,” amesema Guede.
“Wengine ni wachezaji wenzangu. Hakuna kitu bora kama wenzako waone kwamba una kitu licha ya kwamba nilikuwa nahitaji muda. Ilikuwa kila nikimaliza mazoezi au hata mechi unaona wananifuata na kunimbia kwamba mabao yatakuja au nikifunga mazoezini wanafurahi.”
Guede ameongeza kuwa ushindani na washambuliaji wenzake ulimuongezea presha na kuamua kupambana zaidi kwenye mechi za timu yao.
“Ilikuwa ukipewa nafasi ya kuanza unaona kabisa ili nipate nafasi mchezo ujao natakiwa kufunga hii mechi ya leo niliyopewa muda na kama ikitokea hujafunga na ukatolewa na aliyeingia akaja kufunga moja kwa moja inakunyima raha, hii ikanifanya kuongeza juhudi zaidi,” amesema.
Mshambuliaji huyo raia wa Ivory Coast amesema uwepo wa viungo bora wa ushambuliaji pia umemwezesha kufanya vizuri kwa kuwa alikuwa ana uhakika wa kufunga mabao akitengenezewa nafasi.
Katika mabao matano ambayo Guede ameifungia Yanga katika ligi ameonyesha ubora wa kukaa vizuri ndani ya eneo la hatari, akitengenezewa na mabeki Lomalisa Mutambala; viungo Khalid Aucho, Mudathir Yahaya huku washambuliaji wenzake Mzize na Musonda ambao kila mmoja amempa asisti moja.
Akizungumzia msimu ujao, Guede ameweka wazi mipango yake akisema kuwa anataka kuwa na kasi kubwa ya kufunga.
“Nimezoea mazingira na ushindani wa ligi ya Tanzania, hivyo msimu ujao ninausibiri kwa shauku kubwa, kwani nitaendeleza moto zaidi ili kuhakikisha naiwezesha timu yangu kupata mafanikio mazuri,” amesema.