Dar es Salaam. Balozi wa Marekani nchini, Michael Battle, amesema Tanzania ina haki ya kuitaka nchi yoyote inayochimba madini katika ardhi yake kuleta tija kwa kufanya uongezaji thamani.
Battle ameyasema hayo Mei 16,2024 wakati wa kuadhimisha miaka 15 ya kampuni ya Pula ya Marekani inayojishughulisha na uchimbaji wa madini ya kinywe mkoani Lindi.
“Serikali ina fursa ya kutouliza wala kuomba bali kuzitaka kampuni za sekta ya madini kuongeza thamani ya madini yanayochimbwa kabla ya kuyasafirisha nje ya nchi ili kupata thamani yake,” amesisitiza.
Battle amesema sekta ya madini Tanzania ni muhimu kwa mustakabali wa dunia kutokana na uwepo wa kinywe na aina nyinginezo. “Madini haya muhimu ambayo Tanzania imebarikiwa ni muhimu kwa mustakabali wa mabadiliko ya tabianchi.”
Waziri wa Madini, Antony Mavunde aliyehudhuria hafla hiyo aliunga mkono kilichosemwa na balozi Battle na kusisitiza kuwa msimamo wa Serikali ni madini yote ya kimkakati ni lazima yaongezwe thamani nchini ili Watanzania wanufaike.
Miongoni mwa manufaa aliyoyaelezea Mavunde ni ajira zitokanazo na shughuli za uongezaji thamani akisema kuuza malighafi nje ya nchi ni kuondoa ajira kwa Watanzania na kupunguza pato la nchi.
“Dunia inaelekea kwenye matumizi ya nishati safi ifikapo 2050, njia pekee ni kuongeza matumizi ya nishati zinazotajwa kuwa rafiki kwa mazingira. Tanzania ina malighafi za aina hiyo ya madini kwa wingi,” amesema Mavunde.
Mavunde amesema Tanzania ina kampuni nyingi zinazochimba madini ya kimkakati, na asilimia kubwa tayari zimeshaanza uchimbaji,
“Lengo la kwanza ni kuvutia wawekezaji katika madini ya kimkakati na pia kuhakikisha kuwa nchi yetu inanufaika,” amesema na kuongeza kuwa kila kampuni inayokuja nchini lazima iwe na mpango wa kuongeza thamani.