Kocha Mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi, amesema licha ya kufanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Simba, amekiri kuwa haikuwa rahisi huku akiwamwagia sifa mastaa wake kwa kufanya kazi kwa usahihi.
Gamondi amefunguka hayo muda mchache baada ya kukamilika kwa mchezo wa Kariakoo Dabi ambapo timu yake imefisha pointi 58 na kuendelea kujikita kileleni wakiwaacha Azam FC ambao wapo nafasi ya pili kwa tofauti ya pointi saba. Simba yenye pointi 46 katika nafasi ya tatu, imeachwa pointi 12.
Mbali ya kuwapongeza wachezaji wake kwa kufanya vizuri, lakini pia wamepiga hatua kubwa katika harakati za kutetea taji lao la Ligi Kuu Bara wanalolishikilia.
“Kupata matokeo mbele ya Simba sio rahisi, timu inatakiwa kupambana kutokana na mpinzani kuwa imara, na hicho kimefanywa na wachezaji wangu ambao walifuata maelekezo niliyowapa,” amesema na kuongeza;
“Siwezi kusema nani alikuwa bora kati ya wachezaji wangu, wote wameonesha ubora ambao sio rahisi kuonekana kama wote wasingekuwa na uwezo.
“Kiufundi wote wamenivutia kwani kila mchezaji ametekeleza majukumu yake na kinachofuata sasa ni kusonga mbele. Mchezo huu umemalizika, sasa uelekeo ni katika mechi zilizobaki ili kujihakikishia ubingwa msimu huu.”
Yanga imebakiwa na mechi nane, inatakiwa kupata ushindi katika mechi sita ili kufikisha pointi 76 ambazo hazifikiwa na Azam wala Simba, hivyo itatangaza ubingwa.