Hii hapa mikakati ya Simba ikifumuliwa, kusuka upya kikosi

SIMBA imekubali yaishe baada ya watani zao wa jadi Yanga kubeba ubingwa wa ligi kwa mara ya tatu mfululizo, jambo lililowaumiza Wekundu wa Msimbazi hao na sasa timu hiyo inaenda kufumuliwa na kusukwa upya kuanzia ngazi ya uongozi hadi chini kwa wachezaji kuhakikisha inarejea kwenye ubora wake.

Ni zaidi ya wiki mbili sasa zimepita tangu vikao vya siri vya ndani ya klabu hiyo kuanza vikilenga zaidi kujadili mabadiliko yatakayofanyika kuanzia kwa viongozi, benchi la ufundi na hata wachezaji lengo kuu ikiwa ni kurejesha heshima ya Simba.

Mwanaspoti kupitia vyanzo vyetu vya kuaminika limebaini baadhi ya mambo muhimu yanayojadiliwa kwenye vikao hivyo na vinavyoendelea vilivyokuwa vikihusisha viongozi, makocha na ya wachezaji kadhaa wa timu hiyo na hapa linakuchambulia baadhi ya maeneo yaliyopangwa kufumuliwa na kurejesha ubora wa Simba.

Moja ya mijadala inayowapa kigugumizi Wanachama na uongozi wa Simba ni kuhusu mfadhili na muwekezaji wa timu hiyo Mohamed Dewji ‘Mo’ kutoeleweka.

Wengi hawaelewi namna anavyotoa pesa hususani katika kipindi cha usajili na sasa inaelezwa tajiri huyo baada ya msimu huu kumalizika atarudi Simba kwa nguvu kubwa na atahusika kwenye usajili wa baadhi ya wachezaji na tayari ameanza kufanya hivyo.

Inaelezwa ‘Mo’ ndiye ametoa mkwanja uliombakiza Kibu Denis Simba zaidi ya sh 300 milioni na sasa anajipanga kuanza kulipa mwenyewe pesa moja kwa moja, baada ya kuhisi kuna ubabaishaji kwa baadhi ya wanaopewa dhamana hiyo.

“Tajiri anarudi na atasimamia moja kwa moja usajili msimu ujao, ameshtuka kuna wapigaji, mfano ishu ya Kibu kuna mtu alitaka kupiga pesa, Mo Dewji alitoa Sh 250 milioni, kuna kiongozi akampa Kibu Sh50 milioni na Sh200 milioni kaiweka mfukoni kwake, hilo lilimshangaza na kumkera ameamua kuingia mwenyewe kazini,” kimeeleza chanzo hicho.

Ukiachana na Mo, pia matokeo mabaya ya Simba yamemfanya mfadhili wa zamani wa timu hiyo, Azim Dewji ambaye ni ndugu wa Mo kuanza kufikiria kurejea Msimbazi msimu ujao na tayari mazungumzo yanaendelea.

“Sio Mo tu, hata ndugu yake Azim naye anarudi kuisapoti timu. Yule ni Simba haswa na ameomba baadhi ya miongozo ili msimu ukianza aweke pesa,” kimeongeza chanzo hicho.

Ndugu hao wawili kwa nyakati tofauti wamekuwa msaada mkubwa kwa Simba hususan kwenye mambo yanayohusu fedha ambapo wameidhamini nyakati tofauti.

Jambo lingine unalotakiwa kufahamu ni kwamba kutakuwa na mabadiliko kwenye ngazi ya uongozi ambapo Simba iko mbioni kumpa mkono wa kwaheri Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa timu hiyo, Imani Kajula.

Inaelezwa mwishoni mwa msimu huu Simba itaachana na Kajula ambaye alitua kikosini hapo Januari 26, 2023 akichukua nafasi iliyoachwa wazi na Barbara Gonzalez aliyejiuzulu Desemba 10, 2022.

Miongoni mwa sababu zinazotajwa juu ya kung’oka kwa Kajula ni pamoja na ushirikiano wake na watendaji wa sekretarieti ya Simba sambamba na wachezaji kuwa chini. Baadhi ya Wanasimba wanaamini Imani sio mtu wa ‘soka’, bali ni mbobezi zaidi katika masuala ya masoko na mawasiliano.

Simba inaendelea na mchakato wa kupata mrithi wa Kajula na miongoni mwa watu wanaopigiwa chapuo kushika wadhifa huo ni Barbara aliyejiuzulu nafasi hiyo 2022, lakini huenda mtaalamu kutoka nje ya Tanzania akashika usukani.

INAUNDWA KAMATI YA USAJILI

Jambo lingine linalokwenda kubadilika Simba ni kuundwa kwa kamati mpya ya usajili.

Katika miaka ya hivi karibuni kamati hiyo haipo hai ndani ya kikosi cha Simba, lakini sasa inakwenda kuwepo na kufanya kazi.

“Mfano sasa hatuna kocha, wala Mkurugenzi wa ufundi nani atasajili? Hapo kuna mdau akaleta hoja, kurejeshwa kwa kamati ya usajili na jambo hilo linafanyiwa kazi ikiwezekana ianze kufanya kazi haraka iwezekanavyo,” kilieleza chanzo hicho.

Mwanaspoti imeenda mbali na kumtafuta mwenyekiti wa zamani wa Simba, Hassan Dalali aliyegongelea nyundo jambo hilo akisema hiyo ndio chachu ya kusajili wachezaji bora.

“Bila kamati ya usajili utamuuliza nani endapo wachezaji watakaosajiliwa wakishindwa kufanya vizuri?” amehoji Dalali na kungeza:

“Nadhani Simba inatakiwa kuwa na kamati ya usajili ili kupata wachezaji wazuri. Lakini pia iwe na maskauti wengi watakaotafuta vipaji vizuri.

“Mfano enzi zangu walikuwepo vijana kama Maestoro ‘Ibrahim Masoud’, Saidi Tuli na wengine wengi, walizunguka kila sehemu kuangalia wachezaji na walitupa vipaji vingi. Simba irudi huko,” alisema Dalali.

Ishu nyingine iliyopo mezani kwa Simba ikiendelea kujadiliwa ni kuhusu kocha mkuu mpya wa kikosi hicho na inampango wa kumtambulisha kabla ya mwezi huu kuisha.

Tayari Simba imepokea wasifu wa makocha zaidi ya 15 wakiomba kazi kikosini hapo, ambapo kati ya majina yote hayo hakuna mzawa hata mmoja.

Simba imeendelea kuyachambua mdogomdogo na inatarajia kutangaza kocha atakayerithi mikoba ya Abdelhak Benchikha mwezi huu.

Hata hivyo jina la Juma Mgunda anayekaimu nafasi hiyo kwa sasa lipo mezani kwa Simba likijadiliwa juu ya kupewa timu hiyo kama viongozi hawataridhika ama kuafikiana na makocha wengine walioomba kazi.

CHAMA, SAIDO UAMUZI MGUMU

Usajili ndilo jambo ambalo wana Simba wengi wanasubiri kwa hamu kuona ukifanyika kikosini kwao.

Lakini pia wanatamani kujua hatma ya mastaa wa timu hiyo, ambao mikataba yao iko ukingoni wakiwemo viungo, Mzambia Clatous Chama na Mrundi Saidi Ntibazonkiza.

Mwanaspoti limepenyezewa Simba haina uhitaji wa wachezaji hao kwa msimu ujao na huenda wote wakaondoka.

“Kuna wachezaji wengi wataondoka kikosini, hata hao (Chama & Saido) wanaweza kuondoka pia, ni suala la muda,” kilieleza chanzo chetu.

Ofisa habari wa Simba, Ahmed Ally alisema wapo tayari kuachana na mchezaji yeyote ambaye haonekani kuwa na moyo wa kuitumikia timu hiyo.

“Tutafanya usajili mzuri na wa kishindo. Tutabaki na wachezaji wenye moyo na ari ya kuitumikia timu yetu na ambao tutaona hawako tayari kwa hilo basi tutaachana nao,” alisema Ahmed.

Ukiwatoa Chama na Saido, wachezaji wengine wa kigeni ambao wanaweza kuondoka Simba baada ya msimu huu kumalizika ni Babacar Sarr, Pa Omar Jobe, Sadio Kanoute, Luis Miquissone na Heneock Inonga.

Ofisa huyo ametamba kuwa Simba ya msimu ujao itakuwa na mabadiliko mengi yatakayorejesha heshima na mataji.

“Tunaendelea na mipango yetu kimya kimya, lakini niwahakikishie msimu ujao tutakuwa na mabadiliko mengi chanya na tutarejea kwenye ubora wetu. Hivi karibuni mtaanza kuona Sapraizi,” amesema.

Related Posts