Sugu arejesha fomu akitaja vipaumbele vitatu kuimarisha Chadema Kanda ya Nyasa

Mbeya.  Mgombea wa nafasi ya uenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Nyasa, Joseph Mbilinyi maarufu ‘Sugu’ ametaja sababu zilizomvuta kuwania kiti hicho, huku akitaja vipaumbele vitatu kati ya 10 atakavyotekeleza akishinda.

Sugu aliyewahi kuwa mbunge wa Mbeya Mjini anawania kiti hicho sambamba na mbunge wa zamani wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa anayetetea nafasi hiyo baada ya kumaliza muda wake.

Akizungumza leo Jumamosi Aprili 20, 2024 baada ya kurudisha fomu katika ofisi za kanda hiyo jijini Mbeya, Sugu amesema ameamua kubeba jukumu hilo kutokana na msukumo wa wanachama wanaotaka mabadiliko.

Amesema kutokana na kazi aliyoifanya kwenye chama, kwa uwezo na uzoefu wake hana hofu, akifanikiwa ataiongoza vema Chadema na kwa mafanikio makubwa kutokana na mikakati aliyojiwekea.

“Nilishafanya mengi na bado naendelea kufanya, kwa kuwa hiki ni chama chetu, nimevutiwa na nguvu ya wanachama waliotaka mabadiliko kwenye kanda,” amesema Sugu.

Kuhusu vipaumbele, amesema kwanza anataka kurejesha kanda hiyo kwa wanachama na sio kujifungia ndani kufanya uamuzi peke yake na kupuuzia mawazo ya wanachama.

Pili, amesema atakwenda kusimamia mkakati wa kusaka ushindi katika uchaguzi ujao wa Serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu na ule mkuu wa mwakani sambamba na kusimamia programu ya Chadema Digitali.

“Lazima tulete imani kwa wananchi na wadau wanaotuchangia, wajue fedha zao zinafanya nini, siyo tunasubiri viongozi wa Taifa ndio tunaleta rekodi kwa kuwafurahisha, bali tuwe na uhalisia mapema, tusimamie mkakati wa ushindi kwa vijana wa hamasa kwa kufanya maandalizi ya uchaguzi,” amesema Sugu.

Pia, amesema atasimamia uunganishaji wa oganaizesheni ya chama kwa kujenga ofisi za kanda, majimbo na kata.

Sugu amesema hata kabla hajafikiria kuwania nafasi hiyo alishanunua kiwanja na kuchora ramani kwa ajili ya ofisi za kanda na kutoa mafunzo kwa viongozi wa chama hicho.

“Nilipanga hadi Desemba mwaka jana niwe nimeamsha msingi na nguzo, lakini kwa figisu tulizopata kwa baadhi ya watu wakieleza kuwa mchakato huo ukikamilika Sugu atapata sifa na kuweza kuharibu kura zao, naamini mkinipa ridhaa ndani ya siku saba mchakato utaanza tena,” amesema Sugu.

Hakusita kuwashukuru makada waliojitokeza kwa wingi kutoka mikoa mitano ya kanda hiyo yenye majimbo 31 akieleza kuwa ushirikiano wao kwake unaakisi uhitaji wa mabadikiko ya uongozi.

Imeshuhudiwa viongozi wa mikoa hiyo wote wakiambatana na wajumbe mbalimbali wakijitokeza kumuunga mkono kada huyo wakieleza matumaini yao kwake katika kuongoza Kanda hiyo.

Katibu Mkuu wa chama hicho Iringa,  Leonard Kulwijira amesema kwa sasa wanahitaji mabadiliko na Sugu ndiye kiongozi mwenye maono kutokana na mahitaji yao kwa sasa.

Amesema ni mambo mengi ameyafanya Sugu na tayari ameonesha nia ya kukitumikia chama kutokana na uwezo kiuchumi jambo linalompa sifa kushika wadhifa huo.

“Kwa kipindi hiki cha mabadiliko Sugu ndiye anatosha, ameshafanya makubwa na bado anaonesha nia ya dhati kukitumikia chama na ana uwezo kiuchumi kufanya mambo mengine,” amesema Kulwijira.

Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Mbeya, Masaga Pius amesema wameamua kumuunga mkono mgombea huyo kutokana na rekodi alizonazo katika chama za mafanikio aliyoonesha.

Amesema wakati wakielekea kwenye uchaguzi, mgombea huyo ana nguvu kubwa ya kuwasaidia ushindi kuanzia Serikali za mitaa hadi uchaguzi mkuu wa mwakani.

“Sababu ni nyingi sana kumuunga mkono Sugu, hakuna asiye mjua kwa umaarufu, uwezo na uzoefu wake katika siasa,  tunataka mabadikiko na yeye ndiye anaweza kutufaa,” amesema Pius.

Mwenyekiti wa chama hicho Wilaya ya Ludewa, John Maponda amesema wanahitaji mabadiliko na mtu sahihi ni Sugu ambaye anaweza kuwavusha kwa kuwa katika majimbo 31, wanaweza kushinda 28.

“Naamini kwa uwezo wako katika siasa nguvu uliyonayo katika chaguzi zote kwa majimbo 31, wale wengine wakijitahidi watapata japo tatu zilizobaki tutachukua sisi,” amesema Maponda.

Related Posts