Iwe isiwe, Kwa Mkapa kitawaka

UBABE, soka la kasi na burudani ndani na nje ya uwanja vinatarajiwa katika mchezo wa Dabi ya Kariakoo unaopigwa leo kuanzia saa 1:15 usiku kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam kwa Yanga kuikaribisha Simba katika mchezo huo wa Ligi Kuu Bara.

Mechi ya raundi ya 23 kwa msimu huu na wa 114 kwa timu hizo kukutana Bara tangu mwaka 1965, inatajwa moja ya dabi ya kusisimua kutokana na timu zote kuwepo katika mbio za ubingwa, huku wageni Simba wakiwa na deni mbele ya watani wao wanaoshikilia taji la Ligi kwa misimu mitatu sasa.

Kwa aina ya vikosi vilivyopo na ushindani huo wa kuwania ubingwa ni wazi Kwa Mkapa kitawaka, kwani hakuna timu itakayotaka kuwa mnyonge kwa mwenzie na hivyo dakika 90 za pambano hilo litakalochezeshwa na mwamuzi mwenye beji ya Fifa, Ahmed Arajiga ndizo zitakazoamua mbabe.

Simba iliyo chini ya kocha Fadlu Davids inashuka Kwa Mkapa ikihitaji mambo mawili mbele ya Yanga nayo si mengine ni kushinda ili kulipa kisasi baada ya kupoteza duru la kwanza kwa bao 1-0 kisha ushindi huo upunguze gepu la pointi dhidi ya watani zao hao wa jadi.

DABI 01

Kwa upande wa Yanga inayofundishwa na Miloud Hamdi, inataka kuendeleza ubabe wao lakini pia kujitanua zaidi kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara kwani hivi sasa inaongoza kwa pointi 58 ikiiacha Simba yenye 54.

MATOKEO YATAMAANISHA NINI?

Wenyeji Yanga wanahitaji kushinda ili kuusogelea ubingwa inaoufukizia ili ibebe kwa msimu wa nne mfululizo, lakini kuwa la 31 kwa ujumla tangu mwaka 1965 katika ligi hiyo, kwa ushindi utaifanya ifikishe pointi 61 na kuiacha Simba kwa tofauti ya pointi saba na kusaliwa na mechi saba mkononi.

Katika michezo hiyo saba, Yanga itahitaji kushinda michezo sita ili kujihakikishia ubingwa bila ya kuangalia wapinzani wanafanyaje kwani itafikisha pointi 79 ambazo hazitafikiwa na timu yoyote hata Simba inayoshika nafasi ya pili.

Simba yenyewe hesabu zao kubwa ni kupunguza pengo la pointi, huku ikikichungulia kiporo dhidi ya Dodoma Jiji watakachokicheza nyumbani Machi 14, 2025 ili kuwabana wapinzani wao hao.

DABI 02

Kwa sasa Simba ina pointi 54, hivyo ikishinda mchezo huu itafikisha 57, ikimaanisha tofauti yao na Yanga itakuwa pointi moja pekee. Hiyo itawafanya Simba kupambana kwa nguvu kubwa kuifunga Dodoma Jiji katika kiporo chao ili kurejea kileleni kwa tofauti ya pointi mbili.

Kocha Fadlu anapambana kushinda kwa mara ya kwanza mbele ya Yanga baada ya kupoteza mechi mbili zilizopita, wakati Miloud Hamdi akitaka kuendeleza rekodi bora ya mtangulizi wake Miguel Gamondi aliyeinyanyasa Simba mara nne kati ya mechi tano alizocheza nao. Tatu za Ligi Kuu na moja Ngao ya Jamii huku pia akipoteza moja ya Ngao ya Jamii katika mechi ya kwanza kabisa.

Katika ligi msimu huu, Yanga ndio timu iliyopata ushindi mechi nyingi (19) ikifuatiwa na Simba iliyoshinda 17. 

Ukiweka kando rekodi hizo, wawili hao katika kukutana katika ligi hii itakuwa mara ya 114 ambapo Yanga imeshinda 41 na Simba ikishinda 32, sare zikiwa 40.

Imeshuhudiwa Yanga ikiifunga Simba mara nne mfululizo katika michuano ya Ligi na Ngao ya Jamii, mara ya mwisho Simba kushinda ilikuwa Agosti 13, 2023 kwa changamoto ya mikwaju ya penalti katika fainali ya Ngao ya Jamii iliyochezwa Uwanja wa Mkwakwani, Tanga. Baada ya hapo, Yanga imeshinda 5-1 (ligi kuu), kisha 2-1 (ligi kuu), 1-0 (Ngao ya Jamii) na 1-0 (ligi kuu).

DABI 03

Matokeo ya mechi tano za mwisho kwenye ligi, Yanga imekusanya pointi 13 baada ya kushinda nne na sare moja, haijapoteza kama ilivyo kwa Simba lakini Wekundu hao wa Msimbazi wamekusanya pointi 11 zilizotokana na ushindi mara tatu na sare mbili.

Kuna wasiwasi mkubwa katika kambi ya Simba kufuatiwa wachezaji wawili wanaounda kikosi cha kwanza, kipa Moussa Camara na beki wa kati Che Fondoh Malone waliopata maumivu kwenye mechi ya Mzizima Dabi dhidi ya Azam, Februari 24  na kuukosa mchezo uliopita dhidi ya Coastal Union.

Wasiwasi huo ukiwa umetanda, kocha mkuu wa Simba, Fadlu Davids amebainisha kuwa wanaweza kucheza kulingana na itakavyokuwa mazoezi ya mwisho yaliyofanyika jana Ijumaa.

Kwa upande wa Yanga, Stephane Aziz Ki ndiye ameonekana kutokuwa fiti kwa kiwango kikubwa lakini beki wa kulia, Yao Kouassi amerejea mazoezini baada ya kuwa nje kwa muda mrefu. 

DABI 04

Hata hivyo, kurejea kwa Yao hakutoi nafasi ya moja kwa moja kuanza mchezo wa leo kufuatiwa uwepo wa Israel Mwenda anayefanya vizuri tangu atue kikosini hapo kipindi cha usajili wa dirisha dogo uliofungwa Januari 15 akitokea Singida BS akifanikiwa kucheza mechi zote saba za Yanga tangu ligi kurejea Februari 28 mwaka huu.

Safu ya ulinzi ya Simba itakuwa katika wakati mgumu zaidi dhidi ya wachezaji wa Yanga wanaocheza eneo la ushambuliaji hiyo inatokana na rekodi zilivyo.

Ukiangalia katika mabao 58 yaliyofungwa na Yanga, nyota wao wawili wanaosimama mbele, Clement Mzize na Prince Dube jumla wamefunga 20 kila mmoja akiwa na 10. Si kufunga tu, hata kutengeneza mabao jamaa hao wapo vizuri, Dube akiwa na asisti 7 huku Mzize anazo tatu.

DABI 05

Nyuma yao wanapocheza viungo, Pacome Zouzoua naye amekuwa vizuri katika mchango wa mabao akifunga saba na asisti sita, Aziz Ki ana mabao saba na asisti 7, huku Maxi Nzengeli naye akifunga manne na asisti tano. 

Ubora huo wa safu ya ushambuliaji ya Yanga, ndiyo unaifanya timu hiyo kuwa tishio kwa wapinzani huku ikiwa ndiyo yenye mabao mengi zaidi.

Lakini hata Simba wapo vizuri katika kushambulia hata kuzuia ikiwa ndio timu iliyoruhusu mabao machache (8), lakini imefunga 46 kinara akiwa kiungo mshambuliaji Jean Charles Ahoua mwenye mabao 10 na asisti sita, pia nyota huyo ni fundi wa kupiga penalti kwani kati ya tano alizopiga amefunga zote. 

DABI 06

Hivyo leo Yanga wakijichanganya na kusababisha mkwaju wa penalti, kuna asilimia kubwa nyavu zao kutikiswa kutokana na ubora wa wapigaji wa Simba.

Leonel Ateba na Steven Mukwala, ndiyo washambuliaji vinara wa Simba, kila mmoja ana mabao manane, lakini Mukwala ana asisti mbili huku Ateba hana. Pia Mukwala katika mabao manane hana la penalti, hiyo inaashiria kwamba ni mshambuliaji hatari mwenye uwezo wa kufunga bila kutegemea mipira ya kutengwa wakati Ateba amefunga nne akikosa moja kati ya penalti tano alizopiga.

Pia uwepo wa Elie Mpanzu wa Simba ambaye hii ni Kariakoo Dabi yake ya kwanza, kuna kitu kinakwenda kuongezeka ndani ya Simba kufuatia makali yake aliyoyaonyesha tangu aanze kucheza alipoingia dirisha dogo akifunga mabao mawili na asisti mbili kwenye ligi akicheza mechi tisa tena zote akianza kikosi cha kwanza. 

Ukali wa safu za ushambuliaji kwa kila mmoja, utaufanya mchezo huu kuwa na mashambulizi yasiyopoa muda mwingi kwani kila mmoja ana uwezo wa kufika kwa mwenzake na kuweka hatari lakini safu zao za ulinzi pia zipo imara. 

DABI 07

Wakati vita kubwa ikiwa katika ushambuliaji na ulinzi, pale kati pia kuna watu nao wana vita yao, viungo wa Simba, Yusuph Kagoma na Fabrice Ngoma ambao ndiyo wamekuwa wakicheza mara kwa mara, wanakwenda kupambana na Khalid Aucho ambaye ana uhakika wa kuanza huku Duke Abuya au Mudathir Yahya mmoja wao akitarajiwa kuungana naye au wote kwa pamoja.

Ukiangalia viungo hao wamekuwa imara katika kusaidia mashambulizi na hata kushambulia kwani Ngoma tayari amefunga mabao matatu kutokana na kucheza juu zaidi kuliko Kagoma ambaye anatumika zaidi katika kulinda ndiyo maana hajafunga wala kuasisti. Kwa Yanga, Mudathir ana asisti mbili na mabao  mawili kama ilivyo kwa Duke akifunga mawili na asisti mbili huku Aucho akifunga bao moja.

DABI 08

Kocha wa Yanga, alisema hii ni dabi ya kwanza akiwa nchini, lakini sio mgeni wa mechi za aina hiyo kwani ameshacheza dabi mbalimbali hivyo ni mzoefu, japo anajua mchezo utakuwa mgumu.

“Wachezaji wote wapo fiti kujiandaa na mchezo, mchezaji pekee ambaye nina wasiwasi nae ni Aziz Ki ambaye alipata shida ya mgongo. Siwezi kusema kama atakuwepo au hatakuwepo bado ni 50/50 nafikiri mpaka kesho nitakuwa na majibu sahihi,” alisema.

“Hii sio dabi yangu ya kwanza, nimewahi kucheza dabi ambayo ilikuwa na mashabiki tarkibani 120,000. Siwezi kuwa na presha. Isipokuwa tu naheshimu wapinzani wangu nasubiri mchezo mzuri na wa kuvutia. Mashabiki waje kupata burudani wasiwe na presha.”

Fadlu alisema anajua mchezo utakuwa mgumu, lakini malengo ya Simba ni kupata matokeo mzuri baada ya kupoteza katika dabi mbili zilizopita za msimu huu, huku akisema wachezaji wapo tayari kuipigania timu uwanjani.

“Maandalizi kwa wiki yamekwenda vizuri na kila mchezaji yupo tayari kucheza akiwa na morali kubwa akitaka kuonyesha alichonacho ili kusidi timu kupata matokeo mazuri,” alisema Fadlu aliyeiongoza timu huyo katika mechi 21 za Ligi msimu huu na kushinda 17, kupata sare tatu na kupoteza mchezo mmoja dhidi ya Yanga siku ya Oktoba 19, 2024.

Related Posts