KWA sasa kuna kelele nyingi kuhusu Yanga kuifunga Simba mara nne mfululizo, lakini kama hujui ni, Simba iliwahi kuhenyeshwa kwa miaka mitano ikicheza mechi 12 mfululizo bila kuonja ushindi wowote mbele ya watani wao.
Balaa hilo kwa Simba lilianzia Septemba 5, 1981 hadi ilipokuja kujikomboa Agosti 23, 1986 huku ikiwa imecheza mechi 12 mfululizo ikitoka kapa, kwani ilipasuka mara sita na kuambulia sare sita, huku ikifungwa jumla ya mabao 17 na yenyewe kufunga sita.
Ukombozi wa Simba ulipatikana katika mechi ya 13 iliyopigwa Agosti 23, 1986 pale Edward Chumila na Malota Soma kila mmoja alipofunga katika kipindi cha mchezo huo na kuizidi Yanga iliyotangulia kwa bao la mapema kupitia Omar Hussein ‘Keegan’. Ndipo Simba ikaja kufunika ilipoikimbiza Yanga katika mechi 15 mfululizo ikiwa ni rekodi iliyoendelea kuishi iliyoweka kati ya mwaka 2000-2008.