Kissa Kyamba, mwanamke pekee kiwanda cha magazeti MCL, safari ya miaka 20

Dar es Salaam. Wakati kelele za mashine nzito za kuchapisha magazeti, harufu ya wino ikitanda kila kona ya kiwanda, Kissa Kyamba amesimama kando ya mtambo mkubwa, macho yake yakifuatilia kwa umakini harakati za vyombo hivyo vilivyokuwa vikichapisha kurasa kwa kasi.

Miaka 20 nyuma alipovuka lango la Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) kwa mara ya kwanza, hakuwahi kufikiria kuwa angeweza kudumu katika mazingira hayo ya kazi, akiwa mwanamke pekee kati ya wafanyakazi 25.

“Sikuwahi kufikiria kuwa ningeweza kufanya kazi hii kwa muda wote huu,” Kissa anasema na kueleza kuwa: “Nilijifunza, nikakubali changamoto na leo hii nipo hapa.”

Akikumbuka siku ya kwanza alipoingia kiwandani, anasema ujasiri wa kufanya kazi iliyojulikana kuwa ya wanaume ulimwezesha kuifanya kwa ufanisi na hakuwa mtu wa kukata tamaa.

Siku zilipita, miezi ikakatika na taratibu alianza kuelewa namna mitambo hiyo ilivyofanya kazi. Aliuliza maswali, alijifunza, na hatimaye kufika alipo sasa.

“Kuna wakati nilihisi kama ningekata tamaa, hasa pale nilipokutana na changamoto, lakini nilijipa moyo na kusonga mbele,” anasimulia Kissa.

Katika miaka 20 aliyofanya kazi, Kissa ameshuhudia mabadiliko mengi kutoka kwenye teknolojia za zamani hadi mashine za kisasa.

Safari yake haikuwa rahisi, lakini kwa bidii, nidhamu na uvumilivu, ameweza kuwa si tu sehemu ya tasnia hii, bali pia mfano wa kuigwa kwa wanawake wengi wanaotamani kuingia katika kazi zinazotawaliwa na wanaume.

Alijiunga MCL mwaka 2004 baada ya kuanzishwa kiwanda cha uchapishaji akiwa mtaalamu wa sanaa anayehamisha kazi kutoka kwenye kompyuta na kuzichapa katika bati maalumu (printing plate) ili zifungwe kiwandani kwa ajili ya kuzalisha magazeti.

Kissa, mhitimu wa Chuo cha Ardhi Tabora (Arita) katika fani ya Usanifu, Sanaa na Uchapishaji alichaguliwa kusoma fani hiyo kwa miaka miwili baada ya kumaliza Shule ya Sekondari ya Wasichana Kilakala mwaka 1994.

Anafanya kazi hiyo tofauti na ndoto alizokuwa nazo awali za kuwa daktari wa binadamu baada ya kumaliza shule.

“Nilitaka kusoma udaktari, nilipomaliza kidato cha nne nilipata daraja la tatu, nikaambiwa subiri chaguo la pili. Nilipoona hivyo niliandika barua nikapeleka Wizara ya Afya kuomba kusoma Chuo cha Afya Bugando. Niliambiwa nisubiri kwa mwaka mmoja ili nikasome medical assistant,” anasema.

Akiwa bado anasubiri mama yake aliyekuwa anafanya kazi Wizara ya Fedha, Ofisi ya Hazina siku moja akitoka kazini alifika nyumbani akiwa na gazeti akamwambia ameona jina lake amechaguliwa kusoma Chuo cha Ardhi Tabora.

Anasema mama yake alimtia moyo akamwambia ataweza na kama Serikali imemchagua ni vyema aende kuliko kukaa nyumbani mwaka mzima.

“Sikutia ugumu nikaona bora nikasome nilikochaguliwa, ukizingatia pia hali ya nyumbani haikuwa nzuri sana nikaamua kwenda wakati huo mama alifanya jitihada kuuliza watu tofauti kujua kwa undani kozi hiyo, wengi walimshauri kuwa ni nzuri,” anasema.

Kissa anaeleza wakati huo hakuwa anajua anakwenda kusoma nini, jambo lililomfanya kuuliza zaidi.

“Nilisoma kwa miaka miwili nikamaliza. Nilipomaliza tu kwa mara ya kwanza niliajiriwa Business Times, lakini Julai 2004 niliajiriwa Mwananchi,” anasema.

Kissa anasema katika utendaji kazi kwa muda wote huo amekuwa mtu asiyeruhusu kukata tamaa kwani safari hiyo imebeba milima na mabonde.

“Kuna wakati unatamani kuacha kazi, lakini Mungu anakupa moyo kuwa hakuna sehemu yoyote unayoishi isiyokuwa na makwazo jitahidi, nafanya hivyo,” anasema.

Hali hiyo imekuwa ikimjenga na kumfanya kujifunza namna bora ya kufanya kazi na watu, hasa baada ya kubaini kuwa kila mtu ana mawazo yake na utashi wake.

Hadi gazeti linakufikia kiganjani mwako, wapo watu nyuma yake ambao hulazimika kutumia muda mwingi kufanikisha hilo.

Kissa ni miongoni mwa hao ambaye kuna nyakati hulazimika kusimama kwa zaidi ya saa tano mfululizo bila kukaa, hasa uzalishaji unapoanza.

“Uzalishaji unapoanza ni kawaida mtu kusimama kuanzia saa 11:00 jioni hadi saa 5:00 usiku bila kukaa. Ukishaingia usiku hapa kama ni kusimama utasimama hadi kazi zinaisha, kwa sababu huwezi ukakaa halafu ukaongoza mashine ni lazima utembee, utumie mashine hii ukitoka unaenda kutumia nyingine,” anasema.

Hata hivyo, jambo hilo halijawa kikwazo kwake kwani sasa kazi hiyo imekuwa ile anayoipenda kutoka moyoni na anaifanya kwa moyo mmoja.

Kissa mama wa watoto wawili, akiwa nyumbani muda mwingi huutumia kuandaa bidhaa za biashara zake ndogo ndogo.

Anasema hatasahau tukio la uchungu wa kujifungua mtoto wake wa pili uliomuanza akiwa kazini usiku.

“Wakati huo sikuwa nimeanza kazi Mwananchi, ilikuwa Jumamosi nikiwa zamu. Kule tulikuwa tunachapa pia vitabu, siku hiyo wakaniambia zamu yako, basi nikaingia. Katikati ya kazi uchungu ulinishika nikapelekwa hospitali na kujifungua,” anasema Kissa.

Anasema kazi ya uandaaji bati maalumu kwa ajili ya uchapishaji inaenda sambamba na uchanganyaji wa rangi nne zilizopo katika gazeti husika ambazo ni cyan (bluu bahari), majenta (pinki nyekundu), njano na nyeusi.

Kuwa mwanamke pekee kiwandani anasema kunaakisi kilichokuwapo chuoni kwao, kwani darasani kulikuwa na wanaume 10 na wanawake wanne, lakini hadi walipomaliza walibaki wawili.

Hiyo ni baada ya mmoja wao kufeli na kushindwa kuendelea na masomo na mwingine kuondoka bila taarifa kamili.

“Ili kuvutia wanawake katika sekta hii ni kuwatia moyo na kuwatia nguvu, kuna watoto kutoka Veta walikuja hapa kufanya mafunzo kwa vitendo, waliponikuta walifurahi, hawakuamini kama wangekuta mwanamke,” anasema.

Anasema alitumia nafasi hiyo kuwatia moyo, akiwaeleza namna kazi zinavyofanyika ili wajue kuwa wanawake wanaweza kufanya kazi hizo kikamilifu kama walivyo wanaume.

Kissa anasema katika maisha hakuna jambo gumu wala jepesi ambalo unaweza kusema hiki nakiweza bali kila kitu ni kuamua.

“Ningependa kuona wasichana wengi wakijitosa katika fani mbalimbali bila hofu. Kama mimi niliweza, basi yeyote anaweza,” anasema.

Anasema ikiwa mtu ataamua kufanya kazi fulani ni vyema kutojiwekea kikwazo kwa kuona jambo hilo ni gumu, badala yake aweke nia na kuhakikisha anafanya kazi vizuri.

“Tusome, tusikimbie baadhi ya fani kwani wakati mwingine kina kaka kufanya kazi peke yao inawapa upweke. Kujichanganya na wavulana inaleta ahueni fulani, kina dada wapende kazi hii ni nzuri na fursa zipo,” anasema.

Anawataka wanawake kufanya kazi kikamilifu pale wanapopewa nafasi ili kuondoa dhana kuwa hawawezi baadhi ya vitu isipokuwa wanaume.

Eugen Collin, msimamizi wa kazi wa Kissa anasema licha ya kuwa mwanamke pekee amekuwa mtu anayejituma, mara zote amekuwa akienda nao sawa katika utendaji.

“Hawezi kusema hii kazi ya mwanamke na hii ya mwanaume hivyo hawezi kufanya. Amekuwa mwepesi kuwaelekeza wasiojua pindi wanapohitaji usaidizi,” anasema na kuongeza:

“Ni mtu asiyependa kukorofishwa, ana misimamo yake ambayo hataki iguswe. Wakati mwingine huwa tunajiuliza au kwa sababu ni mwanamke.”

Related Posts