Arusha. Mamia ya wananchi wa Mkoa wa Arusha na mingine ya jirani wamejitokeza katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake Duniani (IWD), ambayo kitaifa yanafanyika jijini Arusha.
Maadhimisho hayo yanafanyika leo Jumamosi Machi 8, 2025 katika Viwanja vya Sheikh Amri Abeid. Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.
Mageti ya uwanja yalianza kufunguliwa asubuhi saa 12:00 na tayari wananchi wameanza kuingia uwanjani.

Ndani ya uwanja wasanii wanaendelea kutoa burudani, huku viongozi kuanzia ngazi za wilaya hadi kitaifa wakiendelea kuingia.
Mkazi wa Arusha, Mwanaidi Abdallah amesema anatarajia Serikali itatoa msimamo kuhusu kukabiliana na vitendo vya kikatili dhidi ya wanawake.
“Kupitia siku hii ya wanawake tunatarajia Rais atatoa msimamo wa Serikali kuhusu kukabiliana na kupunguza vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake ambavyo vimekuwa vikitokea maeneo mbalimbali nchini,” amesema.

Kabla ya maadhimisho ya leo, jijini hapa kuanzia Machi Mosi, 2025 kumekuwa na maonyesho ya bidhaa na shughuli za wanawake, huduma za kisheria kupitia kampeni ya Mama Samia Legal Aid, utatuzi wa migogoro ya ardhi na masuala mengine.
Maadhimisho ya mwaka huu yanabebwa na kaulimbiu inayosema: “Wanawake na wasichana 2025: Tuimarishe usawa, haki na uwezeshaji.”
Usiku wa kuamkia leo, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha iliandaa tukio lililopewa jina nyama choma eneo la Clock Tower.

Mchoma nyama mkoani Arusha, akitumia jiko la nishati safi. Picha na Ally Mlanzi
Wananchi wengi walijitokeza, huku Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda akitumia tukio hilo kuwahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi katika maadhimisho ya leo.
“Nawasihi na kuwakumbusha kesho (leo Machi 8) tuingie mapema pale uwanjani kumpokea Rais wetu, ni heshima kubwa kwetu kuletewa maadhimisho haya kwa sababu tumenufaika na fursa mbalimbali za kiuchumi,” alisema.