Mbeya. Mmoja wa waliokuwa majeruhi katika ajali ya gari la Serikali na basi la CRN waliokuwa wakipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya ambaye ni mwandishi wa habari, Seleman Ndelage amefariki dunia.
Ajali hiyo ilitokea Februari 25 katika eneo la Shamwengo wilayani Mbeya ikihusisha gari la Serikali na basi la Kampuni ya CRN wakati wa hitimisho ya ziara ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi (CCM) Taifa, Fadhil Rajabu.
Kifo cha mwandishi huyo kinafanya idadi ya waliofariki kwenye ajali hiyo kufikia watano huku majeruhi wengine wakiendelea kupatiwa matibabu.
Siku ya ajali, watu watatu walifariki dunia papo hapo ambao ni pamoja na mwandishi wa habari, Furaha Simchimba, mjumbe wa kamati ya utekelezaji CCM Wilaya ya Rungwe, Daniel Mselewa na Utingo wa basi la CRN, Isaya Geazi.
Hata hivyo, vifo viliongezeka baada ya dereva wa mkoa, Thadei Focus kufariki akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Mkoa wa Mbeya.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na uongozi wa Dream Media, Ndelage amefariki wakati akiendelea kupatiwa matibabu katika hospitali hiyo na wanaendelea na taratibu za mazishi.
Taarifa hiyo imefafanua kuwa mwili wa mwandishi huyo unatarajia kuagwa kesho Jumapili Machi 9, 2025, kisha kusafirishwa kwenda nyumbani kwao mkoani Njombe kwa ajili ya kumpumzisha Jumatatu, Machi 10, 2025.
Katika hatua nyingine, kati ya majeruhi waliokuwa wamelazwa hospitali, tayari waandishi wawili, Epimarcus Apolnali na Denis George wameruhusiwa kutoka hospitali baada ya afya zao kuimarika.
Endelea kufuatilia tovuti ya Mwananchi na mitandao ya kijamii kwa taarifa zaidi.