Mwinjuma Muumin: Simba wamuache Arajiga afanye kazi yake…. Amgusia Aziz Ki

Msanii wa muziki wa dansi, Mwinjuma Muumini ‘Kocha wa Dunia’ amesema baadhi ya mashabiki wa Simba na vigogo wa klabu hiyo wamekuwa na shaka na refa Ahmed Arajiga aliyeteuliwa kuwa mwamuzi wa kati wa mechi ya Simba na Yanga, jambo ambalo halina mashiko.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mwinjuma amesema wasimtie presha mwamuzi Arajiga, wamuache achezeshe kwa haki ili dakika 90 apatikane mshindi kihalali sio kwa ajili ya kumbugudhi bugudhi kwa kumuweka kwenye shinikizo ili aipendelee Simba.

“Nazungunza hivi sababu, nimemuona kaka yangu Kassim Dewji hivi karibuni akizungumzia kuwa na shaka na refa Arajiga, mie nishauri tu wasimtie presha Arajiga wamuache achezeshe mechi, Arajiga huyo huyo wamesahu mwaka 2021 kwenye fainali ya FA kule Kigoma, Yanga walifungwa 1-0 na Simba, katika mchezo ule Mukoko Tonombe alitolewa kwa kadi nyekundu baada ya kumjibu kwa vitendo John Bocco ambaye alikuwa akimchezea rafu mara kwa mara, Mukoko alivyokuja kujibu tu rafu ile, akatolewa kwa kadi nyekundu. Refarii alikuwa huyo huyo Arajiga.

“Na mwaka huu 2025 katika mechi mbili tulizopoteza, ile dhidi ya Azam, Ibrahim Bacca alitolewa kwa kadi nyekundu na ukiangalia kadi aliyoonyeshwa ilitokana na tukio la ‘fifte fifte’ sio faulo ya moja kwa moja, lakini Arajiga alivyoona hii ya kutoa kadi nyekundu akaitoa bila ya kujiuliza. Kwahiyo wasitake kumuweka sasa kwenye shinikizo ili awapendelee hao Simba, wamuache Arajiga mwamuzi achezeshe kwa haki ili dakika 90 apatikane mshindi kihalali, sio kwa ajili ya kumbugudhibugudhi,” amesema Mwinjuma.

Mechi ya Kariakoo Dabi imeingia utata, baada ya uongozi wa Simba kutoa taarifa rasmi ukisema hautashiriki mchezo huo kutokana na watu wa Yanga kuwazuia wachezaji wao kufanya mazoezi ya mwisho kwenye uwanja wa mechi siku moja kabla ya mechi kwa timu mgeni kama kanuni zinavyoeleza.

Aidha, Muummini alimpongeza kiungo wa timu yake anayoishabikia ya Yanga, Stephane Aziz KI kwa kumuoa shabiki wa Simba, Hamisa Mobetto, lakini akasisitiza hamini kama staa huyo wa Ivory Coast atashuka kiwango kwa kuoa kama inavyosemwa na baadhi ya watu.

“Watu huwa na shaka kwasababu mchezaji hatakiwi kushiriki sana tendo la ndoa, yaani kama sisi tu wanamuziki hasa mpiga drums, ukiona mpiga drums anapiga lile goti lisijae maji, anatakiwa akae mbali na hayo mambo, na ndio maana wachezaji mpira mara nyingi kama kesho kuna mechi hawatakiwi wakutane na wenzawao, ilimradi waweze kuwa fiti asilimia mia moja, lakini mimi naamini Azizi KI sio limbukeni wa mapenzi.

“Azizi KI tayari ameshakomaa na muda mrefu alikuwa na huyo mke wake Hamisa Mobetto kabla hawajahalalisha kwa ndoa, alikuwepo naye na bado alikuwa anafanya vizuri, na naamini saa hizi atakuwa na raha zaidi sababu tayari ana ndoa, anajilia vya halali atafanya vizuri zaidi kuliko huko nyuma, kwahiyo sina shaka naye, sababu wachezaji wengi wameoa na wanafanya vizuri, ila kama hujitambui kazi yako ukiendekeza mahaba basi huwezi kuwa fiti uwanjani, kwahiyo bado naamini Hamisa atulindie shemeji yetu afanye vizuri ili asiwape maneno watu, maana hapo nyuma watu wa Simba walikuwa wanasema wamempa Aziz KI binti mrembo Hamisa kwa makusudi ili ammalize kwenye uchezaji, lakini ndio kwanza unasikia Aziz KI anapiga goli mbili, hat-trick wala sina wasiwasi,” amesema Muumini Mwinjuma.

Related Posts