Nachingwea. Chama Kikuu cha Ushirika cha Runali kimetoa msaada wa vifaatiba katika Hospitali ya Wilaya ya Nachingwea ili kupunguza changamoto ya wagonjwa kusafiri umbali mrefu kutoka wilayani humo hadi Hospitali ya Ndanda mkoani Mtwara kwa ajili ya kupata huduma hizo.
Chama hicho cha ushirika kinachojumuisha wilaya za Ruangwa, Nachingwea na Liwale, kimetoa msaada huo kikilenga kuwapunguzia wananchi adha ya kusafiri umbali mrefu kutafuta huduma hizo, jambo ambalo limekuwa likiwagharimu kwa kuwapoteza ndugu zao.
Akizungumza na Mwananchi jana Ijumaa Machi 7, 2025, Mwenyekiti wa Runali, Odas Mpunga amesema wameamua kutoa vifaatiba kwa watoto njiti na wajawazito vyenye thamani ya Sh44 milioni ili kurahisisha huduma.
Amesema vyama vya ushirika vimekuwa na tabia ya kurudisha kwa jamii, hivyo Chama cha Runali kimeamua kukabidhi vifaatiba.
“Sisi Runali tumeona faida tunayoipata turudishe kwa jamii, ndiyo maana tumetoa vifaatiba hivi vyenye thamani ya Sh44 milioni ili viwasaidie wajawazito pamoja na watoto njiti. Awali, watoto njiti na wajawazito walikuwa wanapelekwa Hospitali ya Ndanda iliyopo mkoani Mtwara,” amesema Mpunga.
Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hosptali ya Wilaya ya Nachingwea, Emanuel Kambei amesema wanakishukuru Chama cha Ushirika cha Runali kwa kuwapatia vifaatiba kwa kuwa, wagonjwa walikuwa wanapata shida kwenda Hospitali ya Ndanda mkoani Mtwara.
“Hospitali yetu ilikuwa haina mashine ya Ultrasound pamoja na mashine ya kukuzia watoto njiti, tunawashukuru sana Runali kwa kutupa msaada huu wa vifaatiba, utapunguza changamoto ya kwenda umbali mrefu,” amesema Dk Kambei.
Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Mohamed Moyo amewataka wauguzi na viongozi wa hospitali hiyo kuhakikisha vifaa hivyo vinatumika ili wananchi waondokane na adha ya kwenda umbali mrefu.
“Niwaombe wauguzi na viongozi, vifaa hivi vikatumike kama ilivyokusudiwa, sio kuviweka hadi vinaingia vumbi, nendeni kawahudumieni wagonjwa ili kupunguza changamoto yao ya kwenda umbali mrefu, na pia wauguzi niwaombe kuwa na lugha nzuri mnapowahudumia wateja wenu. Ukiwa na lugha nzuri, hata mgonjwa anapona kwa maneno mazuri,” amesema Moyo.
Pili Omary, mkazi wa Nachingwea, ameishukuru Runali kwa kutoa msaada wa vifaatiba akisema awali, walikuwa wanalazimika kutembea umbali mrefu kufuata huduma hizo Hospitali ya Ndanda.
“Runali wametupa msaada mkubwa sana kwetu wananchi wa Nachingwea, tulikuwa tunapata shida sana za huduma za Ultrasound na mashine ya kukuzia watoto njiti, tunashukuru sana kwani changamoto hiyo kwa sasa imemalizika,” amesema Omary.