Yanga, Simba yaahirishwa, kupangiwa tarehe nyingine

Mechi ya watani wa jadi kati ya Yanga na Simba iliyokuwa imepangwa kuchezwa leo Jumamosi Machi 8, 2025 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa imeahirishwa rasmi na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB).

Uamuzi huu umetokana na sintofahamu iliyotokea baada ya klabu ya Simba kuzuiwa kuingia uwanjani kwa ajili ya kufanya mazoezi ya mwisho kuelekea mchezo huo, jambo ambalo klabu hiyo ililalamikia kama ukiukwaji wa kanuni za ligi. 

Baada ya kupitia malalamiko ya Simba, Bodi ya Ligi ilibaini kuwa kulikuwa na dosari katika utekelezaji wa taratibu za matumizi ya uwanja, ikiwemo ushiriki wa watu waliovaa sare za Yanga katika kuziba njia ya Simba kufanya mazoezi.

Pia, taarifa za usalama zilionesha kuwa kulikuwa na matukio mengine yaliyohitaji uchunguzi zaidi ili kuhakikisha haki inatendeka kwa pande zote mbili. 

Kutokana na hali hiyo, Bodi ya Ligi kupitia Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi imeamua kuahirisha mchezo huo hadi uchunguzi wa kina utakapokamilika na maamuzi sahihi kufanyika.

Tarehe mpya ya mchezo huo itatangazwa mara baada ya uchunguzi huo kukamilika ili kuhakikisha haki na usawa vinazingatiwa katika uendeshaji wa ligi.

Endelea kufuatilia Mwanaspoti.

Related Posts