Dar es Salaam. Ripoti mpya imebaini kuwa vijana wa Kitanzania wana ustahimilivu mkubwa wa kiakili, wakipata alama za juu zaidi ikilinganishwa na wenzao katika nchi 76 zilizofanyiwa utafiti duniani kote hata hivyo watu wazima wana utulivu zaidi.
Hayo yamebainishwa na ripoti ya Mental State of the World 2024, iliyotolewa na taasisi mashuhuri kwa utafiti wa afya ya akili, Sapien Labs.
Kituo cha Utafiti wa Ubongo na Akili cha Sapien Labs (CEREBRAM) kilichopo katika Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Afrika ya Nelson Mandela (NM-AIST) iliyopo jijini Arusha, kimeeleza sababu za vijana wa Tanzania kuwa na ustahimilivu kwa kiwango hicho.
Kituo hicho kimekusanya takwimu kutoka kwa watu zaidi ya 5,000 kutoka makabila mbalimbali ya Tanzania, jamii na maeneo tofauti ili kuelewa athari za mazingira katika ubongo na akili.
Ripoti hiyo, pia ilichambua zaidi ya majibu milioni moja kutoka mtandaoni katika nchi 76 duniani, matokeo yanaonyesha kuwa Tanzania ni nchi pekee ambayo wastani wa Mental Health Quotient (MHQ) kwa vijana wenye uwezo wa kutumia intaneti unazidi 70.
Hata hivyo, ni muhimu kutambua kuwa pamoja na ustahimilivu huo, takwimu za vijana wa Kitanzania bado ziko chini ikilinganishwa na wastani wa utulivu wa akili wa kundi la watu wazima duniani kote.
Katika nchi zote, vijana wana afya duni ya akili kulinganisha na vizazi vya zamani.
Katika nchi 15 pekee kati ya 79, wastani wa alama za MHQ kwa vijana ulizidi 50, na ni katika nchi moja pekee ya Tanzania, wastani wa MHQ ulizidi 65, sawa na wastani wa chini zaidi wa nchi zilizo na watu wa umri wa miaka 55+.
“Takwimu za Tanzania zinakinzana na hali ilivyo katika nchi za Magharibi, ambako ustawi wa kiakili wa vijana umekuwa ukidorora kwa kasi tangu 2019, bila dalili za kuimarika. Kuporomoka kwa afya ya akili duniani kunahusishwa na kushuka kwa uwezo wa kudhibiti na kurekebisha mawazo na hisia, pamoja na ugumu wa kuunda na kudumisha uhusiano chanya miongoni mwa,” inaeleza sehemu ya ripoti hiyo.
Sababu zinazosababisha takwimu bora za ustawi wa kiakili kwa vijana wa Kitanzania zinaweza kuhusishwa na mambo kadhaa hasa ulaji wa vyakula vya asili, udhibiti wa mifuko ya plastiki na kiwango kidogo cha sumu itokayo viwandani kwani uchumi wa nchi unategemea zaidi utalii na kilimo.
Sababu nyingine kuu inayowanufaisha vijana wa Kitanzania ni kiwango kidogo cha matumizi ya simu janja wakiwa na umri mdogo na muda mfupi wanaotumia kwenye simu jambo ambalo pengine linasababishwa na usambazaji mdogo wa huduma za mtandao wa kasi.
Sababu nyingine muhimu inayosaidia vijana wa Kitanzania kuwa na ustahimilivu mkubwa wa kiakili ni kwamba nchi ina utamaduni wa kijamii zaidi, wenye msisitizo mkubwa katika mafungamano ya kifamilia na urafiki.
Mwanzilishi na Mwanasayansi Mkuu wa Sapien Labs, Dk Tara Thiagarajan, amesema Afrika ina fursa ya kipekee katika afya ya akili ya vijana wake, na ni rasilimali ambayo lazima ilindwe kikamilifu ikizingatiwa kuwa kwa sasa bara linapitia mabadiliko makubwa ya kiteknolojia na kiuchumi.
“Kwa kuwa idadi kubwa ya vijana wa Afrika inatarajiwa kuwa mhimili wa uchumi wa dunia katika miongo ijayo, Serikali zinapaswa kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha kuwa uhamaji wa mijini, matumizi ya kidijitali na mabadiliko ya mtindo wa maisha hayaharibu ustahimilivu wa kiakili ambao kwa sasa unawatofautisha vijana wa Afrika na sehemu nyingine za dunia,” amesema Thiagarajan.
Matokeo ya ripoti hiyo yanapendekeza kuwa, mshikamano wa kijamii na kifamilia ulio imara, kuchelewa kwa matumizi ya simu janja na mwingiliano wa ana kwa ana wa kijamii huenda vinachangia katika viwango hivi vya juu vya ustawi wa kiakili.
Mambo haya, husaidia kujenga ustahimilivu wa kihisia, yamekuwa yakishuka katika mataifa yenye kipato cha juu kwa zaidi ya muongo mmoja uliopita, ambako mwingiliano wa kidijitali na utamaduni wa kujitegemea umechukua nafasi ya miundo ya kijamii ya kitamaduni.
Hata hivyo, kwa kadri Afrika inavyoendelea kuhamia katika maisha ya mijini na kupanua matumizi ya teknolojia, watafiti wanatahadharisha kuwa faida hizi zinaweza kufifia ikiwa hazitalindwa, jambo linaloweza kusababisha kuporomoka kwa ustawi wa kiakili kwa vijana kote barani.
Ripoti hiyo inaonyesha pengo linalopanuka la kizazi katika afya ya akili duniani kote.
Wakati watu wazima wa miaka 55 na kuendelea, wanaendelea kustawi, vijana wanakabiliwa na viwango vya juu vya msongo wa mawazo.
Matokeo ya hili ni kwamba, kadri kizazi cha wazee kinavyoondoka katika soko la ajira, tunakabiliana na kizazi kipya ambacho huenda kisiweze kukabiliana na shinikizo za maisha ya kila siku.
Ripoti inaeleza miongoni mwa athari za jambo hilo ni kupungua kwa tija, ongezeko la likizo za ugonjwa, kushuka kwa mshikamano wa kijamii na kuongezeka kwa wasiwasi na uwezekano wa ongezeko la vurugu katika maisha ya kila siku kutokana na kizazi ambacho hakina uwezo wa kiakili wa kukabiliana na changamoto.
“Kwa Tanzania, hili linatoa fursa na changamoto kwa pamoja, ni fursa ya kujifunza kutokana na mwenendo wa kimataifa na kuchukua hatua sasa ili kulinda ustahimilivu wa kiakili wa vijana wake,” amesema Thiagarajan, mwanasayansi wa wa Sapien Labs.