KAMATI ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi Kuu Bara (TPLB) imetangaza kuahirisha mchezo wa Kariakoo Dabi kati ya Yanga na Simba uliopangwa kuchezwa leo Jumamosi Machi 8, 2025, saa 1:15 usiku kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Kabla ya kuahirishwa kwa mchezo huo, Simba ilitoa tamko usiku wa kuamkia leo Jumamosi ikisema haitapeleka timu uwanjani kufuatia msafara wa kikosi chake kuzuiwa jana usiku kufanya mazoezi ya mwisho kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, ambapo kanuni zilikuwa zinawaruhusu.
Simba ilizuiwa na kundi la watu wanaodhaniwa ni mashabiki wa Yanga maarufu kwa jina la makomandoo, na ndiyo sababu ya kuchukua uamuzi huo.
Hata hivyo, baada ya sakata hilo, Yanga ambayo ndio wenyeji wa mchezo huo ilibainisha kuwa ratiba ya mchezo huo iko palepale na kama mechi haitachezwa leo, hawatakuwa tayari kucheza siku nyingine.
Baada ya mzozo huo, Bodi ya Ligi imetoa taarifa rasmi ya kuahirishwa mchezo huo ili kutoa nafasi ya kufanya uchunguzi zaidi ili kutoa uamuzi wa haki.
Taarifa iliyotolewa na Bodi ya Ligi imebainisha hayo kwa kueleza itatoa taarifa kamili ya tukio hilo sambamba na kutangaza tarehe ya mchezo huo.
Sehemu ya taarifa hiyo imesema: “Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) katika kikao chake cha leo Machi 8, 2025 ilipitia shauri la Klabu ya Simba kuzuiliwa kuingia kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa ajili ya kufanya mazoezi ya mwisho kuelekea mchezo namba 184 wa Ligi Kuu (Yanga na Simba) uliopangwa kufanyika kwenye uwanja huo leo kuanzia saa 1:15 usiku.
“Katika shauri hilo, Klabu ya Simba iliiandikia barua Bodi ya Ligi kueleza kuhusu tukio tajwa hapo juu, huku pia ikielezea nia yao ya kutoshiriki mchezo huo kwa sababu imezuiliwa kutumia haki yao ya kikanuni kama ilivyoanishwa kwenye kanuni ya 17:45 ya Ligi Kuu kuhusu taratibu za mchezo.
“Baada ya kupokea barua hiyo, Bodi ya Ligi iliwaagiza maofisa wake wa mchezo (ambao walishuhudia tukio hilo) kutuma taarifa ya tukio haraka ili hatua zinazostahili ziweze kuchukuliwa, ikiwemo kuitishwa kwa kikao cha dharura cha kamati ya uendeshaji na usimamizi wa Ligi.”