Dhana ya utawala wa sheria ambayo Tanzania tunaiheshimu na kuifuata japo sio kwa asilimia 100, inasisitiza hakuna mtu au taasisi iliyo juu ya sheria au nje ya sheria, lakini sasa hivi tunaona kama utawala wa siasa unashika hatamu.
Tukiacha siasa itawale badala ya sheria, utekelezaji wa sheria bila woga wala upendeleo unasahauliwa na itakuwa ni vigumu kuelezea kwa ukamilifu hasara ambayo utawala wa siasa utailetea nchi yetu tusiporudi kwenye msitari.
Mathalani, Ibara ya 13(6) (b) ya Katiba yetu ya mwaka 1977, inasema ni marufuku kwa mtu aliyeshtakiwa kwa kosa la jinai kutendewa kama mtu mwenye kosa hilo mpaka itakapothibitika kuwa ana hatia ya kutenda kosa hilo la jinai.
Sababu kubwa inayotolewa ni kuwa upelelezi wa kesi haujakamilika, sasa unajiuliza kifungu cha 131A (1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) kama ilivyorekebishwa mwaka 2022) kilitungwa kwa ajili ya kazi gani hasa?
Kifungu hicho kiko wazi kuwa kinazuia hakuna kesi itafunguliwa kama upelelezi haujakamilika, isipokuwa kwa makosa mazito kama mauaji, uhaini, usafirishaji dawa za kulevya na binadamu na wizi au unyang’anyi wa kutumia silaha.
Ukisoma kifungu kidogo cha (2) kinasema ikiwa upelelezi wa kesi kwa makosa yale yanayodhaminika haujakamilika, basi mshukiwa atapewa dhamana, lakini tunaona washukiwa wa makosa ya kimtandao wakinyimwa dhamana.
Acha kifungu hicho, ukisoma kifungu cha 4(3) cha CPA kinasema kama shauri ni la jinai, madai au kiutawala, basi ni takwa la lazima kesi ya jinai haitafunguliwa isipokuwa pale tu kesi ya madai imesikilizwa na kuamuliwa na Mahakama.
Tujiulize, hakuna kesi za madai ambazo hadi leo zinafunguliwa na watu wenye uwezo wa kifedha kwa kushirikiana na polisi na kuzigeuza kuwa za madai, tena washukiwa wa kesi hizo wakishikiliwa mahabusu hadi zaidi ya saa 24.
Ukisoma Katiba yetu ibara ndogo ya 6(e) inasema ni marufuku kwa mtu kuteswa, kuadhibiwa kinyama au kupewa adhabu zinazomtweza au kumdhalilisha, tujiulize mbona jeshi letu la Polisi linanyooshewa sana kidole? Wanaonewa?
Wakati tunasikia uwepo wa mahabusu kuteswa hadi kufariki, ibara ya 13(6)(d), inasema heshima ya mtu itatunzwa katika shughuli zote za upelelezi na uendeshaji wa mambo ya jinai ambazo mtu anakuwa chini ya ulinzi bila uhuru.
Waendesha pikipiki maarufu kama bodaboda, wanatakiwa kuwa na leseni, vyombo vyao viwe na bima na kuheshimu sheria za barabarani, lakini kuna ubishi wanavunja sheria waziwazi ikiwamo kubeba mishikaki mbele ya trafiki?
Kwa sheria ya Mamlaka ya Usafirishaji Ardhini (Latra), pikipiki za magurudumu matatu zinatakiwa kufanya biashara kwa kukodiwa, leo hii zinafanya biashara kama daladala tena zikibeba abiria hadi sita ilihali kihalali abiria ni watatu tu.
Madereva wetu leo hii hawazingatii sheria za usalama barabarani wawapo barabarani hadi wapewe ishara na madereva wenzao kuwa mbele kuna trafiki au kamera au anaheshimu tu sheria anapowaona askari wa usalama barabarani.
Sasa hivi matukio ya utekaji na kupotezwa kwa watu yameshamiri sana nchini kwetu, lakini raia wema wanashindwa kutofautisha kati ya ukamataji wa polisi na ule unaofanywa na magenge ya kihalifu kwa sababu staili ni ile ile.
Leo hii watu wanajichukulia sheria mkononi na kuwaadhibu wahalifu ikiwamo kuwaua kwa kuwachoma moto au kuwaponda kwa mawe, ukichunguza utabaini kuna kutepeta kwa mifumo ya haki jinai kuanzia polisi hadi mahakamani.
Nimetangulia kusema tunapaswa kusema tunapaswa kulinda utawala wa sheria kwa wivu mkubwa kwa sababu tukifanya uamuzi kwa kukiuka sheria, upendeleo (double standard) au kukomoa mtu au kikundi fulani, tunaipeleka kubaya nchi.
Utawala wa sheria ni nini? Kwa lugha ya kawaida kabisa ni kwamba hakuna mtu aliye juu ya sheria, kila mtu anawajibika kwa sheria.
Aristotle, aliyekuwa mwanafalsafa wa Kigiriki aliyeishi zaidi ya miaka 2,000 iliyopita, naye alitamka maneno haya kuwa, “utawala wa sheria ni bora kabisa kuliko utawala wa mtu binafsi,” hivyo tunapaswa kuulinda kwa wivu mkubwa.
Tangazo la Umoja wa Mataifa la mwaka 1948 kuhusu haki za binadamu linatahadharisha watu wanaweza kulazimika kuasi ili kupinga dhuluma, maonevu na ukandamizaji ambayo hutokea pale utawala wa sheria haupo.
Utawala wa sheria unaanzia kwa watawala na hili liliwahi kuelezwa na Lord Denning (1899 1999) ambaye alikuwa Jaji wa Uingereza na mwanamapinduzi ya sheria aliyepanua mtazamo wa Mahakama nyingi za Jumuia ya Madola.
Alisema hivi, “Once great power is granted, there is a danger of it being abused.” Kwa Kiswahili alisema, “Pale madaraka makubwa yanatolewa (kwa vyombo vya dola) basi ipo hatari kubwa kwamba yanaweza kutumiwa vibaya.”
Kuwabana wale walio madarakani ili wasitumie vibaya madaraka waliyopewa kisheria ndio hatua ya kwanza ya kusimika utawala wa sheria katika nchi yetu.
Kila tunachoamua dhidi ya vyama vya siasa kiwemo kwenye sheria na si hisia au utashi wa mtu.
Kwanza, sheria zinazotoa madaraka lazima zitafsiriwe na Mahakama kwa ukali mkubwa dhidi ya wale walio madarakani ili wasidhulumu au kukandamiza raia.
Pili, watawala wasikubaliwe kutenda chochote ambacho hakiko katika sheria.
Mwaka 1765 Lord Camden ambaye alikuwa Jaji Mkuu wa Uingereza alisema hivi kuhusu watawala kufuata sheria “lf it is the law, it will be found in our books. lf it is not to be found there, it is not law.” Kama ni sheria tutaiona kwenye vitabu.
Watawala wasipoheshimu sheria na kuzizingatia katika kila hatua na katika kila uamuzi wanaochukua, basi kama tangazo la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa linavyosema, fujo na maasi ya raia huwa ndio matokeo ya dhambi hii.
Katika nchi yetu kwenye miaka hii ya karibuni limekuja jambo la kutisha sana hasa kuanzia mwaka 2016, kuna mazingira sheria inawekwa pembeni pale inapoonekana kama itatekelezwa kutakuwa na hasara ya kisiasa.
Mathalan, kwanini leo kundi kubwa kama bodaboda na bajaji linavunja sheria wazi wazi na halichukuliwi hatua? Tulitunga sheria za nini? Kama tunaziweka pembeni kwa masilahi ya kisiasa, ni za nini?
Sheria ya vyama vya siasa ya mwaka 2019 inatoa ruksa na utaratibu kwa chama cha siasa kinachotaka kufanya mkutano wa hadhara au maandamano kufuata.
Ni vigumu kuelezea kwa ukamilifu hasara ambayo utawala wa siasa utailetea nchi yetu kwa sababu wale wanaopendelewa kisiasa wanalemazwa kwa kuwa watadai zaidi na zaidi bila kuridhika.
Uimarishwaji wa utawala wa sheria utatokana pia na sheria zenyewe.
Kwa maneno rahisi, sheria nazo lazima zifuate “sheria.”
Sheria kandamizi hazina uhalali wa kisheria. Sheria zinazokiuka Katiba ya nchi hazina uhalali wa kisheria. Utawala wa sheria kandamizi sio utawala wa sheria ninaozungumziwa hapa.
Tuulinde utawala wa sheria, tusipofanya hivyo huko mbele ni giza nene.