SHABIKI wa Simba aliyeonekana kuwa na hasira sana baada ya kupata taarifa ya kuahirishwa kwa mchezo wa Ligi Kuu Bara kati ya Yanga na Simba, amefichua kuwa ametumia kiasi cha shilingi laki tatu ili tu kuja kumshuhudia Elie Mpanzu, lakini imeshindikana.
Mnazi huyo wa Simba ambaye kwa hasira alizokuwa nazo aligoma hata kutaja jina lake, amesema ametoka mkoani Kagera kuja kushuhudia mchezo huo lengo ni kumuona Mpanzu ambaye ndiye nyota pekee mpya wa Simba aliyetarajiwa kuchezwa dabi yake ya kwanza baada ya ile ya kwanza kutokuwepo kufuatia kusajiliwa kipindi cha dirisha dogo.
“Nimeumia sana kuahirishwa kwa mechi hii, nimetoka Kagera ndanindani huko, nimetumia shilingi laki tatu kufika hapa, Simba ingetumia busara na kuingia mchezoni.
“Tunaoumia ni sisi na sio wao kwani tunatoka mbali kuja kuwaona wachezaji wetu, hili jambo walichukulie kwa uzito jamani.
“Kama mimi nimekuja kwa ajili ya kumuona Mpanzu, lakini nimeshindwa kwa sababu mechi haichezwi leo,” amesema shabiki huyo.
Mchezo huo ulipangwa kuchezwa leo saa 1:15 usiku kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, lakini umeahirishwa na Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi Kuu Bara (TPLB) kufuatia uamuzi wa Simba kugomea kucheza mechi ikidai imenyimwa haki ya kikanuni ya kufanya mazoezi kwenye uwanja wa mechi siku moja kabla.
Taarifa ya TPLB imesema kuwa mechi hiyo imeahirishwa ili Bodi ipate fursa ya kuchunguza zaidi undani wa tukio hilo na kusaidia kufanya uamuzi wa haki huku ikijipanga kupanga tarehe mpya ya mchezo huo.