Arusha. Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi amesema amani ya Taifa la Tanzania iko mikononi mwa wanawake.
Amewataka wanawake wasichoke kufundisha, kukumbusha na kukemea pale wanapoona amani inahatarishwa.
Dk Nchimbi amesema hayo leo Jumamosi Machi 8, 2025 wakati akizungumza kwenye kilele cha maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake (IWD) ambayo kitaifa inafanyika mkoani Arusha.
“Wanawake tunawaomba amani ya nchi yetu iko mikononi mwenu, msichoke kutufundisha, msichoke kutukumbusha, msichoke kutukemea kila mtakapoona tunahatarisha amani ya nchi yetu.
“Jukumu la amani ya nchi yetu ni la kina mama, sisi tutaendelea kuwa wanafunzi wenu na tutaendelea kuwasikiliza bila kujali umri wetu, bila kujali madaraka na nafasi zetu,” amesema.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda amesema katika maadhimisho hayo, wananchi wa Arusha na maeneo ya jirani wamenufaika na huduma mbalimbali ikiwamo za matibabu, uwezeshaji wananchi kiuchumi na msaada wa kisheria.
Ameshukuru viongozi wa dini Mkoa wa Arusha kwa kutoa ushirikiano kwa viongozi wa Serikali katika kutatua changamoto za wananchi.