Wakati Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara ikitangaza kuahirishwa kwa mchezaji wa watani wa jadi, Yanga na Simba uliokuwa uchezwe saa 1:15 usiku wa Jumamosi, Machi 8, 2025, Makamu wa Rais wa Yanga, Arafat Haji ameweka msimamo kuhusu kinachoendelea kwa sasa.
Amesema atakuwa mtu wa mwisho ndani ya klabu hiyo kuamini kwamba, Yanga itashiriki tena kwenye Kariakoo Dabi msimu huu zaidi ya mchezo uliopangwa kufanyika leo Machi 8, 2025.
Bodi ya Ligi imeahirisha mechi hiyo ya mzunguko wa pili iliyokuwa ichezwe katika Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Tayari Bodi hiyo imeeleza kuwa mashabiki waliokata tiketi kwa ajili ya kushuhudia mchezo huo, watarejeshewa fedha zao kupitia njia zile zile walizotumia kukata tiketi.
Uamuzi huo umefikiwa kufuatia uamuzi wa Simba kugomea kucheza mechi ikidai imenyimwa haki ya kikanuni ya kufanya mazoezi katika uwanja wa mechi siku moja kabla.
“Nitakuwa mtu wa mwisho kuamini kwa msimu wa 2024/2025 @yangaAfricansSC itacheza mchezo mwingine wa Derby zaidi ya uliokuwa umepangwa Machi 8, 2025,” ameandika Arafat kwenye ukurasa wake wa X.
Tayari uongozi wa Yanga umetangaza msimamo ukisema kuwa inatambua kuwa mchezo baina ya klabu hiyo na Simba uliopangwa kufanyika leo na kwamba, watapeleka timu uwanjani na kuwataka mashabiki kujitokeza kwa wingi.
Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe amesema kuwa kuwa timu hiyo itakwenda uwanjani hapo kama ratiba ya awali ilivyoonyesha.
“Kikosi cha Yanga kitawasili uwanja wa Mkapa saa 11:00 jioni kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wa leo wa Kariakoo Derby. Hakuna Kipengele,” ameandika Ally Kamwe.
Klabu ya Simba ililalamika kikosi chake kuzuiwa kufanya mazoezi kama kanuni inavyotaka timu mgeni kufanya mazoezi siku moja kabla ya mchezo katika muda uliopangwa.
Kwa mujibu wa kanuni, inaeleza kuwa ikiwa itabainika maofisa wa usalama wa Yanga walihusika kuizuia Simba kufanya mazoezi, kanuni ya 47 (1) inafafanua adhabu ambayo inaweza kupata.
“Klabu ina wajibu na jukumu la kuhakikisha kuwa wachezaji, viongozi, wanachama na wapenzi wake wanajiheshimu na hawajihusishi na vitendo vyovyote vya utovu wa nidhamu kama vile matusi, vitisho, vurugu, vitendo vinavyoashiria imani za kishirikina na vitendo vyovyote vingine visivyokuwavya kimichezo kwenye viwanja vya michezo.
“Klabu ambayo ashabiki/wachezaji/viongozi wake watafanya vitendo hivyo itatozwa faini ya Sh5 milioni na kwa makosa ya kujirudia, faini itatozwa kati ya Sh10 milioni na Sh20 milioni,” inafafanua kanuni hiyo.
Ikiwa Simba itabainika imegomea mchezo, kanuni ya 47(6) inafafanua kuwa adhabu kubwa ni timu kushushwa daraja.
“Klabu itakayoshindwa kupeleka timu uwanjani baada ya kuhudhuria kikao cha maandalizi ya mchezo kitatozwa faini ya Sh5 milioni na kushushwa daraja.
Kiongozi aliyeshiriki kutopeleka timu uwanjani atafikishwa kwenye Kamati ya Nidhamu au Kamati ya Maadili ya TFF,” imefafanua kanuni hiyo.
Kuhusu viingilio kwa mashabiki
Ofisa habari wa TPLB, Karim Boimanda amesema kuwa viingilio vya mchezo huo vitatumika katika tarehe ambayo utapangwa kuchezwa tena.
“Tiketi zinarejeshwa kwenye kadi na zitasalia hapo kwa hiyo zitakuja kutumika kwenye mchezo huu namba 184 siku ambayo utachezwa,” amesema Boimanda.