LICHA ya kwamba Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) kutangaza kuahirisha mchezo wa Kariakoo Dabi, timu ya Yanga imefika uwanjani kwa lengo la kucheza mechi hiyo iliyopangwa awali kuchezwa dhidi ya Simba.
Mchezo huo uliopangwa kuchezwa leo Jumamosi Machi 8, 2025 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, umeahirishwa na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) kufuatia uamuzi wa Simba kugomea kucheza mechi hiyo ikidai imenyimwa haki ya kikanuni ya kufanya mazoezi kwenye uwanja wa mechi siku moja kabla.
Yanga ambayo ilitoa taarifa ikisisitiza kuwa mechi hiyo iko pale pale na kwamba kama haitachezwa leo basi haitachezwa tena, iliwasili muda wa saa 10:30 jioni, huku msafara wao ukiongozwa na ving’ora vya polisi.
Baada ya kuwasili, moja kwa moja wachezaji wakaingia ndani kwa ajili ya maandalizi huku watu wakitaka kuona itakuwaje.
Wakati timu ikiwa imeingia uwanjani, mashabiki ambao nao waliingia wametolewa. Hata hivyo, sababu ya mashabiki hao kutolewa bado haijajulikana, huku wakiendelea kusimama nje ya uwanja.
Nyuso za mashabiki hasa wa Yanga zinaonyesha wazi kuwa bado hawakubaliani na hali halisi kuwa mchezo huo umeahirishwa huku ulinzi ukiimarishwa nje na ndani ya uwanja.