Dar es Salaam. Umewahi kujiuliza changamoto za msichana wa Kitanzania ni zipi? Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Girl Effect Rita Mbeba amezitaja kwa uchache akisema zikifanyiwa kazi jamii inaweza kubadilika.
Akizungumza kuhusu siku ya wanawake, Mbeba anasema vijana wengi hawafikishi malengo yao na wengi wao hawamalizi masomo yao kwa sababu jamii haitoi nafasi haiwapi nafasi kupata taarifa sahihi.
Changamoto yao nyingine ni imani potofu kwamba hakuna maendeleo kwa mwanamke ambaye hana elimu kubwa, hivyo anaishia kuolewa au kupata mimba akiwa bado mdogo jambo ambalo linaibua changamoto lukuki.
Amesema wasichana wa Kitanzania wapo wanaobakwa, wanaotekelezwa, wengine wanapata uzazi pingamizi, kutengwa na familia kutokana na hali yao huku wengine wakikosa nafasi ya kutoa maoni kama vijana.

“Unakuta kwa sababu mtu amekatisha malengo yake ya kielimu anakuwa na hali ngumu ya kiuchumi. Kwa wale wa kijijini unakosa taarifa ya fursa mbalimbali ikiwemo kujifunza ufundi, elimu ya fedha na mengineyo ya kumuinua kiuchumi,” amesema na kusisitiza kuwa wengi katika kundi hilo hawapati nafasi ya kupata elimu sahihi.
Mbeba anasema kupitia chapa yao ya Tujibebe, taasisi ya Girl Effect inatoa jukwaa kwa vijana kupaza sauti zao lakini pia kupata taarifa sahihi na maarifa muhimu.
“Madhara makubwa kwa msichana asiyewezeshwa ni mimba za utotoni, unyanyasaji ikiwemo kubakwa na kutengwa na fursa muhimu ikiwemo uongozi katika ngazi mbalimbali,” amesema na kuongeza kuwa hawana hata taarifa kuwa akipata mimba anaruhusiwa kurudi shuleni.

Amesema jamii inamwangalia mtoto wa kike kwa namna ambayo haimpi kipaumbele kuwa kiongozi hata kama hali inaimarika kidogo, lakini bado safari ni ndefu kwani kuna wajibu wa kuhakikisha wanawake wanapewa nafasi mbalimbali katika uongozi.
Ujumbe wake kwa wanawake katika siku hii ya kimataifa ya wanawake duniani, “kukiwa na taarifa sahihi, uungwaji mkono sanjari na mazingira rafiki ya kupata haki ya huduma za kijamii na uchumi wanawake watatoa mchango mkubwa katika uchumi wa nchi.”
“Tukipewa haki ya kupata huduma za afya, haki ya elimu, haki ya kujikwamua kiuchumi maana yake Taifa letu litakuwa na wanawake na wasichana wadogo wenye uelewa na uwezo wa kufanya vitu vikubwa katika nchi yetu, wanakuwa vitega uchumi na chimbuko la viongozi,” amesema.
Mbeba amesema uwezeshaji wa wasichana ni muhimu kwani asilimia kubwa ya watu nchini ni vijana na jukumu la tujibebe ni kubadilisha hali iliyopo kwa kuweka mazingira bora zaidi.